MWENDO WA MABAO! Arteta akinasa bunduki hizi Arsenal inajipata kwenye ligi

Muktasari:
- Hata kama, Gabriel Jesus na Kai Havertz wasingekuwa majeruhi, kimsingi Arsenal bado inahitaji nguvu mpya kwenye safu yake ya ushambuliaji, kusajili straika mwenye uhakika wa kuwafungia mabao ili kushindana kikwelikweli kwenye mbio za kufukuzia mataji.
LONDON, ENGLAND: MAJERUHI yameilazimisha Arsenal kumchezesha kiungo Mikel Merino eneo la mshambuliaji wa kati, jambo lililomfanya Kocha Mikel Arteta kubebeshwa lawama za kushindwa kusajili straika dirisha la Januari.
Hata kama, Gabriel Jesus na Kai Havertz wasingekuwa majeruhi, kimsingi Arsenal bado inahitaji nguvu mpya kwenye safu yake ya ushambuliaji, kusajili straika mwenye uhakika wa kuwafungia mabao ili kushindana kikwelikweli kwenye mbio za kufukuzia mataji.
Kwa maendeleo ya soka la kisasa, straika anahitajika kuwa na uwezo wa kupangua ngome ya timu pinzani mwenyewe na hicho ndicho ambacho Arsenal inakosa ili kuwa kikosi hatari.
Lakini, ni straika gani wa aina hiyo Arsenal anaweza kumsajili kwenye dirisha lijalo amalizane na tatizo la kuwa na uhakika wa mabao na hatimaye kunyakua mataji?

Viktor Gyokeres - (Sporting Lisbon & Sweden)
Jina la kwanza kwenye orodha ya mastraika wanaohusishwa na Arsenal ni mkali wa Sporting Lisbon na timu ya taifa ya Sweden, Victor Gyokeres, 26.
Gyokeres ni moja ya mastraika wa kiwango cha juu Ulaya kwa misimu miwili ya karibuni na msimu huu amehusika kwenye mabao 50 katika mechi 41 alizochezea Sporting na msimu uliopita, alihusika kwenye mabao 58.
Kutokana na hilo na ndio maana hata bei yake ipo juu, Pauni 83 milioni. Straika huyo anauwezo wa kufunga kwenye eneo lolote lile, licha ya kwamba utulivu wake kidogo unashida anazungukwa na mabeki wengi kwa pamoja.

Victor Osimhen - (Galatasaray & Nigeria)
Osimhen, 26, ni mchezaji mwenye uzoefu wa soka la kimataifa, ambapo kwenye kikosi cha Nigeria amecheza mechi 39 na kufunga mabao 23, huku kwenye klabu akichangia mabao 166 katika mechi 253.
Nyakati zake kwenye kikosi cha Napoli, alikosaidia timu hiyo kushinda taji la kwanza la Serie A tangu zama za Diego Maradona, zilionekana kufika mwisho na kupelekwa kwa mkopo Galatasaray, ambako msimu huu amefunga mabao 26 na asisti tano katika mechi 30 za michuano yote na kuwa na mabao sita katika mechi saba za Europa League.
Tofauti yake na Gyokeres ni kwamba Osimhen hahitaji kuachiwa nafasi kubwa kufunga, hata upenyo mdogo tu, anakuadhibu. Bei yake ni Pauni 62 milioni.

Hugo Ekitike - (Eintracht Frankfurt & Ufaransa)
Eintracht Frankfurt kwenye Bundesliga imejitengenezea umaarufu mmoja wa kuwa shule ya mastraika matata na kwa miaka ya karibuni imeibua kadhaa na kuwauza kwa mkwanja mrefu. Straika huyo Mfaransa mwenye umri wa miaka 22, anaonekana ni zao jingine kutoka kwenye klabu hiyo, ambaye anaweza kunaswa kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi, huku bei yake ikitajwa kuwa ni Pauni 67 milioni.
Ekitike amefunga mabao 19 katika mechi 38 za michuano yote aliyocheza msimu huu na alijiunga na Frankfurt mwaka jana tu akitokea Paris Saint-Germain ya Ufaransa.
Ekitike ni mchezaji anayeweza kushambuliaji kupitia pande zote kwenye fowadi na amekuwa na uwezo wa kuchukua mipira nyuma na kupanda nayo bila ya shida yoyote.

Benjamin Sesko - (RB Leipzig & Slovenia)
Ishu ya Arsenal kutaka straika imekuwa kawaida sasa na kuna baadhi ya washambuliaji hao majina yao kuhusishwa na timu hiyo imekuwa kawaida. Moja ya majina hayo ni straika wa RB Leipzig na timu ya taifa ya Slovenia, Benjamin Sesko, 21.
Arsenal imehusishwa na straika huyo kwenye madirisha yote mawili yaliyopita la usajili, lakini Sesko aliamua kubaki kwenye soka la Bundesliga msimu huu. Hadi sasa, straika huyo ameshafunga mabao 17 katika mechi 36, ikiwamo manne kwenye mechi nane za Ligi ya Mabingwa Ulaya. Sesko ni mrefu, ana nguvu na kasi ambayo imemfanya kuhama kwenye maeneo ya kushambulia kwa haraka sana na kuleta madhara kwa timu pinzani. Eneo hatari zaidi la straika huyo ni mashuti yake, lakini miguu yake pia ikiwa na ufundi mkubwa.

Sehrou Guirassy - (Borussia Dortmund & Guinea)
Straika mwingine kwenye orodha hii ni mkali wa Borussia Dortmund na Guines, Sehrou Guirassy, 29, huku bei yake ikitajwa kwamba anaweza kuigharimu Arsenal, Pauni 40 milioni tu.
Baada ya kuanza kwa kasi hafifu kwenye maisha yake ya soka, Guirassy aliibuka na kuwa tishio msimu uliopita alipokuwa kwenye kikosi cha VfB Stuttgart kabla ya kuhamia kwenye timu nyingine ya Ujerumani, Dortmund.
Guirassy amefunga mabao 24 katika mechi 36 alizocheza msimu huu, ikiwamo mabao 10 aliyofunga katika mechi 12 alizokipiga kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Guirassy ni mshambuliaji anayecheza juu sana, hivyo akitua Arsenal atakwenda kuwafundisha mstraika waliopo kwenye timu hiyo namna ya kufunga wakiwa kwenye msitu wa mabeki. Guirassy ni mchezaji hatari ndani ya boksi.

Samu Omorodion - (FC Porto & Hispania)
Kuibuka kwa straika Samu Omorodion kumekuwa gumzo kubwa Ulaya nzima. Straika huyo kutoka timu ya daraja la nne huko Hispania misimu miwili iliyopita hadi kwenda kuwa mshambuliaji matata kabisa anayeibukia kwa kasi kwenye soka la Ulaya.
Straika huyo kinda ambaye awali alitua Atletico Madrid, aliibuka na kuanza kucheza kikosi cha kwnaza huko Granada na alikuwa akihusishwa sana na Chelsea kabla ya kwenda kujiunga na FC Porto. Hadi sasa msimu huu, Omorodion amefunga mabao 20 katika mechi 34, huku mabao sita amefunga katika mechi tisa kwenye mikikimikiki ya Europa League.
Omorodion, 20, ni mshambuliaji anayetumia nguvu sana na tishio anapokuwa kwenye eneo la timu pinzani, hasa anapokaribia kwenye penalti boksi. Bei yake ni Pauni 84 milioni.

Liam Delap - (Ipswich & England)
Kiwnago cha Liam Delap kimejipambanua tofauti kabisa na kikosi kizima cha Ipswich Town kwenye Ligi Kuu England. Straika huyo mwenye umri wa miaka 22, anaitumikia timu ya taifa ya England kwa kikosi cha U-21 na aliibukia kutoka kwenye akademia ya Manchester City kabla ya kutimkia zake Suffolk jumla kwenye dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana.
Ni straika mwingine anayetumia sana nguvu na kasi mwenye uwezo pia wa kuhama na mabeki wa timu pinzani kutokana na mikimbio yake akiwa hana mpira kwenye eneo la timu pinzani. Hadi sasa amefunga mabao 10 katika mechi 31, huku akiwa na changamoto kubwa ya kuipambania timu hiyo ili isishuke kutoka kwenye Ligi Kuu England msimu huu. Delap uwezo wake mwingine ni kukimbia na mpira kutoka nyuma kwenda mbele, kitu ambacho amekuwa akiwatesa sana mabeki wa timu pinzani.