Mpanzu sasa ndo ailipe Simba
Muktasari:
- Kwanza ni kwa sababu mshambuliaji huyo alikuwa akihusishwa mara kwa mara kwenda upande wa pili tena kuna baadhi ya watu walisema hadi ameshasaini mkataba wa awali na timu mojawapo kubwa hapa nchini.
HABARI ya winga Elie Mpanzu Kibisawala kuongeza mkataba wa kuichezea Simba hadi mwishoni mwa msimu wa 2027/2028 ilitikisa sana mwanzoni mwa wiki hii.
Kwanza ni kwa sababu mshambuliaji huyo alikuwa akihusishwa mara kwa mara kwenda upande wa pili tena kuna baadhi ya watu walisema hadi ameshasaini mkataba wa awali na timu mojawapo kubwa hapa nchini.
Lakini pili ni namna Mpanzu anavyotazamwa kama mmoja wa wachezaji wazuri wa kigeni ambao hivi sasa wanacheza katika ligi yetu.
Hapa kijiweni tunaamini kwamba mkataba huo mpya ambao Simba imempa Elie Mpanzu, ni deni kwa nyota huyo kutoka DR Congo ambaye zamani aliwahi kuitumikia AS Vita Club kabla ya kuja nchini.
Mchezaji huyo sasa ana kazi kubwa ya kuisaidia Simba kwa vile imeonyesha kumpa thamani kubwa hadi ikaamua kubaki naye kwani hata ingeamua kutomuongezea mkataba isingekuwa jambo la kushangaza.
Tangu ajiunge na Simba bado hajawa mchezaji ambaye klabu hiyo inaweza kusimama hadharani na kusema siku za usoni anastahili kuwa miongoni mwa magwiji wake kwa sababu bado hajawa na muendelezo wa ubora na mchango kwa timu. Miezi michache ya mwanzoni aliyoichezea Simba baada ya kujiunga nayo, alionyesha kiwango kizuri ambacho kiliwapa wengi matumaini kuwa atakuwa msaada mkubwa kwa timu.
Lakini msimu huu mambo yanaonekana kumuendea tofauti kiasi ambacho hadi amepoteza nafasi katika kikosi cha kwanza cha Simba huku hata akiwa anaingia uwanjani, makali yake mara kwa mara hayaonekani. Simba imeshatimiza wajibu wake kwa Mpanzu kwa kumuamini na kumpa mkataba mpya. Ni wajibu wa mchezaji sasa kurudisha kwa timu.