Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kina Job wasukiwa mkakati Mtibwa

Muktasari:

  • Mabingwa wa Ligi Kuu Bara wa mwaka 1999 na 2000, Mtibwa Sugar wamekuwa wakibeba sifa ya kuwa pia ni kituo cha kukuza na kuendeleza vipaji na walikuwa moja ya timu chache ambazo hazikuwa na nyota wa kigeni kabla ya jambo hilo kubadilika hivi karibuni.

MAMBO yanabadilika. Hivyo ndivyo unavyoweza kusema unapoizungumzia Mtibwa Sugar ya sasa kutokana na kuingia kwenye mfumo wa kusajili nyota wa kigeni, tofauti na ilivyokuwa miaka iliyopita, huku kocha mpya Mkenya Yusuf Chippo, akiwa na mlima wa kupanda katika kutimiza majukumu yake.

Mabingwa wa Ligi Kuu Bara wa mwaka 1999 na 2000, Mtibwa Sugar wamekuwa wakibeba sifa ya kuwa pia ni kituo cha kukuza na kuendeleza vipaji na walikuwa moja ya timu chache ambazo hazikuwa na nyota wa kigeni kabla ya jambo hilo kubadilika hivi karibuni.

Mwanaspoti limefanya mahojiano maalumu na Mtendaji Mkuu wa Mtibwa Sugar, Swabri Aboubakar ambaye amefunguka mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na sababu ya kuingia kwenye sajili za nyota wa kigeni huku akibainisha kuwa dirisha dogo wana mpango wa kuongeza idadi zaidi.


KINA JOB WAPYA

Kwa miaka mingi, Mtibwa Sugar imekuwa ni chimbuko la vipaji na mastaa wengi wa soka ambao wametamba katika klabu nyingi akiwamo nahodha wa zamani wa timu ya taifa, Taifa Stars -- Mecky Maxime, kiungo fundi wa boli Abdulhalim Humoud ‘Gaucho’ na wengine wengi.

Hata katika kizazi cha sasa, wapo wakali kibao waliopikwa katika akademi ya Mtibwa Sugar. Nahodha msaidizi wa Yanga na Taifa Stars -- Dickson Job, beki wa timu hiyo ya Jangwani, Kibwana Shomary, kipa wao Aboutwalib Mshery, beki wa Singida United, Nickson Kibabage na Ladack Chasambi wa Simba ni kati ya matunda ya Mtibwa Sugar.

Licha ya timu hiyo kuamua kuingia kwenye ‘siasa’ za kusajili nyota wa kigeni, Swabri anasema bado wataendelea kuibua na kukuza vipaji vya nyota wa ndani ambao watafanya biashara kwa klabu nyingine.

“Kusajili nyota wa kigeni haina maana kuwa tumepoteza utamaduni wetu wa kuinua na kuendeleza vipaji vya wachezaji ukiondoa msimu tuliocheza Championship msimu mmoja nyuma tulimuuza Chasambi,” anasema na kuongeza;

“Hadi sasa pia tumewekeza katika kutengeneza kikosi chetu cha ushindani sio kuachia wachezaji kila msimu. Tumebaini kuwa ndio sababu ya kutetereka na kujikuta tunaanza upya msimu hadi msimu,” anasema.

Swabri anasema walikuwa na mchakato wa kusaka vipaji kwa kukusanya wachezaji zaidi ya 800 ambao wamefanya mchujo na kubakiwa na baadhi ambao wamewagawa kwenye makundi tofauti.

“Kuna wachezaji wa umri wa chini ya miaka 17 ambao wamekusanywa pamoja na chini ya miaka 20 makundi haya mawili nina imani yataleta tija kubwa kwa kutoa wachezaji wengi bora kama ilivyokuwa kwa kina Dickson Job, Kibwana Shomary na wengine wengi,” anasema na kuongeza;

“Utaratibu tunaoufanya kwa sasa hauwezi kuonekana kuwa na tija, lakini baada ya miaka kadhaa mbele tutakuja kufanya biashara kubwa na pia tutakuwa na timu za vijana nyingi shindani.”


SITA WAMEPANDA

“Tumepandisha vijana sita na tuna imani watatajwa sana Ligi Kuu Bara kutokana na ubora wao msimu huu. Tumepandisha mabeki watatu, wiungo wawili na washambuliaji wawili ni zao letu kutoka timu ya vijana. Tuna imani watafanya mambo makubwa. Sitaki kuzungumza sana mdomoni, ubora wao utaonekana uwanjani.”

“Omary Mmanga, Harous Evods, Omary Yahya na wengine hawa ni sehemu ya matunda bora ambayo tumeyatengeneza hapa.”


WAGENI KIBAO

“Ni kweli mambo yanaenda kasi na sisi tunaendana na ushindani uliopo, tumeamua kusajili nyota wa kigeni kwa lengo la kuongeza chachu ya ushindani, ligi imebadilika inakua siku hadi siku. Kuchanganya wenyeji na wageni ni kuongeza ubora na ushindani,” anasema Swabri na kuongeza:

“Kuna dalili kubwa dirisha dogo tukaongeza nyota wengine wa kigeni ukiondoa waliopo sasa ambapo kuna baadhi tumechukua kwa mkopo na wengine wamesajiliwa. Ila hii haiondoi utamaduni wetu wa kukuza na kuendeleza vipaji vya vijana.

“Ligi imebadilika ina ushindani na sisi tunataka kuendana na kasi iliyopo kukiwa na wazawa na wageni kutakuwa na chachu ya ubora wa kikosi lakini pia na ushindani kwa wapinzani.

“Ushindani ukiongezeka ndani ya timu kwa wazawa kuchuana na wageni tutakuwa na timu bora shindani ndani na nje ya uwanja tukikutana na wapinzani.

“Hatutasajili kwa majina ya nchi walizotoka, tutazingatia ubora wao na tutaangalia ni namna gani watakuja kuongeza ushindani kwa nyota tulionao sasa kikosini bila kuangalia wa ndani au wageni.”

CHUPUCHUPU KUSHUSHWA DARAJA

Mtibwa Sugar ilianza msimu huu bila ya kuwa na kocha mkuu na jambo hilo liliiweka hatarani kushushwa daraja kama kanuni za Ligi Kuu zinavyosema endapo timu itafikisha mechi sita bila ya kuwa na mkuu wa benchi la ufundi.

Baada ya kucheza mechi tano sasa ikibakisha mechi moja ili kushushwa daraja, Mtibwa imejinasua mtegoni kwa kumnasa kocha Mkenya Yusuf Chippo.

“Tuna benchi ambalo lina vijana Salim Mbonde, Awadh Juma, Shaban Nditi na Dickson Daud. Uwezo wao ulikuwa unahitaji kupata mtu mzoefu ambaye anaweza kuwaongoza, lakini pia awe na uzoefu na soka la Tanzania, Chippo tuliona ni sahihi kwetu,” anasema Swabri na kuongeza;

“Chippo tuliona anafaa kukaa pamoja na makocha wetu ambao wamekuwa na msaada mkubwa hasa kwa timu za vijana, tunaamini atakuwa chachu ya kuongeza uzoefu lakini pia kuisaidia timu kufikia mafanikio.”

Anasema alichelewa kuanza kukinoa kikosi kutokana na matatizo ya kifamilia lakini wao kama viongozi walifanya mazungumzo naye kwa muda na kumalizana naye na sasa amekuwa pamoja na timu na wana imani naye atawafikisha kule wanakodhamiria kufika.

“Tulipokea CV nyingi, lakini tulikuwa na vigezo vyetu kwa kuangalia kocha ambaye atakuwa na ushindani na pia mlezi mwenye uzoefu ili kuendelea kutoa darasa kwa makocha wetu vijana tulionao na pia kujenga timu bora ya ushindani.”


MTIBWA PRESHA KUBWA

Imezoeleka kuwa Simba na Yanga ndio timu zenye presha kubwa kutokana na kuwa na mashabiki wengi Swabri anafunguka kuwa sio timu hizo pekee hadi Mtibwa Sugar kuna presha.

“Wakati naondoka Mtibwa Sugar msimu mmoja kabla ya kushuka kulikuwa na presha kubwa. Nakumbuka niliondoka baada ya mechi tatu tulishinda mechi moja, sare moja na kufungwa moja, mambo yalikuwa mengi sana.

“Nimeondoka timu ikiwa inapitia wakati mgumu, presha ilikuwa ni kubwa na kelele zilikuwa ni nyingi, lakini pia kuna watu wanakuwa na maslahi yao unaweza ukawa unaona hakuna kelele lakini kuna mtu anakaa anapanga mipango yake anakuzidi.

“Hivyo nakiri kuwa kipindi hicho presha ilikuwa ni kubwa na mambo yalikuwa mengi nikachagua kuondoka kwani nilivurugwa sana.”


UMOJA UMEIREJESHA MTIBWA

Baada ya kusota kwa siku 481 katika Ligi ya Championship, Mtibwa Sugar ikarudi Ligi Kuu msimu huu ikiwa na mikakati kibao ya kuhakikisha haifanyi makosa na kuangukia tena ilikotoka.

 Swabri anasema siri ya kurudi kwao Ligi Kuu haraka ni mipango thabiti na umoja baina ya viongozi, wanachama na wachezaji.

Mtibwa ilishuka daraja msimu wa 2023-2024 kwa kumaliza mkiani na imerejea msimu huu baada ya kutwaa taji la Ligi ya Championship iliyoshiriki kwa msimu mmoja tu uliopita wa 2024-25.

“Umoja na mikakati sahihi ndio siri kubwa iliyoturudisha Ligi Kuu, timu iliungana kuanzia viongozi, wachezaji, mashabiki na kila anayetuzunguka. Lengo letu lilikuwa ni moja tu, kuhakikisha tunarudi Ligi Kuu. Ni jambo zuri na tumefanikiwa,” anasema na kuongeza;

“Hayo yamepita. Sasa kilicho mbele yetu ni kuendeleza mazuri yote tuliyoyaonyesha msimu uliopita ili kuiweka timu kwenye ushindani na kufanya makubwa bila kukosea ili tusirudi tulikotoka.”


UBINGWA BADO KWANZA

Baada ya kurudi mikakati imefanyika ikiwa ni pamoja na uwekezaji mkubwa kuanzia kwenye usajili hadi bajeti ili kuhakikisha hawarudi walikotoka.

“Hatuna malengo makubwa sana. Kwanza hatupo kwenye harakati za kuwania taji la Ligi Kuu. Hii ni kutokana na uwekezaji tulionao. Kilichopo na mipango yetu ni kuhakikisha tunabaki Ligi Kuu Bara.

“Kubaki kwetu hatutaki kuwe kwa kusuasua kama misimu miwili nyuma ambayo tulikuwa tunacheza ligi kwa presha na kuangukia katika mechi za kujiokoa kushuka za play-offs. Tunatamani kuona Mtibwa Sugar inamaliza ndani ya tano bora.”

Swabri anasema kwa usajili walioufanya wana kila sababu ya kufikia malengo hayo kwani timu yao ina wachezaji wengi wenye kiu ya mafanikio na wao kama viongozi watapambana kuongeza nguvu kwa kuweka motisha za kutosha.


USAJILI BORA DIRISHA HILI

Mtibwa hivi sasa ina pointi tano, mbili tu juu ya mstari wa kushuka daraja baada ya mechi tano za kwanza za msimu huu, ikishinda mechi moja, sare mbili na vipigo viwili.

Lakini baada ya kumpata kocha mkuu, Mtibwa ina matumaini ya kubadili upepo na kumaliza katika Top 5.

 “Tuna timu ya ushindani hatujarudi kugawa pointi kwa wapinzani, naweka wazi kuwa Mtibwa Sugar imeweka uwekezaji wa kutosha kwenye usajili ambao utatusaidia kuongeza ushindani msimu huu,” anasema Swabri na kuongeza;

“Licha ya kwamba tumetoka Championship na kurudi Ligi Kuu haikuwa kazi ngumu kwetu kushawishi wachezaji kuja Mtibwa Sugar ingawa kuna baadhi tumewakosa lakini kuna ambao wamekuja.”

Anasema ukiondoa Simba na Yanga, jina la Mtibwa Sugar kwenye ligi linawabeba hivyo hawakupata ugumu kufanya sajili kubwa ambazo wanaamini zitakuwa chachu ya mafanikio yao msimu huu.

“Sisi pia ni watekelezaji wazuri kwenye maslahi ya wachezaji hivyo hii inaweza kuwa sababu kubwa ya kupata mteremko kwenye usajili ambao naweza kusema tumefanya usajili bora na utakuwa na manufaa baadaye.”


OSCAR MASAI HAIKUWA RAHISI

Ukiondoa wachezaji wengi kati ya wachache walioondoka Mtibwa Sugar kazi kubwa aliyokuwa nayo Swabri ni kuhakikisha anambakisha nahodha wa timu hiyo, Oscar Masai ambaye ametaja kuwa ndiye alikuwa anampasua kichwa.

“Kipindi ndio natoka Singida Black Stars narudi Mtibwa Sugar kitu ambacho kilikuwa kinaniumiza kichwa ni namna gani nitambakiza Masai ambaye licha ya timu kushuka daraja alikuwa kwenye ubora na alikuwa amepokea ofa nyingi,.

“Hakuna mchezaji aliyetupa shida kumbakiza kama Masai. Haikuwa rahisi, kwani alikuwa na ofa nyingi na ukizingatia alikuwa bora sana. Licha ya timu kushuka, alikuwa amepokea ofa kutoka timu bora ambazo zilimaliza katika nafasi za juu hivyo sio mchezo kumshawishi kubaki kwenye timu ambayo imeshuka daraja;

“Kubaki na Mtibwa na ameweza kuipandisha daraja na bado yupo kwenye ubora. Haikuwa kazi rahisi kwetu kama viongozi. Lakini ukimuondoa yeye kama kiongozi kulikuwa na wachezaji wengine ambao tuliwapambania na wao waliipambania Mtibwa Sugar ili irudi Ligi Kuu.”


BAJETI IMEBADILIKA

“Hata tulivyokuwa Championship bajeti yetu ilikuwa sawa na Ligi Kuu hivyo naamini kilichobadilika ni huku kuna fedha inaongezeka na imekuwa msaada mkubwa kwa uendeshaji wa timu,” anasema na kuongeza;

“Azam Media imekuwa chachu ya kuongeza ushindani kutokana na bajeti ya fedha ambayo imekuwa ikitengwa kwa timu shiriki za LIgi Kuu hivyo huo ndo unaweza ukawa utofauti na msimu uliopita tukiwa Championship.”

Swabri anasema uwekezaji mzuri ndio umekuwa chachu ya mafanikio kwa klabu hivyo wanaamini bajeti nzuri waliyoiweka kwenye timu itakuwa msaada kwao kuweza kufikia malengo ya kuendelea kucheza ligi kwa misimu mingine zaidi mbele bila ya kurudi walikotoka.


WACHEZAJI KUKIMBIA

“Wakati timu inashuka sikuwepo, nilikuwa Singida Black Stars, lakini Mtibwa Sugar kwa kiasi kikubwa wachezaji wote nilikuwa nimesimamia mimi usajili hivyo niliporudi nilikuta kuna wachezaji hawapo.

“Kwa asilimia 10 tuliwapoteza wachezaji ambao hawakutaka kucheza Championship, lakini kuna watu walikuwa tayari kuendelea akiwamo nahodha wa timu licha ya kupata ofa.”

UBINGWA FA, KURUDI LIGI KUU

Licha ya changamoto nyingi akiwa kiongozi wa Mtibwa Sugar, Swabri anafunguka kuwa kuna mazuri anajivunia kwenye uongozi wake na yataendelea kuishi ndani ya timu na kwenye maisha yake binafsi.

“Zipo nyakati nyingi bora lakini nakumbuka ubingwa wa FA na kurudisha timu Ligi Kuu, ubingwa wa Mapinduzi na ubingwa wa timu ya vijana chini ya miaka 20, hizi ni nyakati zangu bora na zimeandikwa kwenye historia,” anasema na kuongeza;

“Nikiwa kiongozi wa Mtibwa Sugar najivunia mataji hayo na bado nina mipango mingi ya kuacha alama ndani ya timu hii ambayo ina historia kubwa ya kukuza na kuendeleza vipaji. Natamani kutengeneza vijana bora ambao watazungumzwa kuwa ni zao la Mtibwa ikiwa chini yangu.”

Swabri anasema ukiondoa mazuri anayojivunia pia kulikuwa na nyakati ngumu ambazo ni pamoja na uamuzi wa kuamua kutoka ndani ya timu hiyo na kwenda kujaribu changamoto nyingine nje ya timu hiyo.


JAMHURI  SOON

Mtibwa Sugar msimu huu inatumia Uwanja wa Jamhuri Dodoma baada ya uwanja wao wa nyumbani kufungiwa kutokana na kuto kukidhi ubora unaotakiwa na Bodi ya Ligi Tanzania na wamefunguka mkakati wa kurudi nyumbani.

“Mpaka sasa tupo kwenye mchakato, tunaamini hadi mwishoni mwa mwezi huu wa Novemba tutakuwa tumekamilisha na kurudi kwenye uwanja wetu wa nyumbani sasa tutaendelea kutumia Jamhuri Dodoma,” anasema na kuongeza;

“Uongozi wetu kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa wa Morogoro tunaboresha pia Jamhuri Morogoro, lakini sisi mpango wetu mkubwa ni kuuboresha haraka Manungu ili tuanze kuutumia huo.”

Swabri anasema endapo watafanikiwa kutengeneza viwanja vyote watakuwa na chachu ya kurudisha furaha ya mashabiki wao ambao walikuwa pamoja nao timu iliposhuka daraja na hata ilivyopanda.

“Tupo kwenye maandalizi ya awali kuna vitu vilitukwamisha kuhusu uwanja lakini nawahakikishia wana Mtibwa Sugar kuwa katika marekebisho tunayofanya tutazingatia ubora wa maagizo kutoka Bodi ya Ligi. Kuhusu uwanja utakuwa unabeba mashabiki wangapi naomba hili nisilizungumze kwa sasa ila vigezo na ubora vitazingatiwa.”


KILICHOMNG’OA MTIBWA

“Muda wa mimi kuondoka ulifika lakini pia uongozi ulikuwa unataka kufanya mabadiliko ambapo mimi sikuwa sehemu ya mipango yao, hiyo ndio ilikuwa sababu ya mimi kuondoka ndani ya Mtibwa Sugar,” anasema na kuongeza;

“Tulifika hatua niliona mimi na wao kwa sera zao waliona hatutawezana na wao hawakuona sababu ya mimi kuendelea kubaki ndani ya timu, hivyo nilichagua kuondoka niliondoka nikapata nafasi ya kujiunga na Singida Black Stars ambayo kipindi hicho ilikuwa ikiitwa Ihefu kabla ya kubadilishwa jina.”

Akizungumzia kurudi tena ndani ya timu hiyo alisema amerudi kwa sababu Mtibwa Sugar ni nyumbani kwake na walimpa vipengele ambavyo hakuwa na sababu ya kukataa kurudi.

“Baada ya makubaliano kwenda sawa na mikakati waliyonipa kuvutiwa nayo niliamua kurudi na niliamini kuwa mikakati sahihi waliyoweka kuhakikisha Mtibwa Sugar inapamba ipo vizuri sikuwa na hiyana kurejea.”