Barnabas: Ishu ya washambuliaji ni janga la kitaifa
Muktasari:
- Kocha huyo ambaye aliwahi kuichezea Mtibwa Sugar, Kagera Sugar na Yanga alikuwa mwiba mchungu kwa vigogo wa Kariakoo Simba na Yanga kutawala soka la vijana.
MIONGONI mwa makocha walioweka rekodi kwenye soka la vijana akiwa na Mtibwa Sugar ni Vicent Barnabas ambaye kwa sasa yupo na Yanga U-17 na U-20.
Kocha huyo ambaye aliwahi kuichezea Mtibwa Sugar, Kagera Sugar na Yanga alikuwa mwiba mchungu kwa vigogo wa Kariakoo Simba na Yanga kutawala soka la vijana.
Msimu uliopita alijiunga na Yanga akitokea Mtibwa na msimu huu tayari kachukua ubingwa wa vijana U-17 akibeba tuzo tatu za kocha bora, huku Ramadhani Ally akiibuka mfungaji bora na Emmanuel Ngunga akitwaa tuzo ya kipa bora huku Laurent Suleiman mchezaji bora (MVP) wakitokea katika timu hiyo.
Mwanaspoti ilifanya mahojiano na kocha huyo akizungumzia mambo mengi ikiwemo changamoto ya washambuliaji inayoonekana kuwa na shida hadi kwenye timu za vijana.
MALENGO YA YANGA
Anasema malengo makuu ya timu za vijana za Yanga kwanza ni kuhakikisha inakusanya makombe na kisha kutengeneza misingi ya vijana.
“Klabu kubwa kama Yanga haiwezi kununua wachezaji kila siku nje tena kwa gharama kubwa wakati sisi tuna vipaji vingi ambavyo vinaweza kushindana na wachezaji wa kigeni.”
“Kama wanaweza kufanya hivyo timu ya Mamelodi kumzalisha mchezaji akaja juu na kushindana na timu kubwa kwa nini isiwe Yanga, kwa hiyo kiu yetu ni kuwatoa kina Mzize wengi.”
NAMNA YA KUWAPATA
Utaratibu wa kuwapata vijana kwa Yanga kwanza wanawafanyia majaribio na kuwachambua kulingana na umri wao kisha kuwatumia kwenye U-17 na U-20.
“Hata kwa Yanga tumerudisha utaratibu kama ule wa Mtibwa kuwafanyia majaribio, wale tunaohisi tunaweza kwenda nao tunawachukua na kutengeneza timu,” anasema na kuongeza;
“Lakini hatutaenda nao kwa muda mrefu kwa sababu tukishatengeneza timu ambayo iko vizuri tunawatenganisha.”
Anaongeza, upo pia mpango wa kuwaongeza vijana watakaocheza vizuri kwenye mashindano na watasajiliwa moja kwa moja na Yanga wakitokea timu nyingine.
KILICHOBADILIKA
Barnaba anasema msimu wa kwanza hawakufanya vizuri kutokana na namna walivyozikuta timu hizo lakini sasa kuna utofauti.
“Wakati tunafika, viongozi wa Yanga waliweka imani na sisi, msimu wa kwanza huu tunawaachia mtengeneze timu angalieni watu mnaoweza kufanya nao kazi klabuni kisha mtupe matokeo chanya,” alisema Barnabas na kuongeza;
“Kwa hiyo maneno yao yalitupa moyo na tulipambana kuhakikisha msimu unaofuata tunarudisha imani kwao, nafikiri sasa angalau kidogo kuna afadhali.”
WASHAMBULIAJI
Anasema changamoto ya washambuliaji ni janga la kitaifa hivyo kama makocha wa vijana wanapambana kuhakikisha wanatengeneza mastraika wazuri.
“Ni kweli kabisa washambuliaji imekuwa tatizo na sio kwamba hatuna nchini, lakini kuna vitu vimepungua, hivyo na sisi huku chini tunajitahidi, tunaamini Yanga ikiwajenga vizuri, Mtibwa na timu nyingine watakuja kuwa msaada mkubwa kwa nchi.”
SIRI YA MATAJI
Mtibwa Sugar U-20 ilichukua ubingwa wa vijana mara tano mfululizo ikianza msimu wa 2018-22 wakati huo Barnabas akiwa kocha mkuu.
Anasema hakuna siri kubwa ya yeye kuchukua ubingwa mara tano mfululizo akiwa na Mtibwa isipokuwa kuishi na kukaa na wachezaji vizuri ambao kwa kiasi kikubwa ndio wamechangia kupata mafanikio hayo.
“Kikubwa tunajitahidi kuwafundisha vijana kuwa na nidhamu na namna ya uchezaji na wanatakiwa kuonyesha kipaji na tunawaambia wasiogope kukosea kwenye mpira jambo hilo lipo kwa hiyo kadri unavyowajenga na wenyewe wanakuwa huru na inakuwa rahisi kukupa matokeo.”
Anaongeza, jitihada hizo zimefanya watengeneze vijana wengi wenye uwezo mkubwa ambao wamekuwa na msaada kwenye klabu mbalimbali nchini na hata nje.
“Naamini kama mambo yatakwenda sawa basi tutawatengeneza wachezaji wengi mfano nyuma niliwafundisha kina Dickson Job, Kibwana Shomari na Aboutwalib Msheri ambao sasa ni tegemeo kwenye klabu zao,” anasema na kuongeza;
“Wapo pia kina Nassoro Saadun, Ladaki Chasambi, Pascal Msindo, Athuman Makambo na huwa najisikia faraja sana kuona wanacheza hata kama sio timu kubwa.”
CHANGAMOTO YA VIJANA
Barnabas anasema kama makocha wanapitia wakati mgumu wanapofundisha vijana ambao wanaamini baadae watakuwa bora badala yake wanapotea.
“Kumbuka vijana wengi ndio umri wao wa kukua kuna mambo mengi wanapitia ikiwemo uvutaji bangi, ulevi kiufupi mambo ya ujana na wengine wanapotea kabisa kwenye dira.”
“Shida ya vijana unaweza kumuamini mwisho wake unakuwa mbaya kama makocha tunapitia changamoto kubwa kwa sababu lazima uhakikishe anakaa kwenye mstari, wanapoanguka tunaumia sana.”
DABI NAYO
Dabi inayowakutanisha mahasimu wa Kariakoo haijawahi kuwa na jambo dogo kuanzia timu kubwa, vijana na hata zile za wanawake na hapa Barnabas anaeleza walivyowadhibiti na upande wa vijana.
“Kwenye U-17 tumeshinda michezo yote miwili ya nyumbani na ugenini lakini U-20 tulishinda moja 4-1 na sare jambo ambalo linawapa motisha vijana,” anasema.
“Kitu kizuri viongozi wanakuja kuitembelea timu na kuwapa moyo vijana sio tu kwenye mechi za dabi hata mechi nyingine na muda mwingine wanawaahidi bonasi kama wakishinda.”
HAJAWAHI KUFUNGWA NA SIMBA
Anasema aanze kufundisha timu za vijana akiwa Mtibwa Sugar hajawahi kupoteza mchezo wowote dhidi ya Simba, jambo ambalo anajivunia.
“Nadhani ndani ya misimu hiyo ambayo tumekutana na Simba sijawahi kufungwa zaidi ya sare ambazo sio nyingi na ji jambo ambalo linanifanya najivunia sana na kuendelea kupambana.”
ANGUKO LA MTIBWA
“Nisiwe muongo wakati Mtibwa inashuka daraja sikujisikia vizuri kwa sababu ni timu ambayo imetoa vijana wengi, tumepita mimi mwenyewe, Zuberi Katwila na Mecky Mexime.”
“Hata hivyo tunaendelea kuiombea irudi Ligi Kuu, najua Championship imeanza vizuri lakini walipo sasa siko ambako wengi tunapenda iwepo, msimu ujao itarudi.”
VIUNGO WAKE
Anawataja wachezaji ambao walikuwa bora wakati anacheza akiwemo Athuman Idd ‘Chuji’ na Amri Kiemba.
“Wakati mimi nacheza kulikuwa na wachezaji wengi wazuri napata wakati mgumu kuwataja lakini wapo kama Kiemba naheshimu alichokifanya akina Mwinyi Kazimoto na Mohamed Issa ‘Banka’.”
MZIZE HATARI
Anasema kama kocha kuwa na mshambuliaji aina ya Clement Mzize inakurahisishia kazi akitaja utajiri mkubwa alionao ni pamoja nguvu aliyonayo.
“Binafsi namkubali sana Mzize kuanzia nidhamu yake uwanjani hadi ubora alionao kwangu natamani aendelee kupambana na kuonyesha uwezo wake na jitihada.”