Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bruno ana tamaa, Manchester United ina tamaa?

PAZIA Pict

Muktasari:

  • Bruno Fernandes ameendelea kututafakarisha kuhusu pesa, lakini anatuachia maswali mengi

ALISEMA mwendawazimu mmoja. "Pesa sio kila kitu, lakini ni afadhali kulia ukiwa katika Mercedes Benz kuliko kulia ukiwa katika baiskeli". Ni wakati mwingine wa kuitafakari pesa. Pesa ni nini hasa?

Bruno Fernandes ameendelea kututafakarisha kuhusu pesa, lakini anatuachia maswali mengi. Majuzi Waarabu wa Saudia Arabia walikuwa wamemuandalia kitita cha Pauni 200 milioni katika mkataba wake kama angeamua kusaini na Al Hilal ya huko. Ni katika mkumbo uleule ambao wengi tunaufahamu. Mkumbo wa kuhamisha mastaa wakubwa wa Ulaya kwenda Saudia.

Mkumbo uliowanasa wengi tangu Cristiano Ronaldo aende Riyadh. Mkumbo ambao wakati mwingine unatuachia maswali kuhusu tabia binafsi za wachezaji, namna pesa inavyoongea na mengineyo. Bruno anakuwa mchezaji wa karibuni kukwepa ulimbo huo. Kabla yake Vinicius Junior wa Real Madrid aliukwepa mtego huo.

Pale Carrington, Bruno anapokea mshahara wa Pauni 250,000 kwa wiki. Chukua kikokotoo chako na kujumlisha mara tatu ya huo mshahara. Ndicho ambacho Waarabu walikuwa wanataka kumlipa Bruno kwa wiki. Pesa ndefu. Pesa chafu. Maisha yanataka nini zaidi? Bruno amekataa. Amekataa akiwa na umri wa miaka 30.

Kwa mujibu wa Bruno ni kwamba anataka aendelee kucheza soka la kiwango cha juu Ulaya. Ni kweli. Sisi wengine sio mashabiki sana wa kuona mastaa wakubwa kama yeye wanaenda Saudia. Tunataka kuona mastaa kama yeye wanaendelea kucheza kiushindani Ulaya tukiamini kwamba kwa sasa Ligi Kuu Saudia bado ni bonanza tu.

PAZ 01

Hata hivyo, swali la kujiuliza ni kwamba Bruno anataka kucheza soka la ushindani la kiwango cha juu akiwa na Manchester United hii hii au klabu nyingine kubwa? Tunaanza kwa kuulizana kwamba mchezaji kama yeye msimu ujao hatakuwepo katika Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara nyingine tena. Na kwa Manchester United hii bado hatuna uhakika kama atakuwepo tena katika Ligi ya Mabingwa Ulaya ule msimu mwingine.

Bruno ana tamaa. Manchester United yenyewe ina tamaa? Nani ana tamaa kubwa kuliko mwenzake? Mpaka sasa hatuelewi. Katika dirisha hili la uhamisho Manchester United wameanza kwa kishindo kwa kumchukua mshambuliaji wa Wolves, Matheauss Cunha. Ni Mbrazili huyu ambaye kwa sasa yupo katika kambi moja na kina Vinicius Jr.

Mwingine ambaye wanamfuatilia ni Bryan Mbeumo wa Brentford. Wote kwa pamoja tunakiri kwamba Manchester United imepata wachezaji wazuri ambao wamefanya vizuri katika Ligi Kuu England. Hata hivyo hii sio simulizi mpya kwa Manchester United. Wanapata wachezaji wazuri lakini timu inazidi kudumaa.

PAZ 02

Ni kama nuksi hivi. Tangu Sir Alex Ferguson aondoke zake United imeendelea kutumia pesa kununua wachezaji tu, lakini nwishowe wanaishia kuwa wachezaji wa kawaida na timu inaendelea kuwa ya kawaida. Msimu ulioisha, kama Leicester City na Southampton wangekaza kidogo tu basi Manchester United ingeshuka daraja.

Wamekuja kina Henrikh Mkhitaryan, Radamel Falcao, Jadon Sancho, Angel Di Maria, Memphis Depay, Alexis Sanchez, Anthony, Paul Pogba na wengineo. Walikotoka walikuwa na sifa kubwa. Walipokuja Old Trafford wakaonekana kuwa wachezaji wa kawaida tu. Mwishowe tukaendelea kukosa jibu lake swali letu maarufu.

Tukakosa jibu lake swali la nini ni tatizo la Manchester United. Benchi la ufundi, wachezaji au matajiri wa timu? Kuna wakati nakumbana na swali hilo, lakini nakosa jibu. Hakuna mwenye jibu kamili. Kama ni matajiri nadhani wamekuwa wakitoa pesa nzuri tu katika masuala ya uhamisho wa wachezaji. Kama ni wachezaji, mbona imekuwa ikisajili wachezaji wazuri.

PAZ 03

Kama ni mabenchi ya ufundi, tazama namna ambavyo United imekuwa ikibadilisha makocha wengi kulingana na mahitaji ya nyakati. Kuna wakati walitaka hadi makocha wakongwe wakaja kina Louis van Gaal na Jose Mourinho. Wakaja makocha wa 'project' kina Erik Ten Hag na Ruben Amorim. Ngoma bado inaonekana kuwa nzito.

Na hapo ndipo tunapomrudia Bruno. Amekataa pesa za Waarabu katika umri wa miaka 30 kwa sababu ya Manchester United hii au nyingine? Septemba anatimiza miaka 31. Ana uhakika Manchester United hii hii itamfikisha katika nchi ya ahadi au ana mpango wake mwingine ambao ameuficha katika mfuko wa nyuma wa suruali?

Mpaka sasa anachofanya Bruno ni kucheza kamari. Naelewa kinachomtokea. Mpira wa Ulaya ni mtamu. Pesa za Waarabu sio kila kitu kwa sababu kuna mengi yanasimama nyuma ya pesa hizo. Kuna hadi wachezaji ambao wameanza kuzitema hizo pesa na kurudi Ulaya au kwenda kwingineko. Hata aina ya maisha ya Saudi Arabia pia yanawatatiza.

Kwa sasa bila unafiki Bruno hayupo katika timu sahihi. Angekuwa katika zama za kina Dwight Yorke angekuwa katika timu sahihi. Hii ya sasa haimhakikishii sana ushindani. Bahati nzuri wanakuja kina Cunha lakini kwa mchezaji wa aina yake sidhani kama anahitaji tena mipango ya muda mrefu kwa ajili ya kupata mafanikio. Anahitaji mipango ya muda mfupi kuweza kupata mafanikio.

PAZ 04

Umri wake hauruhusu sana kusubiri 'project' mpya. Labda kama Manchester United itafanya haraka kuendana na tamaa zake. Sina uhakika sana kama usajili wa kina Cunha unamhakikishia kuwa na Manchester United yenye nyota njema msimu ujao. Kwa kuanzia tu kwanza ni kuwa hatakuwepo katika michuano ya Ligi ya Mabingwa msimu ujao.

Haya yote yanakwenda huku akiwa ameacha Pauni 200 milioni zikiwa zinaelea kule Saudia. Amefanya bahati nasibu ambayo wakati mwingine unaweza kumuelewa na wakati mwingine hauwezi kumuelewa. Kama akiendekeza hili unaweza kukuta mwisho wa siku anakosa kila kitu. Anaweza kukosa pesa ya kustaafia na anaweza kukosa mataji ya maana.

Mwishowe unajikuta unaangukia Galatasaray ukiwa na umri wa miaka 33 na kwenda kutwaa Ligi Kuu Uturuki. Historia huwa haikukumbuki sana kama ulikuwa mchezaji mkubwa kwa kutwaa taji la Ligi Kuu Uturuki. Wakati mwingine bora historia isikukumbuke lakini walau ulienda Riyadh na kubeba magunia ya dola.

Na ndipo ninapokumbuka kwamba wakati mwingine ni bora kulia ukiwa unaendesha Mercedes Benz kuliko kulia ukiwa unaendesha baiskeli. Ni ukweli mchungu kuhusu maisha yetu lakini tunapaswa kuukabili. Wengine wanaukubali wakiwa wana umri mdogo tu. Mfano ni kina Ivan Toney. Wapo wengi walioenda Saudia kwa staili hiyo.

PAZ 05

Unaweza usimlaumu Lamine Yamal kwa kukataa ofa ya Saudia. Unaweza usimlaumu Vinicius Junior. Lakini hapa kwa Bruno, na kwa timu ambayo yupo kwa sasa inaweza kuwa bahati nasibu tu. Labda kama angekuwa Barcelona au PSG ungeweza kumuelewa kwa haraka. Manchester United hii inapaswa kumsaidia kweli ili ahalalishe uamuzi wake.

Vinginevyo Septemba, mwaka huu tu tunaweza kuanza kumlaumu kwanini hakwenda zake Saudia. Labda Amorim afanye kazi nzuri zaidi. Labda kina Cunha walete mabadiliko mapya zaidi. Hapo ndipo tunaweza kuamini kwamba Bruno alikuwa sahihi kukataa dola za Riyadh.