Amani Josiah; Kocha aliyejiwekea rekodi zake Bara
Muktasari:
- Josiah aliyewahi kufundisha pia timu mbalimbali zikiwemo za Tunduru Korosho, Biashara United, Geita Gold na maafande wa Tanzania Prisons kisha msimu huu Dodoma Jiji ameweka na kuandika rekodi za kuvutia.
UNAPOZUNGUMZIA miongoni mwa makocha bora nchini Tanzania hutoacha kulitaja jina la Kocha wa Dodoma Jiji Amani Josiah kutokana na uwezo mkubwa anaoendelea kuuonyesha katika mechi za timu hiyo na nyingine alizowahi kuzifundisha pia mwanzo.
Josiah aliyewahi kufundisha pia timu mbalimbali zikiwemo za Tunduru Korosho, Biashara United, Geita Gold na maafande wa Tanzania Prisons kisha msimu huu Dodoma Jiji ameweka na kuandika rekodi za kuvutia kama ambavyo Mwanaspoti linaelezea.
AVUNJA REKODI YA YANGA
Ushindi wa mabao 3-2 ulioupata Dodoma Jiji katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga Mei 13, 2026 umemfanya Josiah kuivunja rekodi ya mabingwa hao watetezi ya kucheza muda mrefu bila ya kupoteza tangu mara ya mwisho Novemba 7, 2024.
Kabla ya kichapo hicho Yanga ilicheza mechi 42 za Ligi Kuu Bara bila ya kupoteza kwa siku 552 ambazo ni sawa na mwaka mmoja miezi sita na siku sita, rekodi ambayo ilivunjwa na Dodoma Jiji wakati timu hiyo ilipochapwa 3-2 Mei 13, 2026.
Mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Liti Singida mabao ya Dodoma Jiji yalifungwa na Bakari Mwamnyeto aliyejifunga pia mwenyewe, Mwana Kibuta na Waziri Junior huku ya Yanga yakifungwa yote na kiungo mshambuliaji Mganda Allan Okello.
Dodoma Jiji ilivunja rasmi rekodi hiyo ya Yanga ya kucheza mechi 42 za Ligi Kuu Bara bila kupoteza tangu mara ya mwisho ilipochapwa na Tabora United sasa TRA United mabao 3-1, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex Novemba 7, 2024.
Rekodi nyingine ya Josiah aliyoweka ni ya Dodoma Jiji kupata ushindi wa kwanza wa Ligi Kuu dhidi ya Yanga tangu imepanda daraja msimu wa 2020-2021 baada ya kushinda 3-2 Mei 13, 2026 kwani kabla ya hapo ilichapwa mechi 10 na sare moja tu.
KOCHA WA KWANZA DODOMA JIJI
Suluhu ya 0-0 iliyoipata Dodoma Jiji dhidi ya Simba Februari 25, 2026 imemfanya pia Josiah kuandika rekodi mpya ya kocha wa kwanza kwa ‘Walima Zabibu’ kupata sare mbele ya kikosi cha Msimbazi tangu kimepanda rasmi kucheza Ligi Kuu.
Tangu Dodoma Jiji icheze Ligi Kuu msimu wa 2020-2021 mechi na Simba ilikuwa ni ya 11 ambapo kati ya hizo imepoteza 10 na kutoa sare moja huku kikosi hicho cha ‘Walima Zabibu’ kikifunga mabao mawili na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 22.
Josiah aliyejiunga na timu hiyo Oktoba 16, 2025 akichukua nafasi ya Mrwanda Vincent Mashami amekuwa ni kocha wa kwanza wa Dodoma Jiji kuandika rekodi ya kupata sare katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba tangu ipande rasmi daraja.
AIOKOA TZ PRISONS
Moja ya jambo la kukumbukwa kwa Kocha Josiah ni ya kuiepusha timu ya maafande wa Tanzania Prisons ya jijini Mbeya na kuepuka janga la kushuka daraja baada ya kutokuwa na mwenendo wa kuridhisha katika Ligi Kuu Bara msimu wa 2024-2025.
Josiah alijiunga na Prisons Januari 2, 2025 akitokea Geita Gold inayoshiriki Ligi ya Championship ambapo kocha huyo alichukua nafasi ya Mbwana Makata aliyeondoka Desemba 28, 2024 kutokana na mwenendo mbaya wa matokeo ya kikosi hicho.
Makata anayeifundisha kwa sasa Polisi Tanzania aliiongoza Prisons katika jumla ya mechi 14 za Ligi Kuu msimu wa 2024-2025 ambapo kati ya hizo alishinda mbili tu, sare tano na kupoteza saba akiiacha ikiwa nafasi ya 15 na pointi zake 11.
Kwa upande wa Josiah akaiongoza katika jumla ya mechi 15 za Ligi Kuu ambapo kati ya hizo alishinda sita, sare tatu na kupoteza sita huku akikiwezesha kikosi hicho kumaliza msimu wa 2024-2025 kikiwa nafasi yake ya 13 na pointi zake 31.
Baada ya Prisons kumaliza nafasi ya 13 na pointi 31 timu hiyo ikacheza mechi ya ‘Play-Off’ kusaka tiketi ya kubaki Ligi Kuu Bara ambapo katika hatua hiyo ilikutana na Fountain Gate ambayo msimu wa 2024-2025 ilimaliza ya 14 na pointi 29.
Katika mechi ya kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa Manyara timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 kisha ile ya marudiano jijini Mbeya Prisons ikashinda mabao 3-1 hivyo kikosi hicho kubaki Ligi Kuu kwa jumla ya mabao 4-2.
Kwa maana hiyo licha ya Josiah kuingia katikati ya msimu wa 2024-2025 ila ni miongoni mwa makocha walioweka rekodi ya kuvutia katika kikosi cha Prisons ambayo hadi leo itaendelea kukumbukwa baada ya kutokuwa na mwenendo mzuri msimu huo.
AIPANDISHA BIASHARA LIGI KUU
Moja ya kitu kitakachokumbukwa na mashabiki wa Biashara United ni baada ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo Amani Josiah kuipandisha rasmi Ligi Kuu Bara msimu wa 2017-2018 huku msimu huo ukiwa wa kihistoria baada ya kupoteza mechi mbili tu.
Msimu huo wa 2017-2018 Biashara United maarufu ‘Wanajeshi wa Mpakani’ ilimaliza mabingwa wa Ligi ya Daraja la Kwanza kwa sasa Championship nyuma ya Alliance ya jijini Mwanza iliyokuwa ya pili na Dodoma Jiji iliyomaliza nafasi ya tatu.
Baada ya kupanda Ligi Kuu Bara msimu wa 2018-2019 Biashara ikafundishwa na Mnyarwanda Hitimana Thierry aliyewahi pia kuzifundisha baadaye Simba, KMC FC na Mtibwa Sugar huku Josiah akiteuliwa msaidizi wake na meneja pia wa kikosi hicho.
Msimu huo wa 2018-2019 Biashara ilimaliza nafasi ya 14 katika Ligi Kuu Bara na pointi 45 baada ya kushinda mechi 11, ikitoka sare 12 na kupoteza 15 kati ya 38 iliyocheza huku safu yake ya ushambuliaji ikifunga mabao 30 na kuruhusu 35.
Biashara ilipata nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kumaliza nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2020-2021 ilipokusanya jumla ya pointi 50, ikishinda mechi zake 13, ikitoka sare 11 na kupoteza 10.
Katika ushiriki wa michuano hiyo ilienguliwa raundi ya pili baada ya kushindwa kusafiri katika mechi ya marudiano dhidi ya Al Ahly Tripoli ya Libya, mechi iliyopangwa kuchezwa Oktoba 23, 2021 kwenye Uwanja wa Martyrs Benina jijini Benghazi.
Sababu kubwa iliyoelezwa ilikuwa ni kukosa kwa wakati vibali vya Kimataifa vya Anga katika nchi za Sudan, Sudan Kusini na Libya ingawa ilishinda mechi ya kwanza kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam mabao 2-0 Oktoba 15, 2021.
Baada ya hapo timu hiyo ikakumbwa na jinamizi la kutofanya vizuri na kushuka kutoka Ligi Kuu Bara hadi Championship kwa msimu wa 2021-2022 ingawa hali imekuwa mbaya kutokana na kuporomoka hadi kucheza First League tangu msimu wa 2024-2025.
MECHI 34 BILA KUPOTEZA
Moja ya jambo unalopaswa kujua Josiah aliandika rekodi ya kipekee ya kuiongoza Polisi Mara ambayo kwa sasa ni Biashara United ya kucheza mechi 34 bila ya kupoteza msimu wa 2009-2012 kuanzia ikicheza Ligi ya Wilaya hadi Daraja la Kwanza.
Katika mechi hizo 34 Josiah alikiongoza kikosi hicho cha Polisi Mara ambacho kwa sasa ni Biashara United kushinda 26 na kutoka sare minane ikiwa ni kiwango kizuri kilichoonyeshwa na kocha huyo anayefanya mambo makubwa katika Ligi Kuu Bara.
ATWAA UBINGWA TUNDURU KOROSHO
Msimu wa 2021-2023 Josiah aliifundisha Tunduru Korosho kuanzia Ligi Daraja la nne hadi Daraja la pili ambapo alitwaa ubingwa wa Ligi ya Mkoa (RSL) iliyopigwa mjini Kigoma baada ya kuifunga Kurugenzi ya Simiyu kwenye fainali bao 1-0.
Pia Josiah alishinda Tuzo ya Kocha Bora ambapo akiwa Tunduru Korosho alicheza misimu miwili bila ya kupoteza jumla ya mechi 28, rekodi iliyovunjwa dhidi ya Mashujaa FC kwa kuchapwa bao 1-0 katika nusu fainali ya kupanda Daraja la Kwanza.
MSIKIE MWENYEWE
Akizungumzia mafanikio hayo, Josiah anasema siri kubwa ni kufanya kazi kwa weledi na ushirikiano wa watu wanaomzunguka, jambo ambalo limekuwa chachu ya kufika hapa alipo leo, licha ya changamoto mbalimbali ambazo ni za kawaida kwa binadamu.
“Katika safari ya mafanikio kuna milima na mabonde kwa kila mmoja wetu, nami pia ni sehemu hiyo ambayo naweza kusema wazi ndio iliyonifikisha hapa nilipo leo, uvumilivu na kutokata tamaa ndio chachu ya kutimiza malengo,” anasema Josiah.
Aidha, Josiah anasema licha ya hatua kubwa ya kisoka aliyofikia hadi sasa, ila bado anataka kufika mbali zaidi ya hapa, ndio maana amekuwa mstari wa mbele kujifunza mara kwa mara kwa makocha wengine waliopiga hatua katika karia zao za soka.