Timu njooni Kigoma mchukue vipaji RCL
Muktasari:
- Leo inapigwa mechi za nusu fainali na keshokutwa bingwa wa mashindano haya atapatikana pamoja na timu mbili ambazo zimefuzu katika daraja la First League ambalo zamani lilijulikana kama Ligi Daraja la pili.
HAPA Kigoma kumechangamka na mwakilishi wa Kijiwe yupo hapa akifuatilia hatua ya fainali ya Ligi ya Mabingwa ya Mikoa (RCL) ambayo kesho inafikia tamati.
Leo inapigwa mechi za nusu fainali na keshokutwa bingwa wa mashindano haya atapatikana pamoja na timu mbili ambazo zimefuzu katika daraja la First League ambalo zamani lilijulikana kama Ligi Daraja la pili.
Sasa kama mnavyofahamu, wachezaji ambao wanaruhusiwa kikanuni kucheza haya mashindano ya RCL ni wale ambao umri wao upo chini ya umri wa miaka 20.
Kwa muda ambao mwakilishi wa kijiwe yupo hapa mkoani Kigoma, amebaini wachezaji wengi sana wenye vipaji ambao kama wakiendelezwa vizuri watakuwa msaada mkubwa kwa soka la Tanzania katika siku za usoni.
Ni wachezaji ambao klabu zetu mbalimbali za Ligi Kuu Bara zinaweza kujiokotea na kuwaingiza katika vikosi vyao vya vijana au hata katika vile vya wakubwa na kuwakuza taratibu kwa vile wameonyesha kuwa na kitu kwa nafasi wanazocheza.
Kijiwe kilitegemea makocha au wasaka vipaji wa klabu za Ligi Kuu na hata zile za Championship wawepo hapa Kigoma ili wajionee wenyewe vipaji mbalimbali na vila ambavyo wataridhishwa navyo waweze kuvisajili.
Hata hivyo katika siku zote ambazo mashindano haya yanachezwa hapa Kigoma hadi leo hii yanapokaribia mwisho wake, hakujaonekana watu wa hizo timu kuja kuangaza macho yao kwa vipaji vinavyocheza hapa.
Tulitegemea kuwaona hapa kwa sababu hakuna gharama kubwa kumtuma mtu mmoja au wawili kuja kuweka kambi hapa Kigoma kwa muda wote ambao mashindano haya yanachezwa.
Zinapotuaminisha zinathamini program za maendeleo ya soka la vijana, zinapaswa kutoa kipaumbele mashindano kama RCL ambayo yatawapatia wachezaji wadogo wenye vipaji.