Prime
Jicho la mwewe katika dabi ya mzizima, Arajiga mmh!
MBAGALA kwa mbele, kule Chamazi juzi kulikuwa na mechi nzuri ya soka. Azam dhidi ya Simba. Moja kati ya mechi chache kubwa nchini katika ligi yetu. Walau Azam ni timu ambayo inaweza kukupeleka uwanjani ukiamini itapata kitu katika mechi dhidi ya Simba au Yanga.
Na ndicho kilichotokea. Msimu huu wamepata pointi nne mbele ya Simba. Walishinda mechi ya kwanza pale Temeke katika Uwanja wa Mkapa na juzi walipata pointi moja baada ya Suluhu. Niligundua machache baada ya kutazama mechi kwa makini.
Jambo la kwanza kabisa nadhani tunashuhudia siku za mwisho za Clatous Chota Chama. Hatimaye miguu imemsaliti. Mwili hautaki tena. Kuna mechi ambazo atatuonyesha ubora wake lakini kama Simba itakuwa inacheza na wapinzani wasio na afya.
Katika mechi hii James Akaminko na Fei Toto walichukua dimba lao na wakawa mabosi. Akaminko ndiye ambaye alitawala dimba kwa muda wote huku akipokea mipira kwa mbwembwe na kugeuka kwa mbwembwe.
Fei alichoka katika kipindi cha pili kiasi cha kutolewa lakini Akaminko alikuwa bosi kwa muda wote. Kwa kiwango alichoonyesha juzi kama angekuwa ni mchezaji wa Simba au Yanga basi mitandaoni kote jina lake lingeimbwa. Hata hivyo, hakuna kelele sana kwa sababu yupo Azam.
Kingine? Ni kuhusu mwamuzi msaidizi wa pili. Kipindi cha kwanza alikuwa ananyoosha kibendera muda wote kuashiria wachezaji wa Azam walikuwa wameotea hata kama walikuwa hawajaotea. Kipindi cha pili akafanya hivyo hivyo kwa wachezaji wa Simba.
Sio kwamba alikuwa anafanya makusudi, Hapana, alikuwa anajihami tu. Kila mchezaji alipoonekana akiwa peke yake alinyoosha kibendera chake hata kama mchezaji alikuwa amevunja mtego wa kuotea.
Kuhusu mwamuzi, Ahmed Arajiga kutoka Manyara? Ukweli ni kwamba alikuwa na mechi bora kwa jumla wake. Alichezesha vizuri na baadaye akaonekana amewanyima Simba penalti halali wakati Libasse Gueye alipoonekana kugongwa kwa nyuma na mlinzi Fuentes Mendoza wa Azam.
Niliwahi kuandika mahala. Tunaweza kumaliza waamuzi wote na waamuzi wasaidizi na tukalazimika kwenda kuwatafuta wa nchi jirani kama makosa kama haya yatakuwa yanasababisha waamuzi kufungiwa kila mkeka wa bodi ya ligi unapotoka.
Sisi tunaotazama mpira katika televisheni tunapata faida ya kuangalia marudio ya picha jongefu. Arajiga na wenzake huwa hawapati faida hiyo. Wazungu walipoona hali inazidi kuwa mbaya ndipo wakampa faida mwamuzi naye awe anaangalia marudio ya video. Ndio hiki kitu kinaitwa VAR.
Arajiga huyu huyu ndiye ambaye msimu huu aliwahi kuwapa Simba penalti yenye utata wiki chache zilizopita lakini ndiye huyu huyu ambaye juzi aliwanyima Simba penalti. Ni mwanadamu. Hana msaada wa VAR. Dhamira yake inamtuma kufanya jambo jema lakini hana msaada wa video za marudio.
Tuhamie kwa mchezaji anayeitwa Libasse Gueye. Alipoingia katika timu niliona ataleta jambo jipya. Ana kipaji maridhawa lakini nimeanza kuwa na mashaka na msaada wake katika timu. Kipaji siyo kila kitu. Kipaji inabidi kilete bidhaa ya mwisho uwanjani. Bao au pasi ya bao.
Libasse anahitaji kubadilika. Awaangalie wenzake kwa haraka pindi anapomalizana na chenga zake au mbio zake. Pia awe makini katika umaliziaji wake. Vinginevyo ataingia katika kundi la wachezaji wanaoitwa kazibure. Kila siku anaanza kuninyong’onyesha baada ya kumsifia sana alipoanza vema.
Libasse pia anapaswa kuufahamu mpira wa kisasa ulivyo. Anampa wakati mgumu, Shomari kapombe kwa sababu hamsadii katika majukumu mengine ya ukabaji uwanjani. Kwa staili hii ni rahisi kudhani kapombe hafai kumbe hana msaada wa haraka.
Suleiman Mwalimu naye anahitajika kuwa makini na umaliziaji wake. Baada ya pambano hili huenda mabosi wa Simba wakabadilisha mawazo yao juu ya mshambuliaji wao, Jonathan Sowah ambaye ana matatizo ya nidhamu. Suleiman anashindwa kutumia nafasi zake vema.
Simba kwa jumla? Mechi hii kipindi cha kwanza walikuwa wanafukuza vivuli vya wachezaji wa Azam ambao walikuwa bora zaidi uwanjani. Kipindi cha pili ndipo maisha yalipobadilika baada ya kuingia kwa Neo Maema huku Azam wakionekana kuchoka zaidi.
Katika siku za karibuni kumekuwa na kauli Simba imejipata. Hapana, bado haijajipata lakini ina mwelekeo wa kujipata. Pambano hili lilikuwa kipimo tosha cha kujua wamejipata kwa kiasi gani lakini ni wazi kocha wao, Steven Barker ana kazi ngumu ya kufanya kuibadili timu.
Wale Azam ndio ambao wanaonekana wamebadilika chini ya Florent Ibenge ingawa na wao pia wafanyie kazi pumzi zao pamoja na umaliziaji wa muvu zao. Mechi ya juzi katika kipindi cha kwanza huenda wangeondoka uwanjani na uongozi wa mabao 2-0.
Kiingilio cha pambano nacho kilikuwa mjadala kabla ya pambano kuanza. Watanzania tubadilike kidogo ingawa mpira ni mchezo ghali kuutazama. Kiingilio cha Sh15,000 ni sawa na Dola 6 tu. Mechi za wakubwa kule nje kiingilio hufika Sh400,000. Ndio, kwa dakika tisini tu.
Uwanja mdogo kama Chama kutazama pambano kubwa la Simba na Azam kwa Sh3,000 ni sawa na kutazama dabi hii kubwa kwa Dola 1 tu. Kama kiingilio kinakuwa Sh5,000 basi ni sawa na kutazama mechi kwa Dola 2 tu.
Tukumbushane tu kutazama mpira ni kitu cha gharama. Ni starehe kama starehe nyingine. Pambano la ligi ya mabingwa wa Ulaya kati ya PSG na Arsenal pale Paris Aprili mwaka jana nilitazama kwa kiasi cha Euro 500. Karibu Sh2 milioni.