Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kalambo anavyoishi kwa hesabu nzito Championship

Muktasari:

  • Kalambo aliyewahi kucheza pia Geita Gold msimu huu anacheza kikosi cha maafande wa Transit Camp kinachoshiriki Ligi ya Championship, ambapo nyota huyo amefunguka mambo mengi ikiwemo malengo yake kwa ujumla kama ambavyo anaelezea kwa kina.

AARON Kalambo sio jina geni kwa mashabiki wengi wa soka nchini kutokana na kipa huyo kujizoelea pia umaarufu mkubwa hasa baada ya kucheza timu mbalimbali za Ligi Kuu, zikiwemo za ‘Wagosi wa Kaya’ Coastal Union na Dodoma Jiji ‘Walima Zabibu’.

Kalambo aliyewahi kucheza pia Geita Gold msimu huu anacheza kikosi cha maafande wa Transit Camp kinachoshiriki Ligi ya Championship, ambapo nyota huyo amefunguka mambo mengi ikiwemo malengo yake kwa ujumla kama ambavyo anaelezea kwa kina.


UHUSIANO NA MASHABIKI

Nyota huyo anasema licha ya kucheza Championship isiyoonyeshwa, ila bado uhusiano na mashabiki zake uko karibu, kutokana na jinsi anavyoishi nao tangu akiwa Ligi Kuu, jambo ambalo limeendelea kumpa sapoti ya kupambana katika kazi.

“Changamoto iliyopo ni kwa mashabiki zangu ambao wasipokuja uwanjani basi hawataniona katika televisheni, ila uhusiano wetu bado ni imara na wamekuwa ni sehemu muhimu sana ya kunipa pia motisha katika majukumu yangu ya kila siku uwanjani.”

Kalambo anasema mashabiki wamekuwa na mchango mkubwa katika kukuza karia yake ya soka, jambo ambalo limeendelea kumkuza kiakili na kimwili, hata anapopita changamoto mbalimbali hasa za kukaa nje kwa muda mrefu kutokana na majeraha tofauti.


WAKALA AMKWAMISHA

Kipa huyo anasema sababu kubwa ya kucheza Ligi ya Championship msimu huu ni kutokana na wakala anayemsimamia kuchelewa kufanya makubaliano na baadhi ya timu za Ligi Kuu Bara zilizomuhitaji, hali iliyosababisha kushindwa kuendana na muda. “Nilitamani kuendelea kucheza Ligi Kuu Bara ila baada ya kukosa timu nikaona ni vyema kujiunga na Transit Camp, ambayo ilionyesha nia ya kunihitaji, haikuwa rahisi kwangu ila niliona ni vizuri kuliko kukaa bila kucheza,” anasema.


UTOFAUTI WA LIGI

Kipa huyo anasema kucheza Ligi Kuu inahitaji utimamu wa mwili na kiakili zaidi tofauti na Championship, ambayo muda mwingi inatumia nguvu kutokana na mahitaji makubwa hasa kwa timu zinazopigania nafasi za kupanda Ligi Kuu Bara.

“Ligi Kuu unacheza kwa nafasi kwa maana wachezaji wako huru kufanya jambo lolote katika uchezaji wao, ila Championship ni tofauti kabisa kwa sababu hakuna huo muda na matumizi ya nguvu pia ni makubwa kuliko kutumia akili,” anasema Kalambo.

Kalambo anasema kila mchezaji anayecheza Championship malengo yake ni kucheza Ligi Kuu Bara, kwa sababu ndio fursa nzuri ya kutangaza jina lako kutokana na kuonekana sehemu nyingi, ingawa uwekezaji kwa sasa ni mkubwa kutokana na ushindani.


SAIKOLOJIA MUHIMU

Kalambo anasema wachezaji wengi wanashindwa kuendana na mazingira halisi kwa sababu ya matarajio makubwa waliyokuwa nayo tangu mwanzoni, ingawa kwake ilikuwa ni rahisi kukubaliana na hilo la kuamua kuanza moja sio kufeli bali ni uthubutu.

“Saikolojia ni muhimu sana kwa wachezaji kwa sababu kwa mfano mimi nilitaka kuendelea kucheza Ligi Kuu ila ikashindikana kutimiza hilo, sasa ikiwa hautakubaliana na kilichotokea mwisho wake unaweza kusababisha pia matatizo makubwa,” anasema.

Kipa huyo anasema matatizo mengi ya saikolojia yanawakuta wachezaji wengi kutokana na baadhi yao kushindwa kuendana na hali halisi iliyotokea, japo ikiwa utaamua kuanza moja na kutokata tamaa bado una nafasi ya kutimiza malengo uliyoweka.

“Baadhi ya timu za Championship malipo yao ni madogo sasa ikiwa umetoka Ligi Kuu na ukacheza daraja la chini ni lazima ukubaliane na hali halisi, hii itakusaidia kukujengea motisha ya kupambana ili kufikia unapopahitaji,” anasema Kalambo. 

MABADILIKO YA KIFEDHA

Kalambo anasema unapokuwa mchezaji uliyezoea kupata kiasi kikubwa cha fedha ni lazima ujue namna ya kuishi kutokana na mazingira kwa sababu huwezi kucheza katika madaraja ya juu kwa kiwango kikubwa kila siku bila kushuka.

“Kwa mfano kama mimi nilikuwa na matumizi makubwa ya fedha kwa sasa ni lazima nibadilishe muundo wangu wa maisha kwa sababu kipato nachopata ni kidogo tofauti na mwanzo. Ukiweza kuendana na hali halisi basi hutapata shida,” anasema.

Kipa huyo anasema wachezaji wengi wanapotea haraka kwa sababu ya mabadiliko ya kifedha akitoa mfano unapotoka kwenye timu uliyokuwa unalipwa Sh10 milioni na kwenda kulipwa Sh5 milioni ni lazima ujipange kiakili kuendana na hali halisi.


KIPAUMBELE CHA KWANZA

Kipa huyo anasema kipaumbele chake ni kukipigania kikosi hicho cha maafande wa Transit Camp kipande Ligi Kuu msimu ujao, licha ya ushindani mkubwa, hususani kutokana na timu mbili za juu zinazopanda daraja moja kwa moja kutoka Championship.

“Kumaliza nafasi ya kwanza au ya pili ni ngumu sana kwetu kutokana na kasi ya wapinzani wetu, ila moja ya malengo yetu kwa sasa ni kuhakikisha tunakuwa wa tatu au wanne, ili tucheze mechi za play-off (mchujo) ya kuwania kupanda daraja,” anasema.

Kalambo anasema wachezaji kiujumla wanapambana kwa ajili ya kutimiza malengo ya kuipandisha timu hiyo kwenda Ligi Kuu, ingawa hatima yake itajulikana mwisho wa msimu huu, kwa sababu mkataba wake na kikosi hicho cha maafande ndipo unaisha.


MAKUBALIANO YA MKATABA

Licha ya kucheza timu za madaraja yote, ila Kalambo anasema hakuna utofauti wa uongozi katika suala la nidhamu kwa Ligi Kuu Bara na Championship, isipokuwa kinachofuatwa kati ya pande zote mbili ni makubaliano mliyokubaliana ya kimkataba.

“Kabla ya kusaini mkataba kuna makubaliano ni lazima kila mmoja aridhike nayo kwa maana ya upande wa mchezaji na klabu husika, hii inasaidia sana pindi mmoja wapo anapoenda tofauti kutumia miongozo mliyokubaliana tangu mwanzoni,” anasema.

Kalambo anasema kinachochangia kwenda tofauti ni kushindwa kusoma vizuri mkataba mliokubaliana, hasa kwa wachezaji wengi wanapowekewa kiasi kikubwa cha fedha ambacho hawajawahi kukishika wanashindwa kuangalia mambo muhimu ya msingi yaliyopo.


SUALA LA MOTISHA

Kalambo anasema katika Ligi ya Championship motisha ya wachezaji ni kubwa kutokana na matamanio ya kufika mbali zaidi, ila ni kwa baadhi ya timu kubwa na zenye uwezo wa kifedha, ambazo ndizo zinazopigania nafasi ya kupanda Ligi Kuu Bara.

“Licha ya uwezo wa timu kutofautiana kifedha ila mchezaji mwenyewe ni lazima akubaliane na hali halisi, unapopambana ni kwa ajili ya kulitangaza pia mwenyewe jina lako, hiyo ndio motisha pekee inayoweza kukutoa sehemu moja kwenda nyingine.”

Kipa huyo anasema hata ikiwa mchezaji anacheza katika timu za kawaida ambazo uwezo wa kifedha ni mdogo, anapaswa kuamini motisha ya kwanza ni ya yeye mwenyewe kupambana, kwa sababu huenda ikawa ni njia ya kuonekana na kutimiza malengo yako.


KINACHOWAANGUSHA

Kipa huyo anasema wachezaji sio kweli wanafeli Ligi Kuu Bara na kukimbilia Championship kama watu wengi wanavyoamini kwa sasa, isipokuwa kuna changamoto nyingi nyuma ya pazia zinazochangia pia kuamua kutafuta changamoto sehemu nyingine mpya.

“Mpira wa miaka mitano nyuma ni tofauti na huu wa sasa, makocha wengi hawaamini mchezaji anajua mpira kwa kiwango gani, ila wanachotaka wao ni kufuata kitu wanachokiamini, hii mara kadhaa imekuwa ni changamoto kwa wachezaji wengi,” anasema.

Kalambo anasema mchezaji mzuri ni lazima akubaliane na mabadiliko ya mfumo ili aendelee kuonyesha kiwango chake bora kwa muda mrefu, japo baadhi yao hawana nidhamu jambo linaalochangia kuona wengi wao wanazidi kupotea katika ramani ya soka.


USHAURI

Kipa huyo anasema kipaji hakitoshi kwa mchezaji kufikia malengo yake pekee isipokuwa nidhamu ina nafasi kubwa, japo kwa baadhi yao wamekuwa wakilewa sifa na kujisahau, jambo linalochangia kwa kiasi kikubwa kupotea haraka ingawa ni vijana.

“Vijana wengi wana vipaji ila wanashindwa kudumu kwa muda mrefu katika mpira wa miguu kwa sababu ya kitu kidogo ambacho ni nidhamu, mimi nawashauri vijana wenzangu watu wote tunaowaona wamefanikiwa heshima kwao ni kipaumbele cha kwanza,” anasema.

Kalambo anasema misimu mitano nyuma wapo wachezaji wadogo wenye vipaji waliotabiriwa kufika mbali lakini jambo kubwa la kushangaza wamepotea katika ramani ya soka, kutokana na kukosa nidhamu ya kuendeleza vipaji vyao walivyobarikiwa mguuni.