Prime
SIO ZENGWE: TFF, Bodi ya Ligi zijisafishe na tuhuma za marefa

Muktasari:
- Ni bahati mbaya sana kumalizika kwa mechi hiyo baina ya Simba na Mashujaa FC ya Kigoma kumeibuka baada ya mijadala ya uamuzi mbovu kusimama kwa muda mrefu kutokana na ushiriki wa wawakilishi hao katika Kombe la Shirikisho Afrika na mashindano ya Kombe la Muungano.
KWA bahati mbaya sana mechi nyingine ya Ligi Kuu Bara imemalizika kwa kurejesha mijadala mingine kuhusu kiwango cha marefa na tuhuma za upendeleo.
Ni bahati mbaya sana kumalizika kwa mechi hiyo baina ya Simba na Mashujaa FC ya Kigoma kumeibuka baada ya mijadala ya uamuzi mbovu kusimama kwa muda mrefu kutokana na ushiriki wa wawakilishi hao katika Kombe la Shirikisho Afrika na mashindano ya Kombe la Muungano.
Ni bahati mbaya sana uamuzi mbovu umehusu timu ileile ambayo ilijadiliwa sana kabla ya mapumziko ya msimu kiasi cha kusababisha watendaji kama Ali Kamwe, ambaye ni kiongozi wa Idara ya Habari ya klabu ya Yanga, kukumbana na adhabu ya faini ya Sh5 milioni kutokana na kutoa wito wa kutaka mamlaka zichunguze kinachojadiliwa kama kina ukweli ndani yake.
Pia ni bahati mbaya sana mjadala huo umekuja wakati ambao Mahakama ya Kimataifa ya Michezo (CAS), ndiyo kwanza imeirudisha rufaa ya klabu ya Yanga kupinga uahirishaji mechi bila ya kufuata kanuni baada ya Simba kutishia kutocheza mchezo dhidi yao Machi 8.

Mechi hiyo iliahirishwa kwa madai ya Simba kuzuiwa kufanya mazoezi mepesi na hivyo kuzidisha ile dhana kuna kitu kinaendelea, hata kama rufaa imerejeshwa kwa sababu vyombo vya ndani havikuwa vimetoa uamuzi wa kukatiwa rufaa.
Itakuwa bahati mbaya zaidi kama mamlaka za soka, hasa uongozi wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) na Shirikisho la Soka (TFF) zitaendelea na msimamo wa kutotoa matamko au kutoonyesha kuwajibika au kuchukizwa na hiki kinachoendelea.
Kwa kumbukumbu zangu, Kamati ya Waamuzi imewahi kuwajibika mara moja kutoa ufafanuzi kuhusu matukio tata ya mechi za Ligi Kuu. Na hii ilikuwa takriban misimu minne iliyopita wakati Mwamuzi Mbobevu, Leslie Liunda alipotoa ufafanuzi wa bao lililokosolewa kuwa lilikuwa la kuotea.
Ni bahati mbaya sana uamuzi huo pia ulihusu bao lililofungwa na Meddie Kagere wa Simba katika mechi dhidi ya Prisons wakati mshambuliaji huyo aliponufaika na nafasi ya kuotea baada ya mpira uliopigwa na mchezaji mwenzake kumgonga mguuni beki wa Prisons. Liunda alieleza beki huyo alidhamiria kuuokoa mpira huo, hivyo baada ya kuugusa akaua tukio la kuotea.

Ufafanuzi huo umepingana na uamuzi uliotolewa kukataa bao la Fiston Mayele wa Pyramids aliyefunga dhidi ya Orlando Pirates katika mechi ya kwanza ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Tukio hilo lililingana kabisa na la Mayele kwa kuwa beki wa Orlando aliruka juu kujaribu kuuzuia mpira, lakini akaugusa tu na mpira kumfikia Mayele aliyeukwamisha wavuni. Hata baada ya kuhakiki katika video, bao halikukubalika.
Ni bahati mbaya sana matukio ya mechi ya Ijumaa baina ya Simba na Mashujaa yanazalisha kumbukumbu nyingi za uamuzi mbovu ambao sasa unaonekana kukithiri fikra za kuhusishwa na kunufaika kwa klabu moja tu.
Inaonekana Kamati ya Waamuzi au TFF na TPLB wamewaachia wachambuzi ndio wawajibike kwa ‘makosa ya kibinadamu’ yanayoendelea kushamiri kwa kutoa ufafanuzi waamuzi wanakuwa sahihi. Hawa wanatumia picha za marudio za Azam TV kuhalalisha makosa ya waamuzi, lakini cha kusikitisha ni chombo hicho cha habari hakina kamera za kutosha kuweza kumhakikishia mtazamaji kulitokea madhambi. Pia hakitumii teknolojia yoyote iliyoidhinishwa ya kutoa taarifa zaidi za tukio zaidi ya yale marudio ya picha na kuzigandisha.

Nani anatakiwa awajibike katika makosa yanayolalamikiwa na kuibua mijadala kila baada ya mechi fulani? Atumwe tena Liunda kutoa ufafanuzi wa matukio tata kila baada ya raundi?
Wiki hii mchambuzi mmoja alisema haoni sababu ya wao kuendelea kuchambua mechi ambazo anaona dhahiri mshindi alishapangwa. Alisema kuendelea kuchambua mifumo na mbinu za makocha wakati kuna mshindi ameshapangwa ni kupoteza muda na rasilimali wanazotumia kujiandaa kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa mechi ili watazamaji waelewe mambo kirahisi na kwa mapana yake.
Kweli, wachambuzi wakiingia studio ni kujadili makosa ya kibinadamu ya waamuzi na si mchezo, hasa mbinu, mifumo na ustadi wa wachezaji.
Ndiyo maana mijadala yetu kuhusu mechi ya Ijumaa iliyopita ni finyu sana. Mingi imeegemea katika kuangalia uhalali wa refa kuongeza dakika 15 kwa sababu kuna jibu rahisi tu mwamuzi ni lazima afidie muda wowote uliopotezwa. Pia mijadala hiyo inaangalia uhalali wa penalti mbili zilizotolewa kwa Simba badala ya mwenendo wa mwamuzi kwa muda wote, kitu ambacho kilivuruga akili za wachezaji na kujikuta wakifanya makosa hayo.
Kibaya zaidi, uhalali wa wachambuzi unatokana na kutumia picha za marudio za Azam TV ambazo bado hazitoshelezi kumpa mtazamaji tukio halisi zaidi ya hisiahisia tu.

Mamlaka hazitakiwi kuridhika na ufafanuzi unaotolewa na wachambuzi ambao nao hawapati taarifa za kutosha za matukio ya uwanjani kutokana na uchache huo wa vitendea kazi kwa mtangazaji na kutokuwepo na teknolojia ya kuwezesha kupatikana uhakika wa matukio.
Ukitumia mfano wa kuongezwa dakika 15 za kipindi cha pili, takriban theluthi nzima za dakika 45, utaona kuna udhaifu mkubwa na pengine mkakati wa kuhifadhi muda ili uongezwe baadaye kuliko kuhimiza mchezo uendelee bila ya kusimamasimama.
Katika mechi ya Ligi ya Afrika Kusini baina ya Bloem Celtic, wachezaji wa Mamelodi Sundowns wanaonekana kupoteza muda wakati wa kupiga kona. Mmoja anachukua mpira anautenga na kujiandaa kuupiga, lakini anaghairi na kumuachia mwenzake. Refa hafurahishwi na tukio hilo anatoa kadi ya njano. Wa pili anafanya hivyohivyo na kumuachia wa tatu na refa anamuonyesha pia kadi ya njano. Lengo lake si tu kuwaadhibu wanaopoteza muda, bali pia kuhakikisha muda haupotezwi kizembe.
Kwa hiyo kuchambua uamuzi kwa kuangalia muda ulioongezwa pekee bila ya kuangalia refa alikuwa anachukua uamuzi gani kuhakikisha mchezo unaendelea kutiririka, hakuwezi kutoa picha pana ya makosa ya waamuzi. Kama kipindi cha pili pekee kilikuwa na dakika 15 zilizopotezwa kwa matukio ya kawaida, maana yake refa hakuulinda mchezo ipasavyo.
Kwa kawaida matukio yanayoweza kusababisha refa aongeze muda ni mabao na shangwe zake, mabadiliko ya wachezaji ambayo ni nadra kudumu kwa hata dakika mbili, majeraha na matibabu uwanjani kama yatahitajika, penati (kuanzia faulo inapofanyika hadi mpira unapopigwa) na kadi nyekundu (kuanzia rafu inapotokea hadi mchezaji anapotoka uwanjani).

Kulikuwa na kadi nyekundu moja na penalti moja kabla ya refa kuonyesha muda wa nyongeza, wakati mabadiliko yalikuwa machache (kiwango cha juu ni matatu yakihusu wachezaji watano).
Kwa hiyo uchambuzi ukizingatia hayo yote kutaonekana kasoro za wazi kwa mwamuzi na hiyo itasaidia afya ya mpira kwa kuwa itaonekana familia haiishii kuangalia tukio pekee, bali mazingira yake na kanuni zenyewe.
Kwa England, ambako wastani wa muda kwa mechi kuchezwa ni dakika 54 na sekunde 46 kwa mujibu wa takwimu za msimu wa mwaka 2022/23, muda wa majeruhi umeongezeka kutokana na matumizi ya Refa Msaidizi wa Video (V.A.R), kwa kuwa huhusisha mazungumzo na V.A.R kabla ya mwamuzi wa kati kwenda kuhakiki, pia kuangalia marudio ya picha kwa pande zote.
Kabla ya V.A.R, mechi ambayo iliweka rekodi ya kuongezewa dakika nyingi za majeruhi ni ya Kombe la Carabao kati ya Burton Albion na Bournamouth na kulikuwa na sababu. Umeme ulikatika kwa dakika 24 hadi kurudi na mechi ilipoendelea iliongezewa dakika 28, maana yake ni dakika nne tu za ziada ukiondoa zile za umeme kukatika.
Sisi hatuna V.A.R na mechi nyingi zinachezwa mchana. Refa alikuwa wapi hadi dakika 15 au theluthi nzima ya kipindi cha pili inapotea? Hata wakati wa mabadiliko, waamuzi wengine huwafuata wachezaji kuwahimiza waharakishe kutoka uwanjani. Yule refa wa mechi ya Mamelodi na Al Ahly alimuamuru nahodha apige penalti ili kuokoa muda usipotee, yote katika kuhakikisha mtiririko wa mechi unaendelea na si kutunza muda pekee.
Kama refa anawaachia wachezaji wafanye wanavyotaka eti kwa sababu ana haki ya kufidia muda wote uliopotea, mechi zinaweza kuwa zinaisha usiku au siku inayofuata.
Kwa hiyo, haiwezekani kwa miaka yote mitatu ambayo imekuwa na kasoro za uamuzi hadi kukejeliwa kuwa ni “makosa ya kibinadamu”, eti TFF na TPLB hazichukui au kutoa tamko lolote kuhusu kinachoendelea zaidi ya Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi kuwasimamisha na baadaye kuwarejesha waendelee na makosa yao yanayotia doa ligi.
Ukweli kwamba kuna mijadala inayohusu ubovu wa uamuzi hauwezi kuachwa uendelea kana kwamba hakuna anayeweza kuwajibika kwa jambo hilo muhimu katika isingi mikuu minne ya mchezo wa mpira wa miguu.
Ukweli kwamba makosa hayo ‘ya kibinadamu’ yanaendelea kunufaisha timu chache kama sio moja, hauwezi kuachwa ukaendelea kana kwamba hakuna chombo kinachotakiwa kiwajibike kwa umma na mchezo wenyewe.
Ni lazima sasa TFF na Bodi ya Ligi waonyeshe kuwajibika kwa uamuzi mbovu kwa kuwa zile adhabu za kufungiwa zimeshakuwa sugu kwa waamuzi na pengine haziwagusi baadhi wenye maelekezo. Ni lazima waonyeshe kuwajibika kwa tuhuma za uamuzi unaoegemea upande mmoja. Ni lazima waonyesha kuchukizwa na kinachoendelea na kutoa tamko la kunyoosha mambo ili waamuzi wetu waone mamlaka hazihusiki kushiriki katika tuhuma za njama hizo za kupanga bingwa na kuanza kuwajibika.
Kama TFF na TPLB hazitajitokeza kulaani vitendo hivi na kuonyesha kukerwa na chukua hatua zinazoonyesha kuwajibika, itachukuliwa kuwa zinahusika katika kile kinachodhaniwa ni kupanga bingwa mpya. Hii itakuwa na athari kubwa kwenye mpira wetu.
Tulishatoka huko kwenye tuhuma za bingwa kupangwa. Inakuwaje tunarudi kirahisi namna hii wakati ambao wawekezaji wameanza kumimina fedha kwenye mpira?
Tunahitaji kuusafisha mpira wetu dhidi ya tuhuma zozote zinazouchafua na viongozi ni lazima waonyeshe mikono yao ni misafi. Bingwa ni lazima apatikane kwa ubora wake uwanjani na si kwa mipango ya nje ya uwanja.