Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ripoti maalumu… Madokta wa timu 7 Ligi Kuu matatani

Ripoti Pict

Muktasari:

  • Ibara ya 37 ya kanuni za usajili na utoaji leseni za klabu za shirikisho hilo inalazimisha kuwa na daktari anayetambulika na kuidhinishwa na mamlaka za afya za nchi, na kusajiliwa na chama/shirikisho la soka la nchi au ligi husika.

KANUNI za usajili na leseni za Klabu za Shirikisho la Soka Afrika (CAF), ni mojawapo kati ya miongozo muhimu ambayo ndani yake imetoa maelekezo ya kufuatwa ili kulinda usalama wa kiafya katika soka.

Ibara ya 37 ya kanuni za usajili na utoaji leseni za klabu za shirikisho hilo inalazimisha kuwa na daktari anayetambulika na kuidhinishwa na mamlaka za afya za nchi, na kusajiliwa na chama/shirikisho la soka la nchi au ligi husika.

Ibara hiyo inafafanua hivi; "Kila klabu inapaswa kuwa na daktari anayefanya kazi kwa kuajiriwa au kwa mkataba. Daktari huyu anapaswa kuwa na sifa zinazokubalika na kutambulika na mamlaka za afya za nchi husika. Daktari anayekubalika kwa kazi hii lazima awe ameidhinishwa na Baraza la Madaktari au chombo kingine cha kitaifa kinachohusiana na usimamizi wa madaktari.”

Sheria ya afya ya mwaka 2016 pia inatoa tafsiri kuhusu daktari, akifafanuliwa kama mtu aliyehitimu mafunzo ya kitabibu katika taasisi inayotambulika kwa ngazi ya shahada. Baraza la Madaktari Tanzania linakuwa chombo cha pekee cha kuthibitisha, kusajili na kusimamia madaktari hapa nchini.

RIP 01

“Daktari ni mtu ambaye amefanya mafunzo ya kitabibu katika chuo au taasisi yoyote inayotambulika, na ameidhinishwa na Baraza la Madaktari Tanzania kwa ngazi ya shahada au zaidi,” kinafafanua kipengele cha kwanza cha utafsiri wa sheria hiyo.

Kanuni ya 74 (1) ya Ligi Kuu msimu huu inalazimisha timu zinazoshiriki kuwa na daktari.

"Kila klabu ya Ligi Kuu inawajibika kuwa na daktari wa timu mwenye ujuzi na sifa za kutosha kama daktari kamili pamoja na mtaalamu wa tiba ya viungo watakaotambuliwa na kuthibitishwa na TFF walio na vifaa tiba kamili na stahiki," inafafanua ibara hiyo.

Kana kwamba haitoshi, kanuni 74 (4) inafafanua vigezo vya daktari wa Ligi Kuu.

"Madaktari wote Shiriki kwenye Ligi Kuu ni lazima wakidhi mahitaji ya Leseni ya Daktari inayotolewa na TFF na kupatiwa Leseni husika baada ya kutimiza pia Masharti maalum kutoka TASMA na kupata Uthibitisho wa TASMA," inasema ibara hiyo.

RIP 02

MADAKTARI 7 WA LIGI KUU MATATANI

Miongoni mwa mambo ambayo TFF imekuwa ikiyawekea mkazo mkubwa ni utekelezaji wa masharti ya kanuni za utoaji wa leseni za klabu za shirikisho hilo.

Kwa vile klabu ni wanachama wa TFF, ili zishiriki Ligi Kuu zinapaswa kufuata na kukubaliana na maelekezo ya TFF, CAF na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).

Hata hivyo, kati ya timu 16 zinazoshiriki Ligi Kuu Bara msimu huu, ni tisa tu ambazo madaktari wake wanatambulika na Baraza la Madaktari Tanzania (MCT) na majina yao yapo katika orodha rasmi ya baraza hilo.

Madaktari hao ni Moses Etutu (Yanga), Edwin Kagabo (Simba), Sima Shonde (Singida Black Stars), Mbaruku Milinga (Azam FC), Juma Kiswagala (Dodoma Jiji), Richard Yomba (Namungo FC), Mohamed Jumanne (JKT Tanzania) na Martine Valentine wa Tabora United.

Timu saba zilizobaki ambazo ni Fountain Gate, Pamba Jiji, Tanzania Prisons, KenGold, Kagera Sugar, Coastal Union na KMC zina wataalamu wa afya ambao majina yao hayapo katika orodha ya madaktari wanaotambuliwa na Baraza la Madaktari Tanzania.

RIP 03

SIKIA UTETEZI

Daktari wa Pamba Jiji FC, Dishoni Chacha alisema ameanza kufuatilia kupata leseni ambayo kwani ndio pekee ambayo hana na hakuna ugumu kuipata.

"Leseni ya baraza hilo wanatoa kule baraza. Mimi kwa taaluma ni daktari lakini wakati naingia kwenye tasnia ya michezo nilitakiwa kwenda kusoma Sports Medicine ili niwe daktari wa michezo kwa hiyo nilisoma advance certificate ya sports medicine. nilipomaliza nikapewa

cheti changu nikaondoka kwamba nimefanyaje, nimemaliza.

Na wakati tunafanya usajili wa kuingia Ligi Kuu, kule baraza wao waliomba vyeti vyangu kwa hiyo nikawapa vyeti vyangu nikidhani ndivyo wanavyovihitaji kumbe wao wanahitaji vya sports medicine kwa hiyo nikawapa vya sports medicine. lakini baadaye nikagundua kumbe kuna leseni inayotolewa na baraza ambalo mimi natakiwa niifuatilie ili niende nikafanye malipo kitu kama Shilingi 40,000 kwa hiyo hicho kitu ndio sijakifanya kwa hiyo kama kuna orodha ya madaktari na mimi simo, basi inawezekana ni kwa sababu sijalilipia hiyo leseni," alisema Chacha.

"Inawezekana huyo wa Fountain Gate akawa kama hilo la kwangu au naye hajalipia hiyo leseni," alisema Chacha.

Ofisa habari wa Coastal Union, Abbas Elsabr alisema kuwa daktari wao anakidhi vigezo. Sisi daktari wetu ana vigezo vyote vinavyohitajika na hatuna mashaka naye," alisema Elsabr.

Kaimu Mtendaji mkuu wa Tanzania Prisons, John Matei alisema kuwa  atalifuatilia suala hilo na kulitolea ufafanuzi.

"Hilo silijui ndio unaniambia hapa wewe, naomba nifuatilie kujua halafu nitakurudia kwa mrejesho," alisema Matei.

Katibu mkuu wa KenGold, Benson Mkocha alisema apewe muda wa kulifuatilia suala hilo.

RIP 04

"Hilo Baraza sijalielewa, hivyo kutoa ufafanuzi wowote labda nifuatilie nijiridhishe ndio naweza kusema chochote," alisema Mkocha.

Mtendaji mkuu wa KMC, Daniel Mwakasungula alisema kuwa madaktari wao wanashughulikia leseni.

"Madaktari wetu wamefuzu kutibia wachezaji na waliitwa na baraza kwa ajili ya mafunzo. Kwa hiyo kama hawapo kwenye orodha watakuwa wamesahaulika kwa sababu wamerudi siku si nyingi kutoka kwenye hiyo kozi amesema Mwakasungula.


SHIDA IPO HAPA

Mmoja wa viongozi wa TFF ameliambia Mwanaspoti sababu kubwa ambayo inafanya baadhi ya klabu kutoajiri madaktari wanaotambulika na Baraza la Madaktari ni kutomudu gharama za wataalamu hao na hivyo kujikuta zikilazimika kuwatumia wale wa ngazi za chini kielimu.

"Kwa utafiti ambao shirikisho limefanya, kuwa na madaktari hao sio jambo rahisi kwa sababu wengi ni waajiriwa wa hospitali za serikali au zile za binafsi na wanalipwa mishahara mikubwa na mizuri ambayo klabu zetu nyingi haziwezi kumudu kutokana na hali zao za kiuchumi.

"Kumbuka hao madaktari wanapaswa muda wote kuwa karibu na timu, hivyo hawawezi kufanya kazi mahali ambako wanalipwa kidogo wakaacha kule ambako wanapata mishahara mikubwa. Na wengine wana hadi hospitali na zahanati zao binafsi ni vigumu kumshawishi awe kwenye timu ingawa baadhi ya klabu huwapata kwa kuwakodi kwa muda kipindi ambacho ligi inachezwa," anasema kiongozi huyo.

Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), Karim Boimanda anasema bodi imeweka taratibu za kikanuni kuhusu suala la elimu na ubora wa watoa tiba kwenye klabu.

"Tuna kanuni ambazo zinasimamia suala la afya na matibabu kwenye klabu zetu na kuna Chama cha Madaktari wa Michezo (Tasma), ambacho kimekasimishwa mamlaka ya kusimamia viwango vya watu wa tiba kwenye klabu za soka nchini.

"Hivyo hadi sasa niseme hakuna tatizo kwa vile hakuna timu ambayo imeenda kinyume na kanuni na miongozo ya ligi na ya Tasma kuhusu wataalamu wa tiba na kama kutatokea changamoto, hatua zitachukuliwa kwa mujibu wa kanuni na taratibu zilizowekwa lakini kwa maana ya tatizo kwa sasa hakuna," anasema Boimanda.

Katibu wa Baraza la Madaktari Tanzania (MCT), David Paul anasema wataingilia kati ikiwa itatokea shida ya kitaaluma.

"Kwa sasa hakuna shida yoyote ya kitaaluma ambayo tumeipokea na TFF imeweka taratibu zake ambazo naamini klabu zinapaswa kuzifuata, hivyo hakuna tatizo. Lakini kama kutatokea shida ya kitaaluma kwa hao wataalamu wa tiba ambao wapo kwenye hizo timu, baraza litaingilia kati," anasema Paul.

Rais wa TFF, Wallace Karia anasema suala hilo na mengine yaliyo katika mwongozo wa usajili na utoaji leseni za klabu, yanafanyiwa kazi taratibu.

"Utekelezaji wa masharti ya 'club licensing' unafanyika kwa awamu kwa sababu kwa mazingira yetu ni vigumu vitu vyote vilivyomo mule kutekelezwa kwa wakati mmoja na ndio maana unaweza kuona kwa mfano tulianzia katika kulazimisha klabu kuwa na muundo mzuri wa kiutawala kisha tukaja katika timu za vijana na wanawake na tunaendelea.

"Kwa hiyo tunaendelea vizuri na tunaamini baada ya miaka kadhaa klabu zitatimiza kwa asilimia kubwa yanayohitajika katika muongozo huo," anasema Karia.

Katibu Mkuu wa Tasma, Juma Sufiani anasema wataalamu wote wa tiba katika klabu za Ligi Kuu Bara wapo kisheria na kikanuni.

"Tasma inayo hayo madaraja ya madaktari na tuliambiwa na TPLB kwamba daktari wa timu ya ligi kuu awe na sifa hizi. Idara ya tiba kwenye timu sio daktari pekee. Sisi tunachofanya ni kutoa 'advance certificate' (cheti cha juu) ya tiba michezoni.

"Tunaofanya kazi za michezo hatuna wasiwasi kwani tunafuata misingi ya serikali," anasema Sufiani.


Itaendelea...