Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ronaldo aongoza wakongwe Kombe la Dunia 2026

RONALDO Pict

Muktasari:

  • Mashindano hayo yatakayofanyika Marekani, Canada na Mexico yanatarajiwa kuwa makubwa zaidi kuwahi kufanyika huku kila taifa likiwa na matumaini ya kuandika historia mpya. 

TORONTO, CANADA: Kocha mkuu wa WAKATI dunia ikisubiri kuanza kwa Fainali za Kombe la Dunia 2026 zitakazoshirikisha timu 48 kwa mara ya kwanza katika historia, takwimu za vikosi vilivyotangaza majina ya mwisho zimeanza kuibua mjadala kuhusu uzoefu, umri, ubora wa ligi wanazotoka na klabu zinazotoa nyota wengi zaidi.

Mashindano hayo yatakayofanyika Marekani, Canada na Mexico yanatarajiwa kuwa makubwa zaidi kuwahi kufanyika huku kila taifa likiwa na matumaini ya kuandika historia mpya. Mbali na ushindani wa uwanjani, takwimu za vikosi zimeonyesha tofauti kubwa kati ya mataifa yanayowategemea vijana na yale yaliyoamua kuamini uzoefu wa wakongwe.

Klabu ya Manchester City imeibuka kuwa timu inayotoa wachezaji wengi zaidi katika Kombe la Dunia la mwaka huu. Jumla ya nyota 19 kutoka klabu hiyo watakuwa wakiwakilisha mataifa 12 tofauti, rekodi inayothibitisha ukubwa wa kikosi hicho katika soka la Ulaya na dunia kwa ujumla.

RONAL 01

Baada ya City, klabu ya Arsenal imechangia wachezaji 16 watakaocheza mashindano hayo wakiwa wanawakilisha mataifa 10 tofauti. Mabingwa wa ligi za England, Hispania, Ujerumani na Ufaransa pia wamechangia idadi kubwa ya nyota katika fainali hizo.

Licha ya kutwaa ubingwa wa Serie A nchini Italia, Inter Milan imechangia wachezaji saba pekee kutokana na kutokuwepo kwa Italia katika mashindano hayo. Hali hiyo imepunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya nyota wa klabu hiyo wanaoshiriki fainali hizo.

Katika Ligi Kuu England, klabu ya Crystal Palace imewashangaza wengi baada ya kutoa wachezaji 12 wanaokwenda Kombe la Dunia, idadi inayozizidi baadhi ya klabu kubwa barani Ulaya. Sunderland nayo imeonyesha mafanikio ya sera yake ya usajili baada ya kuwa na idadi sawa ya wachezaji wanaokwenda Kombe la Dunia kama Chelsea na Liverpool, kila moja ikiwa na wawakilishi 11.

RONAL 02
RONAL 02

Kwa upande wa ubora wa ligi wanazocheza wachezaji hao, Hispania ndiyo taifa pekee ambalo kikosi chake chote kinaundwa na wachezaji wanaocheza katika ligi tano bora za Ulaya, Ligi Kuu England, La Liga, Bundesliga, Serie A na Ligue 1.

England na Ujerumani zimetoa nafasi kwa baadhi ya nyota wanaocheza nje ya ligi hizo. Miongoni mwao ni mshambuliaji Ivan Toney anayekipiga Al-Ahli ya Saudi Arabia pamoja na Leroy Sane wa Galatasaray ya Uturuki. Ufaransa pia imejumuisha nyota wanaocheza Mashariki ya Kati akiwemo Theo Hernandez na N’Golo Kante.

Mataifa kama Uholanzi, Uswisi na Ubelgiji yanaendelea kunufaika na idadi kubwa ya wachezaji wanaocheza katika ligi za kiwango cha juu barani Ulaya. Nje ya bara hilo, Argentina na Senegal ndizo nchi zenye idadi kubwa zaidi ya nyota wanaocheza katika ligi tano bora za Ulaya.

RONAL 05

Kinyume chake, vikosi vya Curacao, Iran, Iraq na Qatar havina hata mchezaji mmoja aliyeshiriki moja kwa moja katika ligi tano bora za Ulaya msimu uliopita, jambo linaloonyesha tofauti ya viwango vya ushindani baina ya mataifa hayo na vigogo wa soka duniani.

Katika upande wa umri, Panama imeingia kwenye mashindano hayo ikiwa na kikosi kikongwe zaidi kati ya timu zote 48 zinazoshiriki Kombe la Dunia 2026. Wastani wa umri wa kikosi hicho ni miaka 30.4, kikifuatiwa na Colombia chenye wastani wa miaka 30.1. Mataifa hayo mawili ndiyo pekee yenye wastani wa umri unaozidi miaka 30 katika fainali za mwaka huu, jambo linaloonyesha imani kubwa waliyoiweka kwa wachezaji wenye uzoefu mkubwa wa kimataifa.

Brazil, chini ya kocha mpya Carlo Ancelotti, imeamua kutegemea uzoefu wa nyota wake wakongwe akiwemo Danilo, Casemiro na Neymar ambao wote wana miaka 34. Scotland nayo imewasili na kikosi chenye uzoefu mkubwa katika Kombe lao la Dunia la kwanza tangu mwaka 1998.

RONAL 04

Mlinzi wa lango wa Scotland, Craig Gordon, ndiye mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi katika mashindano hayo. Atakuwa na miaka 43 na siku 162 wakati michuano inaanza rasmi, rekodi inayomfanya kuwa mkongwe zaidi kuliko wachezaji wote watakaoshiriki.

Hata hivyo macho mengi yataendelea kuelekezwa kwa nahodha wa Ureno, Cristiano Ronaldo. Nyota huyo mwenye miaka 41 anaendelea kuvunja rekodi na kuonyesha uimara wa kipekee huku akijiandaa kushiriki Kombe la Dunia kwa mara ya sita katika maisha yake ya soka. Ronaldo ataungana na Luka Modric wa Croatia pamoja na Edin Dzeko wa Bosnia ambao pia wamevuka umri wa miaka 40.

Kwa upande wa vijana, Ivory Coast ni moja ya mataifa yenye vikosi changa zaidi katika Kombe la Dunia 2026 ikiwa na wastani wa umri wa miaka 25.8. Ni taifa la pili kwa kuwa na kikosi chenye umri mdogo zaidi baada ya Ecuador (miaka 25.7), jambo linaloonyesha imani kubwa waliyoiweka kwa kizazi kipya cha wachezaji wenye vipaji.

Miongoni mwa vijana wanaotarajiwa kung’ara ni Yan Diomande mwenye miaka 19 na Bazoumana Toure mwenye miaka 20 ambao tayari wameanza kuvutia vigogo mbalimbali wa Ulaya kutokana na vipaji vyao.

RONAL 02 (1)

Mabingwa wa Afrika, Morocco, pamoja na mabingwa wa Euro 2024, Hispania, pia wamewasili na vikosi vya vijana. Hispania hasa inaendelea kufaidika na kizazi kipya kinachoongozwa na Lamine Yamal mwenye miaka 18 pamoja na beki Pau Cubarsi mwenye miaka 19.

Katika orodha ya wachezaji wachanga zaidi, kiungo wa Mexico, Gilberto Mora, ndiye anayeshikilia nafasi ya kwanza. Atakuwa na miaka 17 na siku 240 pekee wakati mashindano yanaanza, huku akitarajiwa kutimiza miaka 18 mwezi Oktoba mwaka huu.

Mchezaji mwingine anayefuatiliwa kwa karibu ni kiungo wa Czech, Hugo Sochurek mwenye miaka 17 ambaye hivi karibuni alipata mechi yake ya kwanza katika timu ya taifa. Pia kuna nyota wa Bayern Munich, Lennart Karl ambaye ameibuka kama moja ya vipaji vinavyopewa nafasi kubwa ya kung’ara katika mashindano hayo.

Kadiri siku za kuanza kwa Kombe la Dunia 2026 zinavyokaribia, takwimu hizi zinaonyesha wazi kuwa kutakuwa na mchanganyiko wa uzoefu na ujana, jambo linaloweza kufanya mashindano hayo kuwa miongoni mwa fainali zenye ushindani mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya soka duniani.