RAMADHAN: Mwamuzi aliyetwaa tuzo ya Kabaddi kimataifa
Muktasari:
- Kabaddi ni mchezo wa kale wenye asili ya India uliotokana na mazoezi ya kivita na mbinu za kujihami ukikadiriwa kuwepo kwa zaidi ya miaka 4,000.
INAWEZEKANA ulishawahi kusikia mchezo unaoitwa Kabaddi na unatamani kujua kwa undani namna unavyochezwa au unaona unavyochezwa lakini huelewi.
Kabaddi ni mchezo wa kale wenye asili ya India uliotokana na mazoezi ya kivita na mbinu za kujihami ukikadiriwa kuwepo kwa zaidi ya miaka 4,000.
Mchezo huo unaaminika kuchochewa na hadithi za kishujaa za Abhimanyu kutoka kwenye andiko la Mahabharata, ukiwa na lengo la kuimarisha nguvu, pumzi na uwezo wa kukabiliana na maadui wengi kwa wakati mmoja. Mwaka 2004, lilianzishwa Shirikisho la Kimataifa la Kabaddi (IKF) ili kusimamia mchezo huo ambao kwa sasa umeenea duniani kote.
UNAVYOCHEZWA, UKUSANYAJI POINTI
Kwa kawaida, mchezo huo unahusisha jumla ya wachezaji 14 wa timu moja, kati yao saba huanza na wengine husubiri nje. Katika kuchezwa kwake, kuna timu A na B hutumia dakika 40 zilizogawanywa katika vipindi viwili ambapo kila kimoja ni dakika 20.
Unatakiwa ufahamu kwamba ili kukusanya pointi, kuna kazi kubwa inafanyika.
Pointi kwenye mchezo huu zinapatikana baada ya mchezaji mmoja kutoka timu A kuwa mvamizi (rider) anayekwenda kufanya mashambulizi kwa wachezaji saba waliopo timu B ambao ni walinzi (defender).
Rider anapoingia kwenye zoni ya walinzi (defenders) anatakiwa atamke neno “Kabaddi” kwa sekunde 30 huku akipambana ili asikamatwe na wachezaji saba bila kuguswa.
Pointi za mchezo huo zinapatikana kwa mifumo miwili ikiwemo kuwagusa wachezaji (kuanzia mmoja na kuendelea). Baada ya kuwagusa defender, rider anatakiwa kuwahi mstari wa kati (middle line), hapo ndipo pointi zinapatikana.
Endapo mvamizi atawagusa wachezaji na kufanikiwa kudhibitiwa asifike kwenye mstari wa katikati, inahesabika hana pointi kwa sababu hajavuka kikwazo hicho.
Pia, mfumo mwingine wa upatikanaji wa pointi ni endapo mvamizi ataingia kwenye mstari wa hatari wa zoni B na kuwagusa bila ya wapinzani kumdhuru, hao walioguswa wanatakiwa kutoka nje ya uwanja na hapo atakuwa amepata alama ya ziada (bonus point).
Hivyo basi, mvamizi ili akamilishe kupata pointi kamili anapaswa kuwagusa walinzi wote na kuufikia mstari wa katikati, ndipo anapata pointi kamili, vinginevyo hapati.
Wakati mchezo huo ukiwa katika mikakati ya kukuzwa zaidi hapa nchini, Zanzibar kuna mwamuzi ambaye Novemba 2025 anabidhiwa tuzo ya kimataifa katika mashindano ya dunia yaliyofanyika Bangladesh.
Aliyekabidhiwa tuzo hiyo ni mwamuzi wa mchezo wa Kabaddi Zanzibar, Ramadhan Mrisho, ambaye anasema nyota yake imeng’ara zaidi baada ya kutwaa tuzo ya mwamuzi bora kwenye mashindano ya Kabaddi wanawake yaliyofanyika Bangladesh.
Anasema hiyo ilikuwa ni bahati kwake kwani wakati anaondoka Zanzibar kuelekea Bangladesh anasimama kama Mkuu wa Msafara wa kikosi hicho, lakini baada ya kufika mambo yakawa tofauti na alivyotarajia.
Anasema ilikuwa ngumu kwa hatua ya awali kwa sababu hiyo ni mara yake ya kwanza kuchezesha mashindano ya kimataifa, japo anabidi ajiamini ili kuitumia fursa hiyo vizuri.
Na kweli, anafanikiwa kutoka na tuzo hiyo yenye historia nzuri katika maisha yake yote tangu anapoanza kuutumikia mchezo huo.
“Tuzo hii ni hatua kubwa kwangu na najivunia kuwa sehemu ya baraza la waamuzi wa mashindano hayo makubwa duniani,” anasema.
Safari ya kufikia hadi kutwaa tuzo hiyo haikuwa rahisi kwake, ijapokuwa anatambua kwamba hakuna mafanikio yanayopatikana kirahisi, lazima upambane ili ufike panapohitajika.
Mwamuzi huyo anasema licha ya kutwaa tuzo hiyo, uzoefu wa mashindano ya aina hiyo ni miongoni mwa changamoto kubwa anazokutana nazo.
Anasema kwa mara ya kwanza kiongozi aliyekuwa anawasimamia hakumpanga, lakini kadiri mashindano yalivyokuwa yanaendelea ndipo anaanza kuwa miongoni mwa waamuzi na anabidi awajibike.
Changamoto nyingine, Ramadhan anasema hata lugha iliyokuwa inatumika ilimuwia vigumu wakati mwingine kwa sababu walitumia Kiingereza, ila chao ni tofauti na sehemu nyingine. Hivyo, mwamuzi huyo anasema anatumia muda mwingi kuwaelewa namna wanavyozungumza na mwisho wa siku mambo yanakuwa mazuri upande wake.
Pia, anasema mashindano hayo yalikuwa sehemu ya kuongeza ujuzi wake kwani zipo baadhi ya sheria za mchezo huo hakuwa anazielewa hapo awali, lakini baada ya kumaliza anapata vitu vipya. Anasema mashindano ya aina hiyo kwa kawaida yana presha kubwa katika kufanya maamuzi, hivyo anazingatia zaidi maagizo yaliyokuwa yanatolewa na kiongozi wao ili wasiharibu.
Anasema kiongozi huyo anatambua udhaifu wao ndiyo maana anatumia kila nafasi kuwakumbusha na kuwaweka katika mfumo sahihi kwani dunia ilikuwa inashuhudia.
TUKIO GUMU KWAKE
Mwamuzi Ramadhan anasema tukio gumu zaidi analokutana nalo katika mashindano hayo ni wakati timu yake inacheza kisha anakuwa sehemu ya waamuzi.
Anasema tukio hilo linamuua na kumgusa sana kwa sababu anapokuwa mwamuzi hawezi kuwa sehemu ya timu wala haruhusiwi kuzungumza chochote, hivyo anajikuta anaumia. Anafafanua kuwa kati ya siku 10 wanazokaa nchini Bangladesh, anatengewa na timu hiyo na anaiona wakiwa uwanjani kwa ajili ya mechi pekee.
MAANDALIZI KABLA YA MECHI
Ramadhan anasema kabla ya kuingia uwanjani kusimamia mechi anafanya mazoezi maalumu ya kujiandaa kimwili na kiakili.
Na maandalizi hayo anafanya zaidi kwa kuucheza mchezo huo kwani anaujua vizuri, na mashindano yake ya mwisho yalikuwa mwaka 2024 ya Kabaddi Championship yaliyofanyika nchini Kenya.
Ramadhan anasema yeye si mwamuzi pekee bali ni mkufunzi na aliwahi kucheza mchezo huo, hivyo anaujua kiundani.
Anasema alikuwa mchezaji wa kwanza Zanzibar kucheza mchezo huo, na baada ya kustaafu anaamua kuwa mkufunzi na sasa ni mwamuzi.
Ramadhan anaeleza kuwa kitu pekee kinachomvutia kuwa mwamuzi ni uamuzi wa wengi uliotokana na yeye kuwa mwanzilishi wa mchezo huo Zanzibar.
Anasema ili uweze kumchezesha mchezaji lazima mwamuzi aujue mchezo huo vizuri, vinginevyo itakuwa vigumu kutoa uamuzi sahihi.
Mwamuzi huyo anasema kitu kikubwa kinachomfanya achaguliwe kutwaa tuzo hiyo ni kuijua Kabaddi, jambo ambalo pia linampa heshima kubwa.
WANAWAKE KUPEWA KIPAUMBELE
Shirikisho la Kimataifa la Kabaddi (IKF) linatoa kipaumbele zaidi kwa wanawake kushiriki mashindano hayo, ndiyo maana hata mashindano ya dunia wanatangulia wao.
Hivyo, mwamuzi huyo anatoa wito kwa wanawake kisiwani Zanzibar kujitokeza kwa wingi kushiriki mchezo huo kwani umekuwa na muamko mkubwa duniani, hivyo wasikae nyuma.
Anasema viongozi wa mchezo huo kisiwani hapa wanajiandaa kuwaelimisha wanawake kuuchangamkia mchezo huo kwani kwa sasa Kabaddi imekuwa nyanja mpya ya fursa kwao.
WASOMEE UAMUZI
Mwamuzi huyo anasema ikitokea aniondoka Zanzibar hakutakuwa na mwamuzi mwingine kwani kwa sasa wapo watatu akiwemo yeye, hivyo anawaambia viongozi kusomea uamuzi wa Kabaddi.
Anasema siku nyingine ikitokea fursa ya aina hiyo, Zanzibar itakosa sifa ya kutoa mtu wa aina hiyo kwani wengi wanasomea ukocha na si uamuzi.
“Mara nyingi anawashawishi watu wasome uamuzi wa mchezo huu, tupo wachache sana wenye kiwango hicho, ni changamoto kubwa iliyopo pia,” anasema.
Akitolea mfano mashindano ya Mapinduzi Kabaddi Cup yaliyofanyika msimu huu, anakuwa mwamuzi pekee anayesimamia kuanzia mwanzo hadi fainali.
Anasema wengi wao hawana ujuzi wa kushika filimbi na kusimamia mchezo huo, hivyo wasiwe wanakimbia madarasa kwa sababu wanapishana na fursa nyingi.
Ramadhan anasisitiza wanawake pia kusomea uamuzi wa Kabaddi, kwani hakuna kisichowezekana na si wote wanaoweza kucheza.
Ni jambo la kupendeza zaidi yakitokea mashindano ya wanawake, wao ndio wachezeshe badala ya wanaume, jambo linalopendekezwa na Shirikisho la Kimataifa.
Anasema waamuzi wanawake ni wachache sana na waliopo bado wana woga na hawajiamini.
Zanzibar inapata nafasi ya kushiriki michuano ya dunia ya Kabaddi wanawake baada ya timu ya taifa ya wanawake Kabaddi Zanzibar kupata nafasi ya pili katika mashindano ya Afrika mara tatu mfululizo.
Licha ya kupata nafasi hiyo, iniachia hatua ya makundi ambapo sababu kubwa ya kufeli ni kukosa uzoefu wa mashindano hayo kwani ni mara yao ya kwanza kushiriki.
Zanzibar inashiriki Kombe la Dunia la Kabaddi kwa wanawake Novemba 2025 lililofanyika nchini Bangladesh, ambao ndio walikuwa wenyeji. Timu 11 zinashiriki mashindano hayo ikiwemo India, Thailand, Kenya, Uganda, Chinese Taipei, Germany, Nepal, Iran, Poland na Zanzibar.
Kati ya timu hizo, India initwaa ubingwa huo kwa mara ya pili mfululizo baada ya kuifunga Chinese Taipei katika mchezo wa fainali. Hivyo, anasema mchezo huo umeimarika sana ikilinganishwa na miaka ya nyuma na hamasa imekuwa kubwa.
Vilevile, Ramadhan anasema mchezo wa Kabaddi umekuwa kivutio kipya cha utalii kisiwani hapa kwani hata ukichezwa wageni huvutiwa nao.