Fainali CAFCL: Rekodi ya mechi 26 ya Sundowns na maajabu ya AS FAR Rabat
Muktasari:
- Fainali hiyo iliyopangwa kuchezwa Mei 15, mwaka huu itakuwa vita ya Waarabu na Wasauzi na Sundowns itakuwa nyumbani, kisha marudiano ni Mei 24 mwaka huu, AS FAR Rabat ndio mwenyeji ambapo mshindi wa jumla katika mechi hizo mbili, ndiye atavalishwa taji la ubingwa baada ya Pyramids kuvuliwa hatua ya robo fainali.
BAADA ya safari ndefu ya msimu wa 2025-2026 katika Ligi ya Mabingwa Afrika iliyoanza Septemba 19, 2025, hatimaye inakwenda kuhitimishwa pale miamba miwili ya soka, Mamelodi Sundowns kutoka Afrika Kusini na AS FAR Rabat ya Morocco itakapokutana katika mechi ya fainali.
Fainali hiyo iliyopangwa kuchezwa Mei 15, mwaka huu itakuwa vita ya Waarabu na Wasauzi na Sundowns itakuwa nyumbani, kisha marudiano ni Mei 24 mwaka huu, AS FAR Rabat ndio mwenyeji ambapo mshindi wa jumla katika mechi hizo mbili, ndiye atavalishwa taji la ubingwa baada ya Pyramids kuvuliwa hatua ya robo fainali.
Kuna maajabu tunakwenda kuyashuhudia katika fainali hiyo ambayo inazikutanisha timu mbili zenye rekodi tofauti.
Sundowns waliofika fainali msimu uliopita na kupoteza mbele ya Pyramids, inasaka taji lao la pili katika michuano hii baada ya kubeba mwaka 2016 huku ikiwa haijapoteza katika mechi 26 za karibuni katika CAF.
FAR Rabat iliyowaondosha mabingwa watetezi wawili msimu huu, Pyramids (bingwa mtetezi Ligi ya Mabingwa) na RS Berkane (bingwa mtetezi Kombe la Shirikisho), inakwenda kupambana pia kuichapa timu ya tatu iliyocheza fainali msimu uliopita. Haijawahi kutokea katika michuano ya CAF timu moja kupambana na wapinzani watatu tofauti waliocheza fainali msimu wa nyuma yake.
ILIVYOKUWA NUSU FAINALI
Mamelodi Sundowns, maarufu kama ‘The Brazilians’, walikuwa wa kwanza kufuzu fainali kwa mara ya pili mfululizo baada ya kuibuka na ushindi wa jumla ya mabao 2-0 dhidi ya miamba ya Tunisia, Espérance Sportive de Tunis
Katika mchezo wa marudiano uliopigwa kwenye uwanja wa Loftus Versfeld huko Pretoria, Sundowns walionyesha ukomavu mkubwa kwa kupata ushindi wa 1-0
Shujaa wa mchezo huo alikuwa mshambuliaji raia wa Colombia, Brayan León, aliyefunga bao pekee katika dakika ya 35, ambapo pia ndiye aliyefunga mechi ya kwanza ugenini dakika ya 51.
Bao hilo lilitokana na penalti ambayo mlinda mlango wa Espérance, Béchir Ben Saïd, alimfanyia madhambi León, ingawa shuti la kwanza la León liliokolewa, lakini aliwahi mpira uliorejea na kuuzamisha nyavuni.
Hii ilikuwa penalti ya kwanza kwa Sundowns katika michuano hii ndani ya kipindi cha miaka miwili, na León ameweka rekodi ya kufunga katika michezo minne mfululizo aliyoanza.
Hii ni mara ya kwanza kwa Esperance kupoteza mechi zote mbili za hatua ya mtoano katika zaidi ya miaka mitatu, ikionesha ukubwa wa mafanikio ya Sundowns.
Kwa klabu hiyo ya Pretoria, ni hatua nyingine muhimu katika harakati za kutwaa ubingwa wao wa pili wa Afrika, baada ya mara ya mwisho kunyanyua kombe hilo mwaka 2016.
Kwa upande mwingine, FAR Rabat imeweka historia mpya kwa kutinga fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa tangu mashindano hayo yalipobadilishwa jina na muundo.
Licha ya kupoteza 1-0 katika mchezo wa marudiano ugenini dhidi ya RS Berkane, ushindi wao wa 2-0 katika mchezo wa kwanza nyumbani uliwabeba kwa jumla ya mabao 2-1, na kufuzu fainali.
Berkane walijitahidi kurudisha matokeo kwa bao la penalti la Yassine Lebhiri katika dakika ya 57 baada ya Paul Valère Bassène kuchezewa rafu, hata hivyo, nidhamu ya ulinzi ya FAR Rabat na kiwango bora cha mlinda mlango Ahmed Tagnaouti vilikuwa kikwazo kikubwa kwa Berkane ambao walitawala umiliki wa mpira.
FAR Rabat sasa inakuwa klabu ya tatu kutoka Morocco kufika hatua hii, ikifuata nyayo za Raja na Wydad Casablanca.
Mafanikio haya ni makubwa kwa klabu hiyo ambayo ilitwaa ubingwa wa mwisho mwaka 1985 wakati michuano hiyo ikiitwa African Cup of Champions Clubs, kabla ya mwaka 1997 kubadilishwa jina na kuitwa Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo timu hiyo kwa sasa inatafuta kurudisha heshima yake baada ya miongo kadhaa ya kusubiri.
FAINALI ITAKUWAJE
Fainali inayokuja inatarajiwa kuwa ya kukata na shoka. Sundowns wanaingia wakiwa na rekodi ya kutisha nyumbani, wakiwa wamepoteza mchezo mmoja tu kati ya 26 ya hivi karibuni katika michuano hii.
Wakiwa na kasi nzuri, uzoefu na uimara wa ulinzi, Sundowns wanaingia fainali kama moja ya timu zinazopewa nafasi kubwa na kwa mara nyingine.
Kuanzia mwanzo hadi wanatinga fainali, Sundowns wamefunga mabao 23, wakiruhusu tisa. Walianzia hatua ya pili ambapo walifunga mabao saba na kuruhusu moja, makundi wakafunga mabao tisa na kuruhusu sita, kisha robo fainali walifunga matatu na kurusu mawili, huku nusu fainali wakifunga mawili, hawakuruhusu.
Kwa upande wao, FAR Rabat watalazimika kuboresha rekodi yao ya ugenini ambapo wamekuwa wakipata tabu kufunga mabao.
Rekodi zinaonyesha FAR Rabat msimu huu tangu hatua ya awali hadi nusu fainali, ugenini wamefunga mabao matano pekee katika mechi saba, ambapo matatu ni hatua za awali, kisha mawili robo fainali, huku makundi na nusu fainali haikufunga ugenini.
Sundowns wanasaka taji lao la pili tangu mwaka 2016 na Rabat wakitafuta kuandika historia mpya wa kushinda taji hilo kwani haijwahi kufanya hivyo tangu libadilishwe jina.
Hata hivyo, FAR Rabt sio wanyonyenge kwani tangu Novemba 22, 2025, walipochapwa na Yanga bao 1-0 kwenye hatua ya makundi, mechi ikichezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, mfungaji akiwa Prince Dube dakika ya 58, timu hiyo haijapoteza tena kwenye michuano hiyo.
Baada ya hapo, ilikwenda kutoka 0-0 dhidi ya Al Ahly mechi ya kumaliza makundi na kufuzu robo fainali ikishika nafasi ya pili Kundi B.
Kisha robo fainali ikaiondosha bingwa mtetezi, Pyramids kwa jumla ya mabao 3-2, ndipo nusu fainali pia ikaichapa RS Berkane jumla ya mabao 2-1.
Kumbuka Berkane nayo ilikuwa bingwa mtetezi wa Kombe la Shirikisho Afrika, hivyo AS FAR Rabat msimu huu imewaondosha mabingwa watetezi wote wa CAF.