Prime
Nondo za Kiemba; Klabu zetu CAF kuna hili pia
MZUNGUKO wa tano kwenye michuano ya klabu barani Afrika unaendelea mwishoni mwa juma hili, huku wawakilishi wetu wakiingia uwanjani wakiwa katika hali ngumu kuelekea hatua ya mtoano. Wawakilishi wetu kwenye michuano ya klabu bingwa wana hadithi tofauti.
Kundi D – Simba SC
Simba, kama mwakilishi imara kwenye michuano ya CAF, ameumaliza mwendo wake mapema ikiwa imesalia michezo miwili. Hata ikitokea akashinda mechi zake zote zilizosalia, atafikisha alama saba pekee, ambazo ni chache ukilinganisha na kinara wa kundi Stade Malien mwenye alama nane.
Esperance de Tunis wana uwezekano wa kufikisha alama saba pia, na endapo watapata angalau alama moja kwenye michezo yao miwili, watanufaika na kanuni ya matokeo ya mikutano ya ana kwa ana.
Petro wao wanahitaji ushindi mmoja tu ili kuvuka alama ambazo Simba anategemea kuzifikia.
Hivyo, kwenye kundi hili, vita ya kuwania nafasi mbili za juu imebaki kwa Stade Malien, Esperance na Petro, huku Simba akikamilisha ratiba.
Kundi B – Yanga SC
Upande wa Yanga, hadithi yake bado inabeba matumaini yanayozitegemea mechi zake yenyewe.
Hadi sasa kinara wa kundi ni Al Ahly mwenye alama nane, huku Yanga na AS FAR Rabat wakiwa na alama tano kila mmoja. Yanga anakaa nafasi ya pili kwa faida ya ushindi walioupata kwenye mchezo uliowakutanisha Amani Zanzibar, waliposhinda kwa bao 1-0.
Endapo Yanga watapoteza mchezo wa ugenini dhidi ya AS FAR Rabat kwa tofauti ya mabao mawili, hadithi yao itaishia hapo, na mchezo wa mwisho dhidi ya Kabylie mwenye alama mbili utakuwa wa kukamilisha ratiba.
Matumaini ya Yanga ni kwamba hesabu zao hazihitaji kuangalia matokeo ya wengine; wao wenyewe wameshikilia hatma ya safari yao.
Katika mechi mbili wanahitaji alama nne ili kufuzu bila kutumia kikokotozi.
Hata hivyo, hali bado ni tete kwa bendera ya taifa kuendelea kupepea hadi hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kundi B – Azam FC (Kombe la Shirikisho)
Kwa upande wa Azam, mwenye alama sita katika nafasi ya tatu nyuma ya Wydad na Maniema Union wenye alama tisa kila mmoja, nafasi yao ni ngumu mno kiuhalisia. Kinachosubiriwa ni yale maajabu ya mpira wa miguu ambayo mara nyingine huwainua waliokatiwa tamaa.
Mchezo unaofuata dhidi ya Maniema Union kule visiwani Zanzibar ndio unaobeba matumaini ya kuelekea mechi ya mwisho nchini Morocco dhidi ya Wydad.
Wydad, kwenye mechi yao inayofuata, watacheza Nairobi dhidi ya Nairobi United wenye alama sifuri, huku mechi ya mwisho Maniema wakimaliza nyumbani kwa kumkaribisha Nairobi United.
Ili Azam apite bila kutumia msaada wa calculator, wanahitaji alama sita; alama nne zitawalazimu kutegemea matokeo ya timu nyingine.
Kama tungetumia karatasi tu bila kusubiri michezo ichezwe uwanjani, kauli nyepesi ingekuwa Azam ameumaliza mwendo, lakini mpira wa miguu unaweza kutuletea hadithi nyingine tamu.
Hivyo, tubaki kusema Azam wana kibarua kigumu kama cha ngamia kupenya kwenye tundu la sindano.
Kundi C – Singida (Kombe la Shirikisho)
Wawakilishi wengine ni Singida, waliopo kwenye kundi C wakiwa na alama 4, sawa na Stellenbosch anayeburuza mkia. Vinara wa kundi ni CR Belouizdad wenye alama tisa, huku nafasi ya pili ikikaliwa na AS Otoho wenye alama sita.
Ili kuyaweka hai matumaini ya kuendelea na michuano, Singida inapaswa kushinda mchezo wa nyumbani dhidi ya CR Belouizdad utakaochezwa Amani Complex Zanzibar, kisha mchezo wa mwisho itakaomalizia ugenini nchini Afrika Kusini dhidi ya Stellenbosch.
Ukitumia macho ya kawaida, huoni wapi Singida anaweza kupenya kuelekea robo fainali; ila kwa kutumia microscope na calculator, unaweza kuiona njia.
Hivyo, kuna uwezekano tusishuhudie bendera ya nchi ikipepea kwenye michuano ya klabu barani Afrika baada ya kumalizika kwa hatua ya makundi.
Taifa linapita njia ngumu mno kuelekea robo fainali. Yanga ndiye pekee ambaye hatma yake iko mikononi mwake, huku Azam na Singida wakitegemea matokeo ya timu nyingine. Hivyo, wakati tunashika calculator, tusisahau dua za kuziombea timu zetu.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu zibariki klabu zetu.