Prime
Kalamu ya Samatta imeandika kurasa tano za Ulaya
MIAKA kumi iliyopita, jina la Mbwana Ally Samatta halikuwa kubwa kama lilivyo leo katika ramani ya soka la dunia.
Alikuwa mshambuliaji kijana kutoka Dar es Salaam, mwenye ndoto kubwa lakini akitoka katika mazingira ambayo hayakuwa na historia kubwa ya kutoa wachezaji kwenda Ulaya.
Leo, baada ya muongo mmoja, Samatta ameandika historia ambayo haitasahaulika sio kwa Tanzania pekee, bali kwa ukanda wa Afrika Mashariki, anaweza kukaa meza moja na McDonald Mariga na Victor Wanyama ambao kwa nyakati tofauti wameuwasha moto Ulaya.
Katika ulimwengu wa soka unaotawaliwa na vipaji kutoka mabara yenye mifumo imara ya maendeleo ya vijana, kupenya kwa mchezaji kutoka Tanzania hadi kucheza katika ligi kubwa za Ulaya sio jambo la kawaida. Lakini Samatta alivunja dhana hiyo, akionyesha kuwa kipaji, nidhamu na uthubutu vinaweza kukufanya utimizi ndoto zako.
Safari yake ilijengwa hatua kwa hatua. Kuanzia mitaa ya Dar es Salaam, kupitia changamoto za soka la ndani ambapo aliichezea Mbagala Market, Simba, hadi kung’ara TP Mazembe, kila hatua ilimjenga na kumuweka tayari kwa mapambano ya kiwango cha juu zaidi.
Mwaka 2015 ulikuwa mwanzo wa mabadiliko makubwa. Alipoibuka mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na mabao saba na kusaidia Mazembe kutwaa ubingwa, dunia ilianza kumtazama kwa jicho tofauti.
Tuzo ya mchezaji bora wa Afrika anayecheza ndani ilithibitisha kuwa alikuwa tayari kucheza soka la kulipwa Ulaya. Ndipo mwaka 2016 alipofungua ukurasa mpya kwa kujiunga na KRC Genk hatua iliyokuwa mwanzo wa safari ya miaka 10 Ulaya.
Huo haukuwa uhamisho wa kawaida, bali ilikuwa ni mwanzo wa historia mpya kwa nahodha huyo wa Tanzania.
Katika kipindi hicho, Samatta amecheza katika ligi tano tofauti za Ulaya, akipambana na mazingira mapya, mifumo tofauti ya uchezaji na ushindani mkali. Kutoka Ubelgiji hadi England, Uturuki, Ugiriki na sasa Ufaransa.
UBELGIJI ALIVYOITEKA
Alipotua Ubelgiji 2016 kwa kujiunga na KRC Genk, wengi waliona kama ni hatua ya kawaida ya mchezaji wa Afrika kutafuta maisha Ulaya.
Lakini kwa Samatta, huu ulikuwa mwanzo wa zama mpya sio kwake tu, bali kwa soka la Tanzania kwa ujumla.
Katika misimu yake ya mwanzo, Samatta alihitaji muda mfupi tu kuzoea kasi ya soka la Ulaya. Tofauti na ligi za Afrika, hapa kulikuwa na mbinu tofauti, kasi ya mchezo na ushindani kila dakika.
Hata hivyo, kwa nidhamu yake na uwezo wake wa kusoma mchezo, alianza kupenya taratibu katika kikosi cha kwanza cha Genk.
Ndani ya miaka minne alicheza mechi 144 na kufunga mabao 56 takwimu zinazothibitisha kuwa hakuwa mchezaji wa kupita, bali alikuwa muhimili wa timu. Msimu wa 2018/19 ulikuwa wa dhahabu kwake alipofunga mabao 20 ya ligi na kuwa mmoja wa wafungaji mahiri wa Belgian Pro League huku akiisaidia Genk kutwaa ubingwa wa ligi hiyo.
Lakini, mafanikio hayo hayakuishia hapo. Katika michuano ya Ulaya alionyesha ubora wake kwa kufunga mabao muhimu ikiwemo hat-trick dhidi ya Brøndby IF katika Europa League.
Huo ulikuwa ushahidi kuwa Samatta alikuwa amepevuka na sasa alikuwa tayari kwa hatua kubwa zaidi.
Tuzo ya Ebony Shoe aliyoshinda 2019 ilikuwa muhuri wa ubora wake. Tuzo hiyo hutolewa kwa mchezaji bora mwenye asili ya Afrika nchini Ubelgiji na kushinda kwake kulimuweka rasmi katika ramani ya wachezaji bora wa Afrika barani Ulaya.
NDOTO YA LIGI KUU ENGLAND
Januari 2020, ndoto ya wachezaji wengi kucheza Ligi Kuu England ilitimia kwa Samatta aliposaini mkataba wa miaka minne na nusu na Aston Villa ambayo kwa sasa inanolewa na Unai Emery.
Uhamisho huo ulimfanya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza katika Ligi ya England, rekodi ambayo bado haijavunjwa hadi sasa ikiwa ni miaka sita imepita.
Samatta aliingia moja kwa moja katika presha kubwa ya ligi yenye ushindani mkali zaidi duniani. Lakini hakusubiri muda mrefu kuacha alama. Katika mechi yake ya kwanza ya ligi dhidi ya Bournemouth, alifunga bao na kuweka historia ambayo itaendelea kutajwa kwa miaka mingi.
Samatta pia alifunga bao katika fainali ya Kombe la EFL dhidi ya Manchester City, akionyesha uwezo wake dhidi ya vigogo hao. Hata hivyo, ushindani mkali ndani ya kikosi na kasi ya ligi hiyo ulimfanya ashindwe kupata nafasi ya kudumu.
Pamoja na changamoto hizo, mchango wake hauwezi kupuuzwa. Alifungua mlango ambao haujawahi kufunguliwa na Mtanzania mwingine kabla yake na hilo pekee linamfanya kuwa sehemu ya historia ya soka la Tanzania.
SAFARI YA KUJITAFUTA
Baada ya England, Samatta alijiunga na Fenerbahçe S.K., moja ya klabu kubwa nchini Uturuki. Hapa alitarajiwa kurejea katika kiwango chake cha juu, lakini mambo hayakuwa rahisi kama ilivyotarajiwa.
Alicheza mechi 30 na kufunga mabao matano huku akikumbana na changamoto za ushindani mkali na mabadiliko ya kimfumo ndani ya timu. Hali hii kutolewa kwa mkopo katika klabu ya Royal Antwerp 2021.
Akiwa Antwerp, alirejea katika mazingira aliyoyazoea ya Ubelgiji alifunga mabao matano katika mechi 32. Mwaka 2022 alirudi tena Genk kwa mkopo, akicheza mechi 33 na kufunga mabao sita.
Hii ilikuwa hatua muhimu ya kurejesha kujiamini kwake, ingawa haikufikia kiwango chake cha awali.
Hata hivyo, alionyesha kitu muhimu zaidi utulivu wa akili na uwezo wa kupambana hata pale mambo yanapokuwa magumu.
UBINGWA UGIRIKI
Mwaka 2023, Samatta alichukua hatua mpya kwa kujiunga na PAOK FC. Hii ilikuwa nafasi nyingine ya kujijenga katika ligi mpya yenye ushindani tofauti.
Ingawa hakufunga mabao mengi, mchango wake ndani ya timu ulikuwa mkubwa hasa katika suala la uzoefu na uongozi. Aliisaidia PAOK kutwaa ubingwa wa ligi ya Ugiriki msimu wa 2023/24 na lilikuwa taji lingine muhimu katika safari yake. Katika kipindi chake PAOK alionyesha kuwa thamani ya mchezaji haipimwi tu kwa mabao, bali pia kwa mchango wake katika mfumo wa timu na uwezo wa kuhamasisha wachezaji wengine.
UKURASA MPYA UFARANSA
Mwaka 2025, Samatta alijiunga na Le Havre AC na kuweka historia nyingine kwa kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza katika Ligue 1. Hatua hii inaonyesha wazi kuwa hata baada ya miaka 10 Ulaya, bado anaendelea kuwa na thamani katika soka la kiwango cha juu.
Ingawa ameanza kwa changamoto ya mabao, uzoefu wake unaendelea kuwa silaha muhimu kwa timu yake.
MSIKIE SAMATTA
“Kucheza Ulaya sio kitu rahisi kama watu wengi wanavyofikiria, kila siku ni vita mpya. Nilipofika KRC Genk niligundua haraka kuwa hapa si tu kipaji kinahitajika, bali nidhamu na akili ya mchezo,” anasema na kuongeza:
“Ilinibidi nijifunze haraka, kubadilika na kukubali changamoto.Ndiyo maana ile miaka yangu ya mwanzo ilikuwa muhimu sana kunijenga.”€
Nyota huyo, anaongeza kwa kusema: “Watu wengi wanaona tu mabao au timu unazochezea lakini hawajui presha iliyopo nyuma yake.
“Nilipofika Premier League, kila kitu kilikuwa kwenye kiwango cha juu zaidi kasi, nguvu na ushindani. Kufunga bao langu la kwanza ilikuwa momenti ya kipekee sana kwangu na kwa Tanzania lakini pia ilinipa motisha ya kuendelea kupambana hata pale mambo yanapokuwa magumu.”€
NANI ANAFUATA?
Safari ya Samatta imeacha swali moja kubwa katika soka la Tanzania, nani anafuata? Kwa miaka mingi, mafanikio yake yameonekana kama hadithi ya kipekee lakini wadau wanaamini kuwa inaweza kuwa mwanzo wa mwelekeo mpya kama mambo sahihi yatafanyika. Wadau wanaeleza kuwa Tanzania ina vipaji vingi lakini changamoto kubwa ipo katika kuvikuza kwa njia sahihi.
Tofauti na nchi nyingi za Afrika Magharibi, bado hakuna mfumo madhubuti wa akademi zinazofuata viwango vya kimataifa. Hili linafanya wachezaji wengi kushindwa kupata maandalizi ya mapema kabla ya kufika katika ushindani wa kimataifa.
Kocha wa zamani wa Yanga na Azam, Hans van der Pluijm anasema; “Vipaji vipo lakini havitoshi. Inatakiwa iwepo mifumo ya kuvinoa tangu umri mdogo ili kuwapa wachezaji nafasi ya kushindana zaidi.”
Kwa upande wa kocha wa zamani wa Taifa Stars, Marcio Maximo anasema: “Nimekaa kwa miaka mingi Tanzania na kuona ni kama nyumbani vile, natamani kuona siku moja ikiwa moja ya taifa tishio zaidi Afrika, najua haishindikani lakini lazima tukubali kushirikiana kusaidia vijana wadogo, kuweka misingi mzuri ambayo itafanya kuonekana mapema kama ilivyokuwa kwa Samatta.”
Wadau wa klabu za ndani kama Simba na Yanga wanaona kuna umuhimu wa kubadilisha mtazamo wa uwekezaji. Badala ya kuwekeza zaidi kwenye matokeo ya muda mfupi, wanasisitiza haja ya kuwekeza kwenye vijana ambao wanaweza kuuzwa nje na kuleta faida ya muda mrefu.
Katika ngazi ya uongozi wa soka, kuna wito wa kuimarisha ushirikiano na klabu za Ulaya. Ushirikiano huu unaweza kusaidia kubadilishana maarifa, kuwapeleka wachezaji kwenye majaribio (trials) na kuongeza uwezekano wa vipaji vya Tanzania kuonekana. “Tunahitaji kufungua milango. Soka la sasa ni mtandao ukikosa koneksheni, hata uwe na kipaji gani ni vigumu kufika mbali,”€ anasema Mohammed Badru ambaye anasimamia mradi wa Yanga Soccer School.