Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

BWENZI: Bao la Diarra liliniheshimisha

BWENZI Pict

Muktasari:

  • Bwenzi aliyejiunga na kikosi hicho dirisha dogo la Januari mwaka huu akitokea Mbeya Kwanza inayoshiriki Ligi ya Championship, amepiga stori na Mwanaspoti na kuelezea mengi, ikiwemo bao kali alilomfunga kipa wa Yanga, Djigui Diarra.

SELEMANI Salum Bwenzi ni miongoni mwa nyota wanaofanya vizuri katika kikosi cha KenGold kutokana na uwezo anaoendelea kuuonyesha, baada ya kuchangia mabao sita ya Ligi Kuu hadi sasa, akifunga matano na kuasisti moja.

Bwenzi aliyejiunga na kikosi hicho dirisha dogo la Januari mwaka huu akitokea Mbeya Kwanza inayoshiriki Ligi ya Championship, amepiga stori na Mwanaspoti na kuelezea mengi, ikiwemo bao kali alilomfunga kipa wa Yanga, Djigui Diarra.


BAO LAKE KWA DIARRA LAMHESHIMISHA

Nyota huyu anasema licha ya kufunga mabao manne ya Ligi Kuu Bara hadi sasa, ila bao bora kwake lililompa heshima kubwa ni lile la mbali alilomfunga kipa wa Yanga, Djigui Diarra, wakati KenGold ilipochapwa mabao 6-1, Februari 5, mwaka huu.

“Iliniuma sana kuona tunapoteza mchezo kwa idadi kubwa ya mabao lakini baada ya kufunga lile bao lilinipa heshima ambayo sikufikiria kama ingetokea, mapokezi yalikuwa makubwa na ndipo nilipoamini nyota yangu inaanza kung’aa upya,” anasema.

Bao la nyota huyo lilitokea baada ya Duke Abuya kuifungia Yanga bao la sita dakika ya 84 na wakati mpira huo unaanza katikati, alipiga shuti la moja kwa moja na kumshinda Diarra ambaye alionekana wazi amezidi mbele kidogo ya lango lake.

BWE 04

SOKA ALIANZIA TANDALE

Anasema safari yake ya soka ilianzia mtaani maeneo ya Tandale Shule jijini Dar es Salaam na mtu aliyemfanya kufika hapa alipo leo ni makocha waliojulikana kwa jina la Kisaga, akishirikiana na Mzee mwenzake, Simeni waliokuwa wanaishi wote.

“Ni miongoni mwa makocha ambao sitokaa niwasahau katika maisha yangu, walikuwa nguzo imara ya kunifikisha hapa nilipo leo, kwa sababu misingi yote ya soka walianza kunipa wao, kuanzia nidhamu ambayo ndio msingi wa jambo lolote,” anasema.


RAFIKI WA WATOTO

Bwenzi anasema moja ya marafiki zake wakubwa ni watoto kwa sababu muda mwingi anaishi nao na wamekuwa wakimpenda pia, jambo linalomfanya kupata baraka zaidi maishani mwake, hata kama akipitia changamoto zozote zinazoweza kumrudisha nyuma.

“Napenda sana watato wadogo na siku zote wamekuwa ni marafiki zangu wakubwa, huwa wana mchango mkubwa na ninaona heshima nikiwa nao, haina maana wengine sina urafiki nao isipokuwa nimekuwa nao bega kwa bega kwa kila ninachokifanya maishani.”

BWE 01

KIASI KIDOGO CHA FEDHA ALICHOLIPWA

Nyota huyo anasema katika safari yake ya soka la kulipwa, aliwahi kupewa kiasi kidogo cha fedha ambacho hatokaa akasahau katika maisha yake, ingawa anashukuru kwa sababu kuanzia hapo ilimpa hasira ya kufanya vizuri ili tu afike mbali kisoka.

“Naomba nifiche kiasi cha fedha nilichowahi kulipwa ila tukio hilo lilinitokea wakati nipo Namungo FC, niliamini huenda muda wangu haukufika na nilivumilia nikiamini ipo siku, kiukweli sijafika mbali ila hapa nilipo sasa nafurahia maisha.”


CHAMPIONSHIP PAGUMU

Kabla ya kujiunga na KenGold, nyota huyu alikuwa Mbeya Kwanza inayoshiriki Championship na hadi anaondoka aliifungia bao moja na kuchangia mengine mawili ‘Asisti’, huku akieleza alipotoka ni pagumu zaidi kuliko kucheza Ligi Kuu Bara.

“Asikwambie mtu rafiki yangu, Championship ni ngumu kuliko Ligi Kuu Bara, mchezaji yoyote aliyecheza huko muulize, watu kule wanacheza bila fomula na wanacheza kwa lengo la timu ipande tu, sasa watahakikisha wanafanya lolote liwezekanalo.”

BWE 02
BWE 02

MZEE WA NDONDO CUP

Nyota huyo alianza kufahamika zaidi katika michuano ya mtaani ya Ndondo Cup, aliyojizoelea umaarufu mkubwa na kuwafanya mashabiki kuliimba jina lake, huku akiweka wazi ataendelea kuithamini na kuipa heshima kutokana na kumfikisha alipo leo.

“Ndondo Cup imetoa wachezaji wengi na miongoni mwao ni mimi hapa, ni mashindano ambayo mtu wa kawaida anaweza kuyaona tu ya ujanja ujanga, ila ukitaka kuona vipaji vikubwa ambavyo huenda hujaviona jaribu siku moja tu kuhudhuria utaniambia.”


HAPENDI MAJIVUNO

Anasema sio mtu wa kujivuna au kujiona machoni mwa watu kama ambavyo baadhi yao wanafanya, huku akiwataka mashabiki au wadau wa soka popote wanapomuona wasisite kumuita na kuongea naye, ikiwemo kumrekebisha wakiona kuna sehemu anakosea.

“Siku zote katika maisha yangu huwa napenda kujifunza, shabiki au mdau yoyote akiniona na kama kuna kitu labda huenda nakifanya alafu hakimpendezi na anaona huenda kikaharibu karia yangu ya soka, ruksa kuniambia ukweli na wala asiogope.”

BWE 03

APOTEZEA NYOTA WAKIGENI

Nyota huyo anasema ni ngumu kushindania nafasi na wachezaji wakigeni kwa sababu wanapewa kipaumbele zaidi kuliko wazawa, ingawa anachoamini mpira ni mchezo wa wazi na ukionyesha kiwango kizuri utacheza tu bila ya kujali jina la mtu yeyote.

“Kiukweli ni mtihani mkubwa kushindana na wachezaji wakigeni kwa sababu wenzetu wanapewa nafasi zaidi kuliko sisi wazawa ila hilo kwangu ni tofauti kabisa, kwa sababu huwa sijali nikipata namba tu huwa napambana hadi wenyewe wananikubali.”


CHANGAMOTO ASIYOISAHAU

Bwenzi anasema licha ya changamoto mbalimbali alizopitia katika maisha yake, ila mojawapo ni ya kukaa nje ya uwanja kwa takribani msimu mzima kutokana na kutopata timu, ingawa haikumrudisha nyuma zaidi ya kuendelea kuamini wakati utafika.

“Kabla ya kwenda Mbeya Kwanza nilikaa takribani msimu mzima nikiwa sina timu na pia niliandamwa na majeraha ya hapa na pale, kiukweli ilikuwa kipindi kigumu sana ila niliamini wakati sahihi ni wa Mwenyezi Mungu pekee na sio mtu yeyote.”


NYOTA ANAYEMKUBALI

Bwenzi anasema miongoni mwa wachezaji anaowakubali na anafuata nyayo zao ni winga nyota wa Manchester City ya England na timu ya taifa ya Ubelgiji, Jeremy Baffour Doku kutokana na aina ya uchezaji wake, ambao umekuwa ukimvutia kila uchwao.

“Jamaa namkubali sana na hata ukiangalia ninavyocheza ni kama ninaiga baadhi ya vitu kutoka kwake, ni mzuri sana akiwa na mpira na ni ngumu kumpokonya, kwa hapa Tanzania wapo wengi ninaowakubali ingawa nisingependa kuweka wazi majina yao.”


AOTA UFUNGAJI BORA

Anasema licha ya kuichezea KenGold katika kipindi kifupi ila moja ya malengo yake makubwa ni kuibuka mfungaji bora siku moja.

“Hata kama haitokuwa hapa KenGold nilipo sasa ila natamani kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara, ni malengo yangu siku moja kuona nayatimiza, naamini sio rahisi kutokana na washambuliaji wazuri waliopo, ila nitaendelea kuyaishi maishani.”


MALENGO YAKE

Bwenzi anasema licha ya kutaka kuibuka mfungaji bora siku moja wa Ligi Kuu Bara ila anahitaji kuipambania KenGold ili isishuke daraja, huku akiwasihi zaidi mashabiki, wadau na viongozi mbalimbali wa jijini Mbeya kuendelea kuwapa sapoti.

“Mwenendo wetu kwa sasa ni mzuri ila bado tuna kazi kubwa ya kufanya ili tutoke chini, tukiendelea na ushirikiano wetu uliopo naamini kabisa tutafikia malengo hayo, mbali na hilo, pia ninapenda kuona siku moja nikicheza soka nje ya nchi.”