Simba, Yanga zinavyopigana vikumbo kwa mastaa JKU
Muktasari:
- Katibu wa JKU, Khatib Shadhil amezungumza mambo mbalimbali kuhusu maendeleo ya timu hiyo mchango wa wageni changamoto za usajili pamoja na malengo ya klabu hiyo katika mashindano mbalimbali.
KLABU ya JKU ni miongoni mwa timu zinazotambulika Zanzibar kwa kazi kubwa ya kukuza vipaji vya vijana na kuwapa nafasi ya kufika kwenye soka la ushindani. Kupitia mfumo wao wa academy na malezi ya wachezaji timu hiyo imekuwa chimbuko la mastaa wengi wanaocheza kwenye klabu kubwa za Tanzania Bara.
Katibu wa JKU, Khatib Shadhil amezungumza mambo mbalimbali kuhusu maendeleo ya timu hiyo mchango wa wageni changamoto za usajili pamoja na malengo ya klabu hiyo katika mashindano mbalimbali.
Lakini changamoto kubwa zinazowakumba hasa pale wachezaji wao wanapoanza kuhitajika na timu kubwa. Hali hiyo imekuwa ikijitokeza pia kwa JKU. Katibu wa klabu hiyo Khatib Shadhil anasema mara kadhaa wamejikuta katikati ya ushindani mkali wa usajili kati ya timu kubwa zinazogombania saini za wachezaji wao waliowalea.
HALI ILIVYO
Anazungumzia mwenendo wa timu kwa sasa na mabadiliko yaliyotokea ndani ya kikosi chao.
“Hali ya timu kwa sasa kuna mabadiliko makubwa imeimarika kuanzia kwenye kikosi mpaka kwa kocha ambaye sasa ni mpya Abubakar Mngazija ndiyo maana umeona hata aina ya uchezaji wa timu umebadilika.”
Anaeleza falsafa ya JKU ya kukuza vipaji na kutoa nafasi kwa wachezaji kwenda kucheza timu kubwa zaidi.
“Ni hatua ya mfano na ya kuigwa pale ambapo timu inazalisha mastaa wakubwa ambapo mpaka sasa imeuza wachezaji wengi lakini lengo letu ni kulea vijana kupata ajira ndiyo maana akihitajika mchezaji kwetu basi tunampeleka ila maslahi siyo kipaumbele chetu.”
FAIDA BADO
Anasema namna klabu hiyo ilivyoanza kuweka mfumo wa kunufaika na uhamisho wa wachezaji wao wanaokwenda timu nyingine.
“Hawa wote ambao wametoka wengine hawajulikani tumeweka vipengele vya kunufaika na biashara hiyo lakini huko nyuma hatukuwa na utaratibu kama huo tulikuwa na focus ya kulea vijana wapate njia ya kujipatia kipato.”
Anafafanua kuhusu mfumo wa academy na namna wanavyokuza vipaji vya vijana tangu wakiwa wadogo.
“JKU ina academy za kukuza vijana kuanzia miaka 15 hadi 20 ndiyo maana kila mwaka tunapandisha ili kuongeza nguvu kwenye timu ya wakubwa ila kwetu tunazingatia vingi ukiachilia mbali vipaji tu lazima kijana awe na nidhamu na moyo wa kujituma.”
ALAMA
Anazungumzia fahari ya klabu hiyo kuona wachezaji waliowalea wakifika kwenye timu kubwa.
“Tunajivunia wachezaji wengi kama Feisal Salum hata kama hakuna tunachokipata kama faida ila zipo alama nyingi kama Yacoub kipa wa Simba Shekhan ambaye yuko Yanga na wengine wengi ambao tuliwalea ili waje kusaidia timu yetu ya Taifa.”
MCHANGO WA WAGENI
Anaeleza namna usajili wa wachezaji wa kigeni ulivyoongeza ushindani ndani ya kikosi chao msimu huu.
“Timu nyingi za taasisi huwa haziruhusu kusajili wachezaji wa kigeni lakini kwetu imekuwa tofauti kidogo kwani msimu huu dirisha dogo tumeongeza nguvu kwa kuchukua wageni na inalipa kwa kweli.”
Anaongeza kwa kueleza idadi na mchango wao ndani ya timu.
“Kwa sasa tunawachezaji wa kigeni saba kutoka mataifa ya Afrika watano Nigeria mmoja Cameroon na mwingine Ghana. Hawa wote wanacheza kikosi cha kwanza na wameongeza kitu kikubwa sana tulikuwa mbali raundi ya kwanza ila sasa anayeongoza ana pointi 38 sisi 36 kutoka mechi 19,” anasema.
USAJILI MGUMU ZAIDI
Anasema changamoto wanazokutana nazo pale timu kubwa zinapohitaji wachezaji wao waliowalea.
“Kutokana na vipaji ambavyo tumevilea kwa hapa kwetu basi tumekuwa na desturi ya kuwa na wachezaji wengi wazuri ambao mwisho wao wanaishia kugombaniwa na timu za Bara na ni jambo jema.”
Akitoa mfano wa baadhi ya usajili uliowahi kuwa na ushindani mkubwa kati ya klabu kubwa za Tanzania anasema ni ule wa Feisal Salum.
“Waliowahi kutusumbua sana katika usajili wao ni Feisal alitakiwa Simba lakini alienda Yanga ingawa Singida ilikuwa imeshamalizana na sisi kabla yao, lakini unajua uhusiano wa hizi klabu mbili basi akaenda alikokwenda.”
Kuhusu tukio lingine lililohusisha ushindani wa usajili wa mchezaji wao anasema lilifanyika vizuri.
Anasema, “usajili wa pili ni wa Shekhan tayari tulishafanya mazungumzo na Simba tukawa tunasubiri wao waje kumchukua lakini ghafla Yanga ilivyosikia muda huo huo ikapiga simu na kutuma tiketi za ndege na mimi nilikuwapo kwenye hiyo safari basi Yanga wakamuwahi.”
Kisha anaafafanua pia kuhusu kipa Yacoub ambaye naye aliwahi kuhitajika na klabu mbalimbali.
“Watatu ni Yacoub golikipa Yanga ilikuwa inamtaka lakini tulikosana kimaslahi Simba wakawazidi nguvu lakini pia aliangalia na aliyekuwepo Djiggui Diarra lakini Simba alikuwa na Camara majeruhi,” anasisitiza.
ISHU YA JKU NA JKT
Anazungumzia mchakato uliomhusu kipa Yacoub Suleiman wakati akitoka kwenda kucheza kwenye timu ya JKT.
“Ishu ya Yacoub Suleiman kule JKT mkataba wao ulikuwa wa kisheria tu ila kimaslahi ilikuwa kwenda kucheza kwenye ile timu halafu akipata mahali penye manufaa zaidi. Kwa hiyo hata kutoka kwake haikuwa ngumu,” anasema.
Anagusia kwamba mazungumzo yalifanyika kwa pande zote mbili na baadaye mchezaji huyo akafanikiwa kupata nafasi kwenye klabu kubwa.
“Kwa hiyo yalifanyika mazungumzo kati ya viongozi wa pande zote mbili JKT na JKU. Hata yeye hakuwa na maslahi makubwa usajili wake hata milioni 15 haikufika lakini kwenda kwake Simba kumemfanya kuwa mchezaji wa kwanza kutuingizia pesa nyingi ya usajili kuelekea timu za Bara,” anasema.
KIMATAIFA BADO
Akizungumzia ushindani wa michuano ya kimataifa na ugumu wake kwa timu kutoka Zanzibar, anadai kuna mengi.
“Ni kweli hizi timu zinazoshiriki michuano hii zina ubora wake huwezi kulinganisha timu ya Zanzibar na baadhi ya za Bara ingawa zipo ambazo tunazizidi ila siyo zote kwa mfano mwaka jana tulipata ubingwa na kushiriki Klabu Bingwa halafu mnapangwa na Pyramids hapo kutoboa ni ngumu,” anasema.
Anaongeza kuhusu baadhi ya matokeo yaliyowahi kuwanyima nafasi ya kusonga mbele: “Yaani tunakuwa na bahati mbaya kama ulikuwa shuhuda msimu juzi tulipangwa na Singida Black Stars lakini tulishindwa kuendelea kwa utofauti wa bao moja pekee lakini hatujawahi kununuliwa na watu ili tulegeze kamba ya kuwapisha wengine kama watu wanavyosema tunarubuniwa.”
MALENGO
Anasema malengo ya klabu yao katika mashindano ya ndani.
“Malengo yetu tunataka tuchukue ubingwa wa ligi mpaka FA na nguvu hiyo tunayo hata ukimuuliza mdau yoyote hapa Zanzibar atakwambia timu gani itakayochukua ubingwa ukizingatia tuna ladha ya wageni na wazawa.”
Anazungumzia pia kuhusu mradi wa ujenzi wa uwanja wa mazoezi wa klabu hiyo, akisema lengo ni hata mechi zao wachezee katika uwanja huo.
Anasema: “Lakini pia tunajenga uwanja wetu wa mazoezi wa nyasi bandia na ukikidhi vigezo tutakuwa tunacheza mechi zetu za nyumbani na mwaka huu mwezi Desemba utakuwa umemalizika labda mambo mengine ya kumalizia majukwaa basi.”
WANAFELI HAPA
Anasema changamoto zinazowakumba baadhi ya wachezaji wa Zanzibar licha ya kuwa na vipaji vikubwa.
“Wachezaji wengi wa Zanzibar kweli vipaji wanavyo vikubwa tu ila unamkuta hayuko makini na mpira mwingine anafanya hivyo kwa sababu kwao maisha mazuri wengi wanaokomaa ni wale ambao maisha yao siyo mazuri,” anasema.
Anaongeza pia sababu inayowafanya baadhi yao kuvutiwa na timu za taasisi za kijeshi.
“Ila wengi wanasogelea hizi timu za jeshi kwa sababu wanajua kwamba wakiingia huku watapata ajira ya kudumu ila kwa sasa uwepo wa wageni umeongeza nguvu kubwa sana kwa hiyo hata wazawa wameamka sana na wanapambana ili kupata nafasi.”
SIO KWELI
Akizungumzia mjadala wa uwepo wa wachezaji wengi wa kigeni kwenye timu anasema kupaswa kuwepo kwa uwiano sahihi.
“Wachezaji wa kigeni wakiwa wengi sana pia ni tatizo lakini wakisajiliwa kwa kiasi wataweza kuisaidia timu kuongeza ushindani unaona kama timu ya Taifa unawaona hawako vizuri kwa sababu hakuna nafasi,” anasema.
Anaongeza kuwa mchezaji mzuri anaweza kupambana na kupata nafasi hata kama kuna ushindani mkubwa.
“Lakini mchezaji mwenyewe anatakiwa kuonyesha uwezo unaona mtu kama Yussuph Kagoma yeye anacheza mbele ya wageni Feisal pia safu ya ulinzi ya Yanga wote ni wazawa Clement Mzize hivyo juhudi tu,” anasema.