Nani katisha, nani kazingua usajili dirisha dogo?
Muktasari:
- Sasa wakati nyota wapya wakisubiriwa kwa hamu na shauku kubwa na mashabiki kuonyesha uwezo wao, Mwanaspoti linakuletea makala ya timu zote 16, ikielezea usajili umezingatia kweli mahitaji kutokana na changamoto zao au wamezingua. Tiririka!
WAKATI Ligi Kuu Bara ikirejea kuanzia Februari Mosi baada ya kupisha michezo ya Kombe la Mapinduzi iliyokuwa ikifanyika visiwani Zanzibar, tumeshuhudia klabu zikifanya uhamisho wa nyota mbalimbali kutokana na mahitaji yaliyoonekana kwao.
Sasa wakati nyota wapya wakisubiriwa kwa hamu na shauku kubwa na mashabiki kuonyesha uwezo wao, Mwanaspoti linakuletea makala ya timu zote 16, ikielezea usajili umezingatia kweli mahitaji kutokana na changamoto zao au wamezingua. Tiririka!
AZAM FC
Matajiri hawa wa Jiji la Dar es Salaam hawajafanya usajili mkubwa katika dirisha dogo la Januari ingawa wamezingatia tu mahitaji yao, kutokana na wengi waliopo kuonekana kufiti mfumo wa kocha mkuu wa kikosi hicho, Mmorocco Rachid Taoussi.
Eneo moja muhimu ambalo kikosi hicho imeboresha ni beki wa kati kwa kumsajili, Zouzou Landry, raia wa Ivory Coast na hii ni baada ya aliyekuwa nyota wa timu hiyo, Yannick Bangala kuondoka na kujiunga na AS Vita Club ya kwao DR Congo.
Azam FC iliyopo nafasi ya tatu na pointi 36, baada ya mechi 16, inapigania ubingwa wa Ligi Kuu ilioutwaa mara moja tu msimu wa 2013-2014, huku ikimuongeza mshambuliaji kinda, Zidane Sereri aliyetoka Dodoma Jiji.
YANGA
Kikosi hiki cha kocha Mjerumani, Saed Ramovic hakijafanya usajili mkubwa kama ilivyotegemewa ikiwaongeza mastaa wawili ambao ni beki wa kulia, Israel Patrick Mwenda aliyetoka Singida Black Stars na mshambuliaji, Mkongomani Jonathan Ikangalombo.
Yanga inayotetea ubingwa wake wa Ligi Kuu Bara iliouchukua kwa misimu mitatu mfululizo, iko nafasi ya pili na pointi 39, nyuma ya wapinzani wao Simba wenye 40, baada ya kila timu kucheza michezo 15.
Mwenda ni moja ya usajili bora baada ya kuumia kwa Yao Kouassi na tayari ameshaanza kuonyesha ubora wake, japo kwa sasa anasubiriwa Ikangalombo aliyetokea AS Vita Club ya kwao DR Congo, kuona ni jinsi gani atapenya kwenye kikosi cha kwanza.
SIMBA
Kikosi hiki ambacho kinaongoza Ligi Kuu Bara na pointi 40, ni kama hakijafanya usajili wa kutisha baada ya kumuongeza tu winga, Elie Mpanzu Kibisawala kikosini, ambaye alikuwa na timu hiyo tangu mwanzoni ila ameanza kuichezea dirisha dogo.
Simba inayonolewa na kocha Fadlu Davids imecheza akili kubwa kwa kutoongeza nyota wengi ambao huenda wangetibua mifumo yake kwa wengine waliopo, huku akiwa pia hajaruhusu mchezaji yeyote wa kikosi cha kwanza kuondoka dirisha dogo.
SINGIDA BLACK STARS
Unapotaja timu bora za msimu huu hutoiacha Singida Black Stars kutokana na mastaa bora waliopo ndani ya kikosi hicho chenye maskani yake mjini Singida, ambapo hadi sasa imeshaonyesha kwa vigogo nchini wa Yanga, Simba na Azam FC.
Kikosi hiki ambacho kwa sasa kiko chini ya kocha, Miloud Hamdi mwenye uraia pacha wa Algeria na Ufaransa, imefanya pia usajili mzuri kwa kuwaongeza beki wa kati, Frank Assinki aliyetokea Inter Allies FC na mshambuliaji, Jonathan Sowah.
Usajili wa Mghana Jonathan Sowah aliyetokea Al-Nasr Benghazi ya Libya ndio unaotazamwa zaidi ni kwa jinsi gani ataweza kushindania nafasi na Mkenya Elvis Rupia ambaye ndiye mfungaji kinara wa Ligi Kuu Bara hadi sasa akiwa na mabao manane.
Sowah amejiunga na timu hiyo kuchukua nafasi ya nyota wa zamani wa Yanga, Joseph Guede aliyejiunga na Al Wehdat Club ya Jordan, huku akiwa na deni kubwa la kukipambania kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu.
TABORA UNITED
Kikosi hiki cha ‘Nyuki wa Tabora’ kimewasapraiz vigogo wa soka nchini Yanga na Azam FC ambao walichezea vichapo, huku ikibadilika kiuchezaji tangu ujio wa kocha, Mkongomani Anicet Kiazayidi aliyechukua nafasi ya Mkenya Francis Kimanzi.
Tabora imefanya maboresho madogo na ya kimkakati kutokana na nyota wengi kutoondoka kikosini baada ya kumuongeza kiungo wa ukabaji Mcameroon, Martial Zemba Ikoung aliyetokea Union Touarga Sportif, akichukua nafasi ya Mnigeria Morice Chukwu.
Chukwu amerejea Singida Black Stars baada ya kuichezea Tabora kwa mkopo, huku nyota wengine wapya ni makipa, Jean-Noel Amonome na Fikirini Bakari, beki wa kushoto Yassin Mustapha aliyepita Yanga na mshambuliaji wa kati, Emmanuel Mwanengo.
Mwanengo aliyekuwa anakichezea kikosi cha FK Vakhsh Bokhtar kutoka Tajikistan, anategemewa kuongeza ushindani wa eneo hilo kwa kushindana na Heritier Makambo na Yacouba Songne ambao wamekuwa chachu ya timu hiyo kufanya vizuri msimu huu.
FOUNTAIN GATE
Licha ya ubora wa kikosi hiki kwenye kufumania nyavu kikiongozwa na washambuliaji, Seleman Mwalimu mwenye sita na Edgar William aliyefunga matano, moja ya changamoto yao kubwa tangu msimu huu umeanza ni kwenye eneo lao lote la ulinzi.
Fountain ndio timu inayoongoza kwa kufungwa mabao mengi hadi sasa ikifanya hivyo mara 32, japo kuwaongeza Jackson Shiga na Cosmas Lucas waliotokea Coastal Union na Said Mbatty aliyekuwa Tabora United ni dhamira tosha ya kutibu eneo hilo.
Kikosi hicho ambacho kinanolewa na kocha Mkenya Robert Matano aliyechukua nafasi ya Mohamed Muya aliyetimuliwa, kama pia haitoshi ikamuongeza beki wa kati, Shabani Pandu Hassan aliyekuwa anachezea kikosi cha JKU kutoka visiwani Zanzibar.
MASHUJAA FC
Kikosi hiki cha ‘Mapigo na Mwendo’, kinachonolewa na kocha, Abdallah Mohamed ‘Baresi’, kimekuwa hakina uwiano mzuri kwa maana ya safu bora ya ulinzi na ushambuliaji, ambapo hadi sasa kimefunga mabao 14 na kuruhusu pia 14, kwenye nyavu zake.
Katika eneo la ushambuliaji kimefanya maboresho kwa kuwaongeza, Danny Lyanga aliyetokea JKT Tanzania na Emmanuel Martin kutoka Dodoma Jiji, baada ya kuondoka kwa aliyekuwa nyota wa timu hiyo, Ismail Mgunda aliyetua AS Vita Club ya DR Congo.
Eneo la ulinzi imefanya maboresho ya beki wa kushoto tu, Yahya Mbegu aliyetokea Singida Black Stars hivyo, kusubiriwa ni kwa jinsi gani itaweza kuendana na ushindani mzunguko huu wa pili, baada ya kukusanya pointi 19 tu, katika michezo 16.
JKT TZ
Changamoto kubwa ya kikosi hiki cha maafande wa JKT Tanzania ni kwenye maeneo mawili muhimu ambayo ni ulinzi na kwenye ushambuliaji, ambapo hadi sasa kimefunga mabao 10 na kuruhusu 12, katika michezo yake 16 iliyocheza ikiwa na pointi 19.
Licha ya uwepo wa washambuliaji nyota akiwamo, mfungaji bora wa muda wote wa Ligi Kuu Bara, John Bocco, imeshindwa kuonyesha makali yake na hata usajili uliofanyika imemuongeza kiungo mkabaji, Ally Msengi aliyetokea Tanzania Prisons.
Urejeo wa mshambuliaji, Charles Ilanfya aliyeumia goti tangu Agosti 28, mwaka jana katika mchezo dhidi ya Azam kwenye Uwanja wa Meja Isamuhyo Mbweni, huenda ukaongeza makali ya kikosi hicho mzunguko huu wa pili.
DODOMA JIJI
Kikosi hiki cha kocha, Mecky Maxime kimekuwa na changamoto maeneo yote mawili ya ulinzi na ushambuliaji, kikifunga mabao 16 na kuruhusu 21, japo ongezeko la mabeki, Mukrim Issa ‘Miranda’ na Abdi Banda umeongeza matumaini makubwa kikosini.
‘Miranda’ aliyeichezea Coastal Union kwa mkopo akitokea Singida Black Stars, atashirikiana vyema na Banda mwenye uzoefu baada ya kuzichezea Simba, Coastal Union, Mtibwa Sugar na Baroka FC, Chippa United FC na Richards Bay FC za Afrika ya Kusini.
KMC FC
Vijana hawa wa Kinondoni, wamekuwa na changamoto kubwa katika eneo la ushambuliaji baada ya kufunga mabao 11, tu katika michezo 16 waliyocheza, ingawa ongezeko la mzoefu, Shaaban Idd Chilunda huenda ukafufua upya matumaini kwao.
Nyota mwingine wa kuangaliwa ni Ahmed Bakari Pipino aliyetokea kituo cha Akademia cha Magnet na kung’ara na kikosi cha taifa ya vijana chini ya miaka 20 (U-20) ‘Ngorongoro Heroes’, kilichotwaa ubingwa wa CECAFA na kufuzu fainali za AFCON (U-20).
COASTAL UNION
Matumaini makubwa ya timu hii ni kwenye eneo la ushambuliaji, baada ya kumuongeza aliyekuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Togo msimu uliopita, Amara Bagayoko aliyejiunga na kikosi hicho katika dirisha dogo akitokea klabu ya ASKO de Kara.
Msimu uliopita, Amara alifunga mabao 19 na kikosi hicho na kuwavutia mabosi wa Coastal Union waliomuhitaji ili kuongeza ushindani katika nafasi hiyo, kwa kushirikiana na Maabad Maulid ambaye hadi sasa amefunga mabao manne ya Ligi Kuu Bara.
NAMUNGO FC
Timu hii imekuwa haina uwiano mzuri wa safu ya ulinzi na ushambuliaji ingawa katika dirisha dogo imefanya maboresho ya kuongeza nguvu, huku viongozi wa kikosi hicho kinachonolewa na kocha, Juma Mgunda kikizingatia maeneo hayo yote mawili.
Namungo imefunga mabao 11 na kuruhusu 19, ila ongezeko la Joshua Ibrahim aliyefunga mabao manne wakati akiwa na KenGold, na mabeki, Daniel Amoah aliyewika na Azam FC, Derrick Mukombozi na Anderson Solomon huenda yakatibu changamoto hiyo.
TZ PRISONS
Kikosi hiki cha maafande hakina uwiano mzuri wa kufunga na kuzuia baada ya kupachika mabao saba tu katika michezo 16 na kuruhusu 17, kimeongeza nguvu kwa washambuliaji, Adam Adam (Azam FC) na Yusuph Athuman aliyewahi kucheza Yanga.
Kwenye eneo la beki wa kati imemuongeza, Athuman Sufian Mwemfua aliyetokea Junguni FC ya visiwani Zanzibar, huku viungo wakiongozwa na Amade Momade aliyetokea kikosi cha ‘Wauaji wa Kusini’ Namungo FC na Gustapha Saimon kutokea Dodoma Jiji.
PAMBA JIJI FC
Pamba iliyorejea Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya miaka 23, tangu iliposhuka mwaka 2001, imeongeza nyota kadhaa wenye majina makubwa kikosini wakiongozwa na Deus Kaseke aliyewahi kutamba na Yanga na Habib Kyombo aliyeichezea Simba.
Moja ya changamoto kubwa ni eneo la ushambuliaji ambapo hadi sasa imefunga mabao saba tu katika michezo yake 16, iliyocheza, ingawa kitendo cha kuwaongeza nyota hao wazoefu ni ishara tosha imejipanga ili kuepuka kurudi ilikotokea.
Washambuliaji wengine ni Abdoulaye Yonta Camara aliyetokea Singida Black Stars na Mkenya Mathew Tegisi Momanyi (Shabana FC), beki Cherif Ibrahim (Coton Sport FC), viungo, Shassiri Nahimana (Bandari FC) na Abalkassim Suleiman kutoka Fountain Gate.
KAGERA SUGAR
Kikosi hiki kinachonolewa na Mmarekani Melis Medo kiko katika nafasi ya pili kutoka mkiani kikiwa na pointi 11 tu, ambacho pia kimekuwa na changamoto kubwa katika maeneo yote mawili kwa maana ya uzuiaji na ushambuliaji tangu mwanzo wa msimu.
Eneo la ushambuliaji limebeba matumaini kwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2021-2022, George Mpole aliyetokea Pamba, akiungana na Omary Buzungu (Mtibwa Sugar), Moubarack Amza (Namungo FC) na Saphan Siwa kutoka Tusker FC ya Kenya.
KENGOLD
Wageni hawa wa Ligi Kuu Bara ni kama walikuwa hawajui ushindani uliopo baada ya kuanza msimu huu na kikosi ambacho tangu mwanzoni mashabiki wengi walikitilia shaka, na kwa hakika wameonja ladha na kujishtukia mapema na kuingia sokoni.
Kengold iliyopanda Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza, inaburuza mkiani na pointi sita tu katika michezo 16, iliyocheza na kutishia kurudi ilipotoka, japo viongozi wao wamefanya usajili bora unaosubiriwa kuona utaisaidia vipi mzunguko wa pili.
Kikosi hicho chenye kocha mpya raia wa Serbia, Vladislav Heric, kimesajili wachezaji 24 wapya wakiwamo waliowahi kutamba na miamba wa soka hapa nchini Yanga na Simba wakiongozwa na Bernard Morrison, Obrey Chirwa, Kelvin Yondani na Zawadi Mauya.
KAULI ZA MAKOCHA
Kocha wa Fountain Gate, Roberto Matano anasema licha ya muda mchache tu aliokaa na wachezaji ila amefurahishwa na jinsi wanavyofuata vyema falsafa zake, huku Kally Ongala wa KMC akiweka wazi wamejipanga na ushindani wa mzunguko huu wa pili.
Kwa upande wa kocha wa Tanzania Prisons, Amani Josiah ameweka wazi ushirikiano ndio siri ya wao kufikia mafanikio.
Kocha wa Mashujaa, Abdallah Mohamed ‘Baresi’, amesema usajili walioufanya umezingatia matakwa ya benchi lao la ufundi, huku kocha wa KenGold, Vladislav Heric amesema licha ya presha kubwa iliyopo na muda mchache aliojiunga na timu hiyo ila ataendelea kukisuka vyema kikosi hicho, huku akiamini usajili uliofanyika dirisha dogo utaleta matokeo chanya kikosini.
“Tuna kazi kubwa ya kufanya na kuangalia ni kwa jinsi gani naitoa timu sehemu moja kwenda nyingine, jambo nzuri na la kuvutia nimeingia kipindi ambacho ligi imesimama, hivyo imenipa nafasi ya kuangalia upungufu uliopo kikosini kwetu.”