Prime
Mo Banka Akataa soka, achagua kufuga #3
Muktasari:
- Staa huyo aliyekuwa mahiri enzi zake kuzungusha boli dimbani anaendelea kuzungumza mengi mengineyo. Twende pamoja!
KATIKA makala mbili zilizotangulia za mahojiano na kiungo wa zamani wa Yanga, Mohamed Banka amezungumza mambo mbalimbali kuhusu soka, ikiwamo kilichomfanya asisikike tena katika ulimwengu wa mchezo huo.
Leo, staa huyo aliyekuwa mahiri enzi zake kuzungusha boli dimbani anaendelea kuzungumza mengi mengineyo. Twende pamoja!
AKATAA SOKA, ACHAGUA KUFUGA
Kutokana na soka la Zanzibar kushindwa kuendelea Banka anasema aliamua kuachana na mpira na kuamua kuwekeza nguvu kwenye ufugaji wa ng’ombe hadi kufikia mahala alikuwa anaitwa mmasai.
“Sola la Zanzibar halikui kwa sababu ya kukosa uwekezaji na wadhamini, hivyo unajikuta unacheza kwa mapenzi tu hakuna unachoingiza hivyo baada ya kuona hivyo niliamua kuachana nalo na kuwekeza nguvu kwenye ufugaji,” anasema na kuongeza;
“Nilikuwa nafuga ng’ombe. Nilikuwa nao wanne kwa Zanzibar kufikia idadi hiyo miaka hiyo ilikuwa ni utajiri, nikabatizwa na jina la mmasai na ng’ombe hao walikuwa wananiingizia fedha kwani pia walikuwa wanatumika kama usafiri kwa kubeba mizigo kama guta.”
Banka anasema alikuwa akitoka na ng’ombe wake ana uwezo wa kurudi nyumbani na fedha nyingi tofauti na akienda kwenye mpira, lakini mzazi wake alikuwa hapendezwi na ufugaji kwani alikuwa anaamini katika kipaji alicho nacho.
“Baba alikuwa hapendi lakini hawezi kunishawishi na wadau wengi wa mpira walikuwa wanavutiwa na uwezo wangu kila nikicheza na walikuja nyumbani kumshawishi baba aniruhusu nirudi nicheze,” anasema na kuongeza mbali na ufugaji pia amefanya biashara ya kuuza vyombo na chuma na kila akitoka mazoezi alienda kwa tajiri yake kuchukua vyombo ili kuzungusha kuuza mitaani.
MILIONI MOJA ILIMRUDISHA UWANJANI
Anasema tajiri mmoja aliyekuwa na timu daraja la pili Zanzibar alimshawishi akachezee timu yake lakini hakumwelewa, akili yake ilikuwa kwenye kufuga. Hata hivyo, tajiri huyo aliyeona kipaji chake alijua akifika kwa mzazi wake mambo yatakuwa mazuri na kuamua kwenda naye.
“Tajiri huyo alikuwa shirika la umeme. Aliniomba nimpeleke kwa baba na alipofika akazungumza naye kuhusu mimi kucheza. Baba alimwambi huyo hataki mpira nimemshawishi sana na alitaka wakubaliane ili nisaini,” anasema na kuongeza tajiri huyo alimwambia baba yake kuhusu mkataba na gharama za kila akija mazoezini jambo ambalo mzee wake alilifurahia.
“Baba akasema haya unataka nini sasa? Utacheza, kisha akamtuma tajiri huyo akachukue fomu kwa ajili ya kunisainisha na wakati ameufuata, baba alizungumza na mimi na ulipokuja nikasaini, ulikuwa wa gharama ya Sh1 milioni na baada ya mechi sita tu timu zote za ligi kuu zikaonyesha nia ya kunihitaji,” anasema Banka na kuongeza kitendo cha kukubali kucheza mzee wake alifurahi na kuamua kupika pilau.
TIMU YA LIGI KUU
Anasema kiwango chake kilisababisha asajiliwe na Chuoni inayocheza ligi kuu kwa mkataba wa miezi sita, lakini hakudumu kutokana na masilahi na yalikuwa chini tofauti na timu ya daraja la pili aliyotoka jambo lililomfanya arudi zake kufuga.
“Niligundua ile timu ya daraja la pili ilikuwa inanipa hela nzuri zaidi ya Chuoni nilikokuwa nalipwa Sh2000 baada ya mazoezi bila ya mshahara. Yule tajiri alinilipa vizuri, nikashangaa ligi kuu pesa ni kidogo na kuamua kurudi kufuga,” anasema na kuongeza akiwa Chuoni ndipo alipokutana na marehemu Ibrahim Rajab ‘Jeba’ ambaye anakiri alikuwa mchezaji mzuri na ndiye aliyemsaidia hadi akacheza Ligi Kuu Bara.
JEBA ALIVYOMPELEKA BARA
Anasema ni katika mechi ya mchangani ya kirafiki ndipo Jeba alivyotambua ana kipaji kikubwa na baada ya mechi alimfuata na kuzungumza naye.
“Yeye alikuwa timu pinzani. Nilimsumbua sana katika mechi hiyo na baadaye aliniuliza unacheza timu gani, nikamwambia nilikuwa Chuoni lakini sijaenda nina mwaka hadi sasa,” anasema na kuongeza;
“Akasema wewe unakipaji sana na siyo cha kucheza Zanzibar. Akaniambia yeye anacheza Mtibwa Sugar na kunuliza kama nikipata nafasi ya kufanya majaribia kwa Wakata miwa hao nitaenda. Nikakubali na akachukua namba yangu ya simu na baada ya mwezi mmoja alinitafuta na kuniambia bosi wake amekubali.”
JEBA ABEBA MAJUKUMU, ASAJILI MTIBWA
Anamtaja Jeba amefanya makubwa katika soka lake kwani kama sio yeye na kipindi hiki ufugaji mjini umepigwa marufuku hajui angekuwa wapi kwani ng’ombe mwanzo ndio waliotumika kwa usafirishaji na sasa kuna bodaboda.
Anasema baada ya kuambiwa aende Bara kufanya majaribio, alimwambia Jeba hakuwa tena mchezaji na hata jezi na viatu hakuwa navyo na ndipo hapo alipojua kweli Jeba amedhamiria akacheza Mtibwa.
“Jeba aliniuliza navaa viastu saizi gani nikamwambia namba tisa na akaniambia anazo pea nane zitamtosha na kumtaka aende mara moja.” anasema na kuongeza;
“Akaniambia kesho yake nipande boti ya saa tisa na akanitumia tiketi na pesa laki moja na nikaanza safari.”
Anasema alivyofika Magomeni, Dar es Salaam aliwakuta wachezaji wa timu hiyo, kina Shaban Nditi ndio mastaa na makocha Salum Mayanga na Zuberi Katwila ndio walikuwepo na alianza kufanya nayo mazoezi.
“Kipindi hicho Mtibwa ilikuwa imewauza Mzamiru Yasin, Mohammed Ibrahim na Shiza Kichuya hivyo ikawa inatafuta wachezaji wa kuziba nafasi zao na tayari alikuwa amepatikana mmoja Rashid Mandawa nafasi ya ushambuliaji hivyo tukapita mimi na Stamil Mbonde, tukasajiliwa.”
MECHI NA SIMBA AMSHANGAZA BOSI
Anasema licha ya kusajiliwa, alikaa benchi katika mechi sita kwani kocha hakuwa amemwelewa na kiungo mwingine, Ally Makalani ndiye aliyekuwa anapata nafasi, hata hivyo, mechi iliyofuata dhidi ya Simba bosi Jamal Baysar akamfuata.
“Siku hiyo nikasema sikubali. Nikaanza mazoezi ya kukimbia kuanzia Manungu hadi Turiani. Nilikuwa nakimbia asubuhi huku nimejifunga chupa.”
“Siku ya mechi nilikuwa sehemu ya kikosi ila nilianzia benchi, nakumbuka kipindi cha kwanza tulikuwa tumefungwa bao moja na wakati mambo yakiendelea kuwa magumu, kocha akageuka nyuma nikiwa benchi na kuniambia nipashe,” anasema na kuongeza;
“Nilicheza kwa kiwango kikubwa sana. Sitasahau kwani baada ya mechi bosi Jamal Baysar alikuja vyumbani na kuhoji kwa nini situmiki na akanipa laki moja kama zawadi na kunitaja kama mchezaji bora wachezo.”
KAZIMOTO AMWOMBEA NAMBA
Anasema baada ya mechi hiyo, pia Mwinyi Kazimoto aliyekuwa Simba, alimfuata Henry Joseph Shindika aliyekuwa naye timu moja na kuhoji kuhusu kiwango chake.
“Alimuuliza kwa nini sianzi katika kikosi chetu kwani nina kipaji kikubwa kinachoweza kuisaidia timu. Aliniuliza ninapotokea, nikamwambia Zanzibar, akasema ndiyo maana una kipaji kikubwa na timu inatakiwa ikuchezeshe sana kama inataka matokeo na hapo ndiyo ukawa mwanzo wangu wa kucheza na hata nikiumia wananiomba nicheze kwani walinitegemea sana,” anasema na kuongeza kuna kipindi aliamua kuwajaribu kwa kuwaambia hawezi kucheza ili aone umuhimu wake na walimzingatia sana.
“Kuna muda mazoezini namwambia kocha nina tatizo kwenye kifundo cha mguu ‘enka’. Anasema tayari wameshakuroga, haiwezekani utoke timu ya taifa urudi uingie moja kwa moja twende kwa mganga,” anasema na kuongeza wanaenda kweli na mganga anamchanja na akirudi mazoezini anafanya vizuri na kocha anakubali ni kweli alirogwa.
TOFAUTI LIGI BARA, ZANZIBAR
Anasema tofauti ni kubwa na kubwa ni ugumu akiitaja Ligi Kuu Bara kutokana na ushindani na mchanganyiko wa nyota kutoka mataifa mbalimbali.
“Kuanzia uwekezaji hadi ugumu. Ligi ya Bara ni ngumu tofauti na Zanzibar, pia kuna ushindani kutokana na wachezaji wengi kutoka mataifa mbalimbali. Pia utimamu wa mwili kwa Bara upo juu tofauti na Zanzibar ingawa kuna vipaji vya mpira,” anasema na kuong4eza utimamu wa mwili ni tatizo kutokana na mazingira ya ligi na wachezaji hawakai kambini kama ilivyo Bara.
“Zanzibar hakuna mwendelezo. Mchezaji anatoka mazoezi anarudi nyumbani na kukutana na kazi nyingine inayomfanya atoe alichokiingiza mazoezini. Bara mchezaji anakaa kambini kujiweka tayari kwa mechi, lazima awe fiti,” anasema na kuongeza Zanzibar vipaji ni vingi sana kwa sababu watoto wengi wanakua wakijifunza mpira kutokana na kuzungukwa na viwanja vingi mtaani na wachezaji wengi wanakuzwa katika mazingira ya mpira wakiwa na umri mdogo.
AITAJA SINGIDA
Anasema amekuwa akifuatilia mwamko wa soka nchini ni mkubwa kutokana na uwekezaji na usajili, akiitolea mfano Singida Black Stars ambayo imeongeza changamoto ya ushindani katika ligi na michuano ya kimataifa.
“Ligi inakua msimu hadi msimu. Kuna ushindani unaongezeka, mfano uwepo wa Singida Black Stars unaleta changamoto ya ushindani kwa timu kama Simba na Yanga ambazo ilizoeleka kila msimu asipokuwa bingwa huyu basi mwngine hivyo kama kutakuwa na ongezeko la timu bora kama Singida basi ubora wa ligi utaendekea kupaa,” anasema na kuongeza:
“Pia uwekezaji kwenye klabu na sajili bora zimeongeza chachu ya ukuaji. Ushindani kwa wachezaji wa ndani na kimataifa pia. Siyo rahisi mgeni kumng’oa mzawa bila ushindani,” anasema Banka na kuongeza kama zikipatikana timu tano kama Singida ambazo zitatoa ushindani, basi nchi itakuwa na timu bora ya taifa ‘Taifa Stars’.
MUDATHIR, FEI TOTO
Kuna nyota kibao wanatajwa ni bora na hasa wageni, lakini anawataja nyota wazawa ambao wanavipaji vikubwa na namba wanazocheza.
“Wazawa wapo wengi bora na wanafanya vizuri. Mudathir Yahya na Feisal Salum ni wachezaji wazuri sana wana uwezo mkubwa hawa kwenye timu yangu wote nawapanga siachi mtu benchi,” anasema na kuongeza;
“Mudathir anacheza namba nane au sita kwa sababu ni namba zote ambazo ana uwezo mkubwa wa kucheza vizuri, halafu Fei Toto namchezesha nane au kumi, najua atanipa vitu sahihi.”
Banka anasema nafasi hizo kwa nyota hao walikuwa wanazicheza hata timu ya taifa ya Zanzinar ‘Zanzibar Heros’ na kama Muda akianza sita basi Fei anacheza nane hivyo anaamini wakicheza pamoja wanafanya kitu kizuri zaidi.
AMKINGIA KIFUA BACCA
Ibrahim Hamad ‘Bacca’ amefungiwa mechi tano za ligi kuu baada ya kumchezea rafu mchezaji wa Mbeya City kwenye mchezo wa ligi timu yake ikiambulia suluhu kwnye Uwanja wa Sokoine Mbeya, Banka anamtetea nyota huyo hajatendewa haki.
“Bacca ni beki bora anatakiwa kuendeleza ubora wake, kwa kilichofanyika hivi karibuni kwa kumfungia mechi tano, sijui nisemeje, sijui niseme kaonewa ila acha niwaachie wenyewe, lakini kwa mchezaji sio kitu kizuri hasa kwa Yanga ya sasa,” anasema na kuongeza inaweza pia ikasababisha Bacca akapoteza namba kikosini kwani mechi tano ni nyingi kwa mchezaji aliyekuwa anampisha kuonyesha kiwango na kumshawishi kocha.
“Yaani uniachie mimi mechi tano urudi utegemee kuchukua namba, siyo kweli labda niwe sina kiwango.”
UFAFANUZI KUHUSU TATUU
Nyota huyo wa zamani wa Yanga amechora tatuu tatu mkononi, moja begani amechora namba nane, mkononi nyavu na mkono mwingine mawingu na nyota na hapa anaeleza maana zake.
“Unajua vitu vingine vinatokea tu na unajikuta unaingia mtego wa ibilisi, ndio kama hivi licha ya kuwa muislam na kupita madrasa nafahamu hii haitakiwi lakini nimechora na naenda msikitini kwa kujificha zisionekane.”
“Nimetumia Sh400,000 kuchora zote. Hii ya nyavu ni kwa sababu mimi ni mfungaji na ya mawingu na nyota ni kwa sababu mimi ni ‘staa’, mimi ni brandi.”
TUKIO GUMU LA SOKA
Kwenye soka kuna wakati wa raha na huzuni kama anavyothibitisha Banka kwa kutaja tukio lake gumu alilowahi kukutana nalo ukiondoa kuugua ugonjwa usiojulikana.
“Kuna siku tulienda Pemba kwenye bonanza sehemu kunaitwa Bungi, kuanzia asubuhi saa mbili hadi saa kumi na huko haina kupumzika unatoka baada ya dakika unaingia kucheza,” anasema na kuongeza;
“Baada ya kumaliza huo mchezo tulipewa Sh5,000, nilichoka sana, nilikuwa hoi na tulienda tulikuwa hatufahamu tunapewa bei gani na matarajio yalikuwa elfu 20,” anasema anasema na kuongeza tukio lingine alialikwa kucheza mechi na bingwa alipewa kiroba cha kilo 20 za mchele, licha ya yeye kuambulia Sh30,000, pia tulipewa maembe na mafenesi kama zawadi,” anasema na kuongeza licha ya changamoto hizo lakini anakumbuka baada ya usajili wa kwanza aliopewa Sh1000,000 pia alisajiliwa na kikosi cha timu ya vijana ya Arizona na alipewa baiskeli na viatu vya mpirana ndiyo ulikuwa usajili mkubwa katika kikosi hicho kwani ndiyo ilikuwa timu yenye hela.