Makocha watano wanaoweza kuinasuru 'Kino Boys' isishuke daraja
Muktasari:
- KMC ambayo inaburuza mkia katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi nane, iliuanza msimu ikiwa chini ya Mbrazil, Marcio Maximo lakini iliamua kuachana na kocha huyo wa zamani wa Taifa Stars, Desemba 6, 2025 baada ya kuongoza timu hiyo katika mechi tisa.
SIKU chache zilizopita, KMC 'Kino Boys' ilitangaza kuachana na kocha wa timu hiyo, Abdallah Mohamed 'Bares' ikiwa ni mabadiliko ya pili kufanywa kwenye benchi lao la ufundi msimu huu wa Ligi Kuu Bara katika jitihada za kujiokoa kwenye hatari ya kushuka daraja.
KMC ambayo inaburuza mkia katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi nane, iliuanza msimu ikiwa chini ya Mbrazil, Marcio Maximo lakini iliamua kuachana na kocha huyo wa zamani wa Taifa Stars, Desemba 6, 2025 baada ya kuongoza timu hiyo katika mechi tisa.
Katika mechi hizo, KMC ilishinda moja, sare moja huku ikipoteza saba, jambo lililowafanya mabosi wa timu hiyo kufanya maamuzi magumu na hatimaye kumpa kazi Bares aliyedumu kwa siku 94, ikiwa ni pungufu ya siku 40 tofauti na mtangulizi wake, Maximo aliyedumu kwa siku 131.
Baada ya Maximo na Bares sasa nani anafuata ambaye atainusuru timu hiyo na janga la kushuka daraja? Hilo ni swali lililopo vichwani mwa wadau na mashabiki wa timu hiyo ya Kinondoni ambayo ilianzishwa mwaka 2014.
Pamoja na hilo hawa hapa makocha watano ambao wanaweza kuisaidia timu hiyo katika kipindi hiki kigumu.
CHARLES MKWASA
Ni miongoni mwa makocha wazawa wenye uzoefu mkubwa na historia ndefu kwenye ligi na timu za taifa, akijijengea sifa kwa akili ya mpira, uongozi na uzoefu wa kimataifa. Uzoefu huu unampa Mkwasa nafasi ya kuelewa changamoto zinazokabili timu kama KMC ambazo zipo kwenye hatari ya kushuka daraja na kujua mbinu za haraka za kuboresha matokeo.
Miongoni mwa timu ambazo amezinoa Mkwasa ni pamoja na Tanzania Prisons, Coastal Union, Ruvu Shooting na Yanga. Pia alifundisha klabu za nje ya nchi kama vile, Al Khaboura ya Oman.
Katika ngazi ya timu ya taifa, Mkwasa aliwahi kuwa kocha mkuu wa Taifa Stars (2015–2017), akiongoza mashindano ya CHAN na mechi za kufuzu AFCON. Uzoefu huu unaonyesha ana uwezo wa kushughulikia timu zenye presha kubwa, akitumia uelewa wa kimkakati na mbinu za kuimarisha wachezaji.
JAMHURI KIHWELO
Msimu wa 2022/23, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ aliteuliwa kuwa kocha mkuu wa KMC FC wakati huo timu ilikuwa ikipambana na hatari ya kushuka daraja, hali iliyoonekana kama ilivyo sasa.
Kocha huyo mwenye uzoefu na maneno mengi alichukua timu iliyokuwa imesalia na michezo michache mbele yake. Katika kipindi kifupi aliibua mikakati ya haraka, kuhamasisha wachezaji na kupanga mbinu za kushinda mechi muhimu, jambo lililoifanya KMC kusalia Ligi Kuu.
Siyo mbaya ikiwa viongozi wa KMC watafikiria kurudi tena kwa Julio, licha ya sasa kuwa kocha wa Mashujaa ya Kigoma, wanachotakiwa kufanya ni kuweka mzigo mezani, ikiwemo kuvunja mkataba wake. Uamuzi huu unaweza kuwa na faida kubwa kwa KMC katika kipindi hiki kigumu cha msimu.
DENIS KITAMBI
Kitambi ni miongoni mwa makocha wazawa wenye uzoefu mkubwa katika soka la Tanzania, aliyewahi kufundisha baadhi ya timu maarufu ikiwemo Simba, Namungo, Geita Gold na Singida Black Stars.
Alitambulishwa kama kocha mkuu wa Fountain Gate FC msimu wa 2025‑26 na kuonekana kwa mara ya kwanza kukiongoza kikosi hicho Agosti 31, 2025 katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Tabora United, kabla ya kuanza kazi rasmi Septemba 20, 2025.
Katika michezo miwili ya ligi aliyoiongoza Fountain Gate FC, ilipoteza dhidi ya Mbeya City 1‑0 na Simba 3‑0, kabla ya kuachana nayo Septemba 28, 2025 kwa makubaliano ya pande zote kwa sababu tofauti ikiwemo changamoto za kikosi.
Kitambi pia alikuwa kocha wa Namungo FC na alikiongoza kikosi hicho na kujenga safu imara ya ulinzi wakati akiitumikia klabu hiyo. Hali hii inaonyesha kuwa ana uzoefu wa kufundisha timu zilizopo katikati ya msimamo wa ligi hivyo anaweza kuwa msaada kwa KMC kama ikimhitaji
ADOLF RISHARD
Ni kocha mwenye uwezo mkubwa wa kubadilika kimbinu. Alipata umaarufu alipokuwa kocha wa Tanzania Prisons kwa vipindi tofauti, akizisumbua timu kubwa kama Simba SC na Yanga SC.
Mtindo wa Rishard unahusisha uelewa wa hali ya mechi na jinsi ya kutumia wachezaji kiakili na kimkakati.
Anaweza kusaidia KMC kuongeza nguvu za ushambulia na kuongeza nafasi za kupata pointi muhimu, jambo ambalo ni muhimu kwa timu iliyo hatarini kushuka daraja.
FRANCIS BARAZA
Ni mmoja wa makocha bora huko Kenya na amethibitisha ubora wake akiwa na Pamba Jiji, akifanya timu hiyo kuwa tishio katika Ligi Kuu Bara.
Licha ya sasa kuwa na mkataba na Pamba Jiji, kwenye fedha siku zote hakuna ambacho kinashindikana. Baraza anajulikana kwa uwezo wake wa kuendesha timu ndogo na kuibadilisha kuwa tishio kwa wapinzani, jambo linalofaa kwa KMC inayohitaji kuongeza pointi haraka na kubaki Ligi Kuu.
Ana uwezo wa kuhamasisha wachezaji na kuunda kikosi chenye ari ya ushindi.