Prime
PUMZI YA MOTO: Haaland alikiona cha moto Emirates
Muktasari:
- Gabriel akamvuta bukta Halaand na kumtaka aende akamtafutie kiatu chake kilichovuka, yaani kama kaka mkubwa anavyomtuma mdogo wake.
SEPTEMBA 22, 2024, kwenye Uwanja wa Etihad, Manchester City iliikaribisha Arsenal, mchezo unaokumbukwa kutokana na kuumia kwa mshindi wa Ballon d'Or, Rodri, pamoja na matukio mengi ya kijivuni kutoka kwa Erling Haaland kwa Washika Bunduki hao.
Sekunde chache kabla ya mapumziko, Arsenał ikiongoza mabao 2-1, winga wao Leandro Trossard alionyeshwa kadi nyekundu, hivyo, kipindi cha pili Arsenal wakaamua tu kupaki basi...wakahimili mafuriko ya mashambulizi ya City hadi sekunde ya mwisho, ndipo John Stones wa City akasawazisha.
Katika kushangilia bao hilo, Haaland akaenda kuuchukua mpira wavuni na kumpiga nao kichwani beki wa Arsenal, Gabriel.
Baada ya filimbi ya mwisho kupulizwa, Haaland akafanya matukio mengine mawili yaliyojaa kibri na dharau.
Kwanza alimfuata kocha wa Arsenal, Mikel Arteta na kumwambia 'STAY HUMBLE' yaani 'kuwa mpole'.
Halafu akakwaruzana na dogo janja mmoja wa Arsenal, Lewis-Skelly, aliyeingia mwishoni kabisa na kupewa kadi ya njano kwa madhambi yake kwa Haaland. Akamfuata na kumuuliza, 'KWANI WEWE NAYE NI NANI?'
Haya mambo matatu yaliwakaa rohoni mashabiki wa Arsenal na hata City ilipoanza kuharibikiwa mwenye ligi, wakasema ni laana ya Haaland.
Siku 133 baadaye, Haaland na City yake wakaenda Emirates kukutana na Arsenal ya Arteta, Gabriel na Lewis-Skelly, na hakika washika bunduki walidhamiria kumfunza adabu nyota huyo wa Norway kwa ufedhuli wake aliowaonesha Septemba 22.
GABRIEL
Kitendo cha Haaland kuuchukua mpira na kumpiga nao Gabriel kichwani wakati akishangilia bao la kusawazisha Septemba 22, kilipata majibu Februari 2.
Majibu haya yalitoka kwa Gabriel mwenyewe, dakika ya 82 ubao ukisoma Arsenal 4-1 Manchester City, alianguka na kiatu kimoja kikavuka mguuni kwake.
Akamvuta bukta Halaand na kumtaka aende akamtafutie kiatu chake, yaani kama kaka mkubwa anavyomtuma mdogo wake.
Hii yote ilikuwa kulipa kile kisasi cha kumpiga na mpira kichwani.
Hata hivyo, Gabriel hakufanya hilo tu, muda wote wa mchezo alikuwa akimkera Haaland kwa kurudia yale maneno aliyomwambia kocha wake, 'STAY HUMBLE'.
Kila wakati alipokuwa akimdhibiti, alimpitia karibu na kumnong’oneza 'KUWA MPOLE'.
LEWIS-SKELLY
Bwana mdogo huyu ambaye wakati ule wanakutana Etihad alikuwa na miaka 17, naye alihakikisha analipa kisasi kwa Haaland.
Dakika ya 62 aliifungia Arsenal bao la tatu na bila kupoteza muda akashangilia bao hili kwa ushangiliaji wa Haaland wa kukaa kama mtu anayefanya 'meditation' au yoga.
Haya yalikuwa majibu yake kwa Haaland aliyejifanya hamfahamu wakati ule. Kwa hiyo alifanya hivyo ili Haaland amfahamu na uwanja ukaitika, 'Haaland now you him…', Haaland sasa unamtambua.
Ama kwa hakika Haaland atakuwa anamfahamu bwana mdogo.
ARTETA
Zaidi ya kwamba Gabriel alimkumbusha Haaland kauli ya kwa Arteta kila wakati, lakini kwa Arsenal kama klabu haikuishia hapo.
Mpira ulipoisha, DJ wa uwanjani akapiga wimbo wa mwanamuziki wa Marekani, Kendrik Lammar wa 'STAY HUMBLE' na mashabiki uwanja mzima wakawa wanaimba huku wakilitaja jina la Haaland.
Hebu pata picha uwanja uliojaa mashabiki zaidi ya 60,000 wanaimba kumzomea mtu mmoja.
Ama kwa hakika Arsenal walipanga kulipa kisasi kwa Haaland zaidi ya kuifunga Manchester City.