Ibenge ametufundisha kitu kwa Issa Fofana
Muktasari:
- Kumbuka Fofana baada ya kuingia Azam FC akawa ndio mchezaji aliyefanya kazi kwa ukaribu zaidi na Ibenge kikosini kuliko mwingine yeyote ndani ya timu hiyo.
FLORENT Ibenge wakati anasaini mkataba wa kuifundisha Azam FC, za ndani zinadai kwamba uongozi wa timu hiyi ulimhakikishia utasajili mchezaji yeyote atakayemhitaji.
Chapchap jina aliloanza nalo lilikuwa ni la kipa Issa Fofana ambaye Azam ilimsajili muda mfupi baada ya kupendekezwa akitokea Al Hilal ya Sudan.
Kumbuka Fofana baada ya kuingia Azam FC akawa ndio mchezaji aliyefanya kazi kwa ukaribu zaidi na Ibenge kikosini kuliko mwingine yeyote ndani ya timu hiyo.
Wengi tuliamini Fofana ndiye atakuwa kipa chaguo la kwanza la Ibenge kwa vile ni mtu wanayefahamiana vizuri kuliko makipa wengine kama Aishi Manula, Zuberi Foba na Anthony Mpemba.
Lakini baada ya siku chache, mambo yakaanza kuwa tofauti kwani alianza kugawana mechi za kucheza na Foba na sasa amejikuta akiwa kipa chaguo la tatu ndani ya Azam FC.
Chaguo la kwanza ni Manula, la pili ni Foba na yeye Fofana yuko nyuma yao na kuna uwezekano mdogo kwake kubakia ndani ya klabu hiyo msimu ujao.
Kuna somo hapa ambalo Ibenge analitoa nalo ni kuzingatia weledi katika utekelezaji wa majukumu ya ukocha badala ya kuleta ushkaji au urafiki na kujuana ambako mara nyingi huwa chanzo cha timu kufanya vibaya.
Ibenge kajaribu kuonyesha kwamba kocha anatakiwa atoe nafasi ya kucheza kwa mchezaji kwa kuangalia kile anachokifanya uwanjani katika mechi na mazoezini na sio kwa sababu ya kufahamiana.
Lakini pia anawakumbusha wachezaji kuwa hawapaswi kuhofia pale Kocha anapoingia katika timu na wachezaji wake bali iwe chachu kwao kuimarisha viwango vyao.