Mattydiola: Simulizi ya Dubai na tumaini la maisha

Muktasari:
- Mwanaspoti limefanya mahojiano (exclusive) na Mattydiola na anayazungumzia maisha yake Simba na anachokifanya Dubai, changamoto alizozipitia zinaweza zikakutoa machozi, lakini alizitumia kama fursa za kutoka kimaisha.
UKITAJA orodha ya wanawake wa shoka basi huwezi kulikwepa jina la Kocha Matty Msetti ‘Mattydiola’, Mtanzania anayefundisha soka katika akademi za Dubai (United Arab Emirates) tangu mwaka 2022.
Mwanaspoti limefanya mahojiano (exclusive) na Mattydiola na anayazungumzia maisha yake Simba na anachokifanya Dubai, changamoto alizozipitia zinaweza zikakutoa machozi, lakini alizitumia kama fursa za kutoka kimaisha.
MAISHA YAKE SIMBA
Anasema miaka miwili aliyofundisha Simba Queens alikuwa akipambania na kutetea maisha ya wachezaji lakini kuna mambo hakuyafurahia na ndicho kilichomwondoka.
Alipenda kutetea masilahi ya wengine kuliko yake, kwani alijua ni moja ya njia ya kuyafikia mafanikio.

“Wanawake tunaojishughulisha na soka tunapitia mambo mengi, najitahidi kuwapambania wengine ili wapate kitu kitakachotafsiri kesho yao, ndiyo maana nilijua Simba napita ila napambania kikubwa ninachostahili kukipata,” anasema Matty.
UNYANYASAJI WA KIJINSIA
Anasema japokuwa aliondoka Tanzania kwa muda mrefu (2022), aliwahi kukumbana na unyanyasaji wa kijinsia, kilichomsaidia ni malezi ya wazazi wake yaliyomjengea kujiamini na kuwa na msimamo wa kuthamini kesho yake kuliko pesa inayoambatana na aibu.
“Kuna maeneo ili upewe kazi wanaanza kuleta ishu za kimapenzi, kwa upande wa wachezaji ili wapewe nafasi za kucheza kuna baadhi ya makocha wanakuwa wanawataka kimapenzi, wengi wamekuwa wakinipigia simu na kulalamika kwa ishu hizo, huwa nawaambia wathamini miili yao kwa ajili ya kesho yao,” anasema kocha huyo na kuongeza;
“Ifikie hatua waheshimu mabinti, wajue wanazipambania kesho zao, hivyo ishu za kuchanganya vipaji vyao na mapenzi siyo kitu kinachopendeza kwa watu wanaonijua mimi wanatambua sipendi mambo ya hovyo, nimenyooka kwa kila kitu na ndiyo maana siwezi kuambatana na mtu asiyependa wasiopenda kusema ukweli.”
VIPI KUHUSU DUBAI
Anasema moja ya changamoto katika nchi hiyo, ni vigumu kuwafokea watoto wala kuwashika. Ikitokea kocha kafanya hivyo anapelekwa mahakamani na hatari zaidi ni kwa mtu mweusi anaweza akapotezwa.
“Watoto wa huku wanaweza wakawa wanakufokea au wanaongea kila wanachojisikia, kwa sababu wazazi wao wana pesa hivyo haitakiwi kuwabughudhi, ikitokea ukawafokea ama kuwagusa basi mtakutana mahakamani, mbaya zaidi kama watoto hawakupendi utaona kazi ni ngumu sana, ila kwa upande wangu nashukuru nakubalika sana,” anasema Matty na kuongeza;
“Katika Akademia ninayofundisha ya Alliance Football Club nimesaini miaka miwili nipo spesho kwa watoto wa kike kuanzia wa umri wa miaka minne hadi 21, wananipenda kuliko makocha niliowakuta hapa, wengi wananieleza mambo mazito wanayoshindwa kuwaambia wazazi wao kutokana na ukali walionao.
“Nimejifunza mambo mengi kupitia hao watoto, Mungu atakaponijaalia kuzaa wa kwangu nitakuwa karibu nao, maana utandawazi ni mkubwa, kuna wakati wanaangalia tv mambo ya ajabu yanayozidi umri wao, lakini kitendo cha wazazi kukosa muda nao inakuwa ni hatari kwao”.

MAISHA YA DUBAI
“Kwa mara ya kwanza nilikuwa Dubai mwaka 2019 na timu ya wanawake iliyokuwa inamilikiwa na mtoto wa Kassimu Dewji, tulikuwa na mashindano ya wiki moja kwa timu za Kiislamu kutoka mataifa mbalimbali duniani kote.
Baada ya mashindano kumalizika timu ilirejea Tanzania ila mimi nikabaki Dubai kwa wiki tatu kwa ajili ya kutafuta kazi ya kufundisha mpira wa miguu,” anasema na kuongeza;
“Kipindi hicho cha mwezi mmoja kilinigharimu zaidi ya Sh6 millioni za Kitanzania kwa ajili ya nauli, malazi, chakula na matumizi madogo madogo, pesa zilipoisha nilikuwa sijapata kazi maisha yakawa magumu na kuamua kuhama kutoka World Trade Center kwenda Deira kwa ajili ya kusubili tarehe ya kurudi Tanzania kwani sikuwa na pesa ya kubadilisha tiketi kwa muda huo, kwa kipindi hicho mlo ulikuwa mkate na soda hadi niliporeja nchini”.
Anachoshukuru Mungu baada ya kurejea nchini ndipo Covid 19 ikawa imepamba moto mwaka 2020, akaamua kuanza kujiendeleza na masomo na kufanya kazi kwa bidii.
“Nilipata hasira ya kufanya kazi kwa bidii na gari langu la kwanza nilinunua Crown la pili Athlete (Sunroof) ndipo changamoto zikaanza kujitokeza nikaamua kuondoka Simba,” anasema.
Japokuwa hakutaka kufafanua ni changamoto gani alikumbana nazo Simba hadi akaamua kuondoka, Mwanaspoti liliwahi kuiona kipande cha video ‘clip’ ya Matty akizungumzia kuna wanawake wanalipwa mshahara mdogo na ikatajwa hiyo ndiyo sababu.
Anasema mwaka 2022 alirejea tena Dubai baada ya kuongeza kiwango cha elimu ya soka na ana leseni B ya Caf akiwa na uhakika wa kujiunga na Goal Academy.
“Nilikuwa nimeshafanya nao makubaliano, hivyo wakanisubili nifike Dubai na walinipokea vizuri na siku ya tatu nikaanza kazi ya kukuza vipaji vya watoto wa kike, sikuwaza kama ningetelekezwa tena kama ilivyotokea mwaka 2019,” anasema na kuongeza;
“Tulianza kazi vizuri lakini mmiliki wa Academy aliingiwa na tamaa baada ya kuona pesa zinakuja kwa wingi, ndipo aliamua kuchukua pesa zote benki na kukimbilia kwao, akatuacha makocha tukiwa tunadai mishahara ya miezi sita, nilikuwa kocha pekee ambaye visa yangu ilibakiza wiki mbili kuisha.
Anaongeza: “Kiikuwa kipindi kigumu kwangu katika maisha yangu, nilikuwa namlilia Mungu kwa nini mimi, mbona napambana kwa ajili ya familia yangu, baada ya wiki hiyo kuisha ndipo nikakutana na mtu aliyekuja kuokoa maisha yangu.
“Nikakutana na mwanamke ambaye mtoto wake nilikuwa namfundisha vipindi vya michezo shuleni, nikamueleza narudi nyumbani kwa sababu sina visa, alitaka kujua sababu, hivyo sikusita kusema ukweli ndipo akaniambia nitakukopesha Dirham 10,000 sawa na Sh7,164,000 milioni ili kutengeneza visa ya miaka miwili, akaniambia nitafute kazi kwani aliamini mimi ni kocha mzuri hivyo nitapata.”

Anasema baada ya kufanikisha mchakato huo na kushika Visa yake, ilimchukua mwezi mmoja kupata kazi ambayo kwa mwezi alikuwa analipwa Dirham 1000 sawa na Sh716,000 ambazo kwa Dubai ilikuwa haitoshi hata kodi, lakini baada ya miezi sita akajiunga na Academy saba tofauti (part-time Coach) zilizomsaidia kupambana na maisha.
Hakukata tamaa. Kwa maisha ya Dubai kuna kupanga kitanda tu na sio chumba kama ilivyo huku. Ilikuaje?
Anasema kitanda hicho ni cha futi mbili ndani ya chumba chenye uwezo wa kuishi watu 10 hadi 15, maisha yasiyotofautiana na ya bweni.
“Katika chumba hicho kunakuwa na friji moja, ukichelewa kuweka vyakula vyako basi inakula kwako, mbaya zaidi kuna wana ndoa, wachumba, wasichana na wavulana, kama umepanga kitanda cha juu wana ndoa wakianza kufanya yao kitanda cha chini hulali kwa amani, kitu kilichokuwa kinanisaidia ni kuvaa headphones, kiukweli kilikuwa kipindi kigumu sana kwangu.”
ANAVYOFANYA KAZI
Matty ambaye kwa sasa maisha yamebadilika anaishi kwenye moja ya nyumba (apartment) zilizoko kwenye ghorofa kubwa huku Dubai na amejipangia utaratibu wake kutokana na kazi na anafurahia maisha.
“Natakiwa kufika ofisini kuanzia saa 2:00 asubuhi tunakutana makocha wote kuandaa programu kwa muda wa saa nne, kisha tunahamia programu ya uwanjani kwa saa nne na kwa siku tunatakiwa kufanya saa nane, ndivyo mkataba wangu unavyosema,” anasema Matty na kuongeza;
“Kipindi cha mfungo wa Ramadhan programu ya uwanjani inaanza saa 10:30 hadi 12:00 kunakuwa na mapumziko kisha tunaendelea saa 2:00 hadi 4:00 usiku baada ya kufuturu.”
Anaelezea soka la nchi hiyo ni la kujifurahisha na halina malengo ya mtu mmoja mmoja na asilimia kubwa ya wawekezaji wa akademi wanatokea Ujerumani, Hispania na England na hajawahi kusikia kuna wachezaji kutoka nchi hiyo wamekwenda kucheza klabu kubwa Barani Ulaya.
“Huku watoto wanaocheza akademi mfano wa kima cha chini analipia Sh2 milioni kwa vipindi 12 vya kujifunza mpira wa miguu, akichoka kucheza mpira wa miguu anakwenda kujiunga na mchezo mwingine kama kikapu, tenisi, ngumi kifupi wanafanya kinachowafurahisha na wazazi wao wanalipia pesa bila shida,” anasema.

LESENI ZAKE CAF-B, UEFA-C
“Kwa Afrika nina leseni B ya CAF na UEFA nina leseni C, bado nina mpango wa kusoma zaidi ili nije nifanye makubwa yatakayofanya nchi yangu ijivunie mimi, pia niwe mfano wa kuigwa kwa wanawake,” anasema Matty anayemtaja Pep Guardiola kumvutia ufundishaji wake na ndiye anayemfuatilia zaidi mbinu zake na ndiyo maana akajiita Mattydiola.
Kabla ya kuanza ukocha alicheza timu mbalimbali za wanawake nchini zikiwamo Shule ya Makongo ambako alisoma bure kutokana na kipaji chake, Vijana Queens, Sayari, Mburahati, Tanzanite ya Magomeni na timu ya Taifa ‘Twiga Stars’.
ALICHOJIFUNZA
Kupitia maisha aliyoishi Dubai, kaapa hatakuja kumdharau mtu awe masikini au tajiri, kitu kizuri zaidi alijifunza kukaa na Mungu kwa ukaribu zaidi na hawezi kufanya jambo bila kuomba.
“Nimemwona Mungu kwa matendo, imenifunza kuwa mnyenyekevu, kujali utu kuliko vitu vinavyotafutwa,” anasema.
MAENDELEO
Anasema hatua alizopiga kimaisha ni kumiliki mashamba, kuwekeza kwenye mfuko wa serikali (UTT), kumiliki Magari, Crown Athlet (Sunroof) ikiwa Tanzania na MG alilonunua Dubai na ndilo gari analoitumia kwa sasa.
“Malengo yangu nikurudi Tanzania, nataka kufungua kituo cha michezo kitakachosaidia kukuza vipaji vya watoto, naamini Mungu ataweka wepesi InshaAllah,” anasema.