Prime
Mabao ya kikatili yaliyotibua hesabu za wapinzani
Muktasari:
- Wakati ushindani wa Ligi Kuu Bara ukiendelea kushika kasi kwa maana ya kuanzia kwa timu zenyewe shiriki na wachezaji kwa ujumla, Mwanaspoti linakuletea mabao ya kikatili yaliyofungwa, yakitibua hesabu za wapinzani tofauti na matarajio yao.
LIGI Kuu Bara inaendelea kushika kasi kwa sasa ikishuhudiwa upinzani mkali kwa timu zote 16 shiriki ambapo imeshuhudiwa ikiwa ni raundi ya pili na ya lala salama, huku kila mmoja ikijitafutia mazingira mazuri kabla ya mwisho mwa msimu huu.
Wakati ushindani wa Ligi Kuu Bara ukiendelea kushika kasi kwa maana ya kuanzia kwa timu zenyewe shiriki na wachezaji kwa ujumla, Mwanaspoti linakuletea mabao ya kikatili yaliyofungwa, yakitibua hesabu za wapinzani tofauti na matarajio yao.
MHESA V YANGA
Bao alilofunga kiungo mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Ismail Mhesa dakika ya ‘90+1’ dhidi ya Yanga lilitibua hesabu za mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara baada ya mechi hiyo kuisha kwa sare ya kufungana kwa bao 1-1, Machi 21, 2026.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini, Dodoma, Mhesa alifunga bao hilo la kona ya moja kwa moja na kuiwezesha Mtibwa kuondoka na pointi moja baada ya Yanga kufunga mapema dakika ya 23 kupitia kwa Pacome Zouzoua.
Bao hilo la Mhesa lilikumbushia lile la Shiza Kichuya alilolifunga la kona ya moja kwa moja katika mechi ya Ligi Kuu kati ya Simba dhidi ya Yanga, iliyopigwa Kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na kuisha kwa sare ya bao 1-1, Oktoba 1, 2016.
Katika mechi hiyo ya ‘Kariakoo Derby’, Yanga ilipata bao kupitia kwa Amissi Tambwe ambaye kwa sasa ni meneja wa timu ya Singida Black Stars, dakika ya 26 kisha Kichuya akalisawazisha kwa kona iliyomshinda kipa Ally Mustapha ‘Barthez’.
PAUL PETER V AZAM FC
Mshambuliaji wa maafande wa JKT Tanzania, Paul Peter, anaingia katika kumbukumbu ya nyota waliotibua hesabu za wapinzani msimu huu, baada ya kufunga bao la kusawazisha na kikosi hicho kutoka sare ya bao 1-1, dhidi ya Azam FC, Oktoba 1, 2025.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, Peter alifunga bao hilo dakika ya ‘90+2’, baada ya kiungo wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’, kuitanguliza Azam kwa kuifungia bao la mapema kunako dakika ya 42.
Nyota huyo aliyewahi kuichezea timu ya vijana ya Azam FC chini ya miaka 20, hadi kupandishwa ya wakubwa na aliyekuwa pia kocha wa kikosi hicho, Mromania Aristica Cioaba, bao lake lilisababisha miamba hiyo kugawana pointi moja moja msimu huu.
SHAHAME V PAMBA JIJI
Mshambuliaji wa Namungo FC, Abdulaziz Shahame, aliinusuru timu hiyo na kichapo baada ya kufunga bao la dakika ya ‘90+4’ na mechi kuisha kwa sare ya 1-1 kufuatia Pamba Jiji kutangulia kufunga bao kupitia kwa Saphan Siwa mnano dakika ya 19.
Bao hilo la Shahame aliifungia Namungo dakika ya 90+4, likiwa ni la kuchomoa kwa kikosi hicho cha ‘Wauaji wa Kusini’, katika mechi kali na ya kuvutia ya Ligi Kuu iliyoisha kwa sare ya kufungana 1-1, dhidi ya Pamba Jiji, Septemba 18, 2025.
Shahame, anayefananishwa na mshambuliaji wa Manchester City ya England, Erling Braut Haaland, tangu amejiunga na Namungo akitokea TMA ya jijini, Arusha, hilo ndilo bao lake la kwanza la Ligi Kuu, ingawa hadi sasa hajafunga tena kuanzia hapo.
Nyota huyo anakumbukwa zaidi msimu wa 2024-2025, akiwa na TMA, ambapo aliibuka mfungaji bora wa Championship, baada ya kufunga mabao 18, sawa na Andrew Simchimba aliyekuwa Geita Gold japo, kwa sasa anaichezea Mtibwa Sugar na Raizin Hafidh.
MUDRIK V DODOMA JIJI
Mshambuliaji wa Fountain Gate, Mudrik Abdi Shehe ‘Gonda’ aliipa timu hiyo pointi tatu baada ya kufunga bao la dakika ya ‘90+2’, dhidi ya kikosi cha Dodoma Jiji ‘Walima Zabibu’, katika mechi kali ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa, Oktoba 17, 2025.
Katika mechi hiyo, Gonda, alifunga bao hilo na kuipa ushindi Fountain Gate wa 1-0, likiwa ni la kwanza kwake akiwa na kikosi hicho katika Ligi Kuu Bara, tangu alipojiunga na timu hiyo, Januari 2025, akitokea JKU SC ya visiwani, Zanzibar.
Akiwa na JKU SC, Gonda, alifunga mabao manane katika Ligi ya Zanzibar msimu wa 2024-2025, akiungana na nyota wengine wa hivi karibuni walioibukia Bara, baada ya Seleman Mwalimu, Maabad Maulid wa Coastal Union na Yassin Mgaza wa Dodoma Jiji.
TCHAKEI V DODOMA JIJI
Kiungo mshambuliaji wa Singida Black Stars, Marouf Tchakei aliiokoa timu hiyo na kichapo baada ya kufunga bao la dakika ya ‘90+3’, kwa penalti kufuatia Yassin Mgaza wa Dodoma Jiji kutupia pia kwa penalti dakika ya 83 na kuisha sare ya 1-1.
Katika mechi hiyo iliyopigwa, Januari 16, 2026, Penalti ya Dodoma Jiji ilitokana na Geoffrey Kasanga, kufanyiwa madhambi na Kennedy Juma eneo la hatari, huku ya Tchakei, ikisababishwa na Augustino Samson Nsata, aliyeushika mpira eneo la 18.
KARABAKA V NAMUNGO FC
Kiungo nyota, Salehe Karabaka aliinusuru timu ya maafande wa JKT Tanzania na kichapo baada ya kufunga bao muhimu la kuchomoa la dakika ya ‘90’ dhidi ya Namungo FC, hivyo miamba hiyo kutoka sare ya kufungana bao 1-1, Oktoba 18, 2025.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo Mbweni, Karabaka anayecheza JKT kwa mkopo akitokea Simba, alifunga bao hilo na kusababisha kuisha sare ya 1-1, baada ya Ali Salehe Machupa, kuifungia Namungo dakika ya 39.
DUBE V COASTAL UNION
Mshambuliaji nyota wa Yanga, Prince Dube alikifungia kikosi hicho bao la ushindi dhidi ya Coastal Union, dakika ya 88, katika mechi iliyopigwa Kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini, Dodoma, Desemba 7, 2025 na kuisha kwa timu hiyo kushinda 1-0.
KARABAKA V MBEYA CITY
Kwa mara nyingine tena, Karabaka aliiokoa JKT Tanzania na kichapo baada ya kufunga bao dakika ya ‘90+4’ na kusababisha timu hiyo kutoka sare ya mabao 2-2, dhidi ya Mbeya City, katika mechi kali ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa, Oktoba 24, 2025.
Karabaka anayeichezea JKT Tanzania kwa mkopo akitokea Simba, msimu uliopita aliichezea pia Namungo ‘Wauaji wa Kusini’, ambapo hadi sasa amekuwa katika kiwango bora na kikosi hicho cha maafande, akiwa tayari amekifungia mabao sita ya Ligi.
IMORO V TZ PRISONS
Beki wa Singida Black Stars, Ibrahim Imoro, aliipa Singida Black Stars pointi tatu baada ya kufunga bao la dakika ya 90, dhidi ya Tanzania Prisons, katika mechi ya Ligi Kuu Bara, iliyopigwa Kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, Machi 18, 2026.
Katika mechi hiyo, Prisons ilitangulia kupata bao kwa mkwaju wa penalti dakika 3, uliopigwa naa George Mpole, huku Ayoub Lyanga akaisawazishia Singida dakika ya 6, kisha, Imoro ambaye ni Mghana akafunga la pili na la ushindi dakika ya 90.
NGOY V SINGIDA BS
Mshambuliaji nyota wa Namungo FC, Mkongomani Fabrice Ngoy aliiokoa timu hiyo na kichapo baada ya kufunga bao la dakika ya ‘90+1’ dhidi ya Singida Black Stars, hivyo kusababisha kuisha kwa sare ya kufungana kwa bao 1-1, Februari 26, 2026.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Kwenye Uwanja wa Majaliwa Lindi, Singida ilitangulia kupata bao la dakika ya 58, kupitia kwa Mkenya Elvis Rupia kwa penalti, kisha, Ngoy mwenye mabao manane msimu huu akaisawazishia Namungo FC, dakika ya 90+1.
SADICK V MASHUJAA FC
Nyota wa Fountain Gate, Sadick Ramadhan, aliiokoa timu hiyo na kichapo baada ya kufunga bao la dakika ya 90+3, dhidi ya kikosi cha maafande wa Mashujaa, katika mechi iliyopigwa Kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini, Kigoma, Machi 13, 2026.
Katika Mechi hiyo ya vuta nikuvute kwa timu zote kutokana na ushindani mkali, Juma Nyenyezi, aliitanguliza Mashujaa FC kupata bao la dakika ya 55, kisha, Sadick Ramadhan, akachomoa dakika ya 90+3 na pambano hilo kuisha kwa sare ya bao 1-1.