Vichapo vya Yanga vilivyotibua vibarua vya makocha Bara
Muktasari:
- Kwa misimu ya hivi karibuni, wapo makocha wa timu mbalimbali walioondolewa kwa makubaliano ya pande mbili, ingawa, Yanga imekuwa ni chanzo kikubwa kutokana na vichapo vikubwa ilivyovitoa, kama ambavyo Mwanaspoti linawaelezea kwa kina zaidi.
MZIMU wa makocha kuondoka katika timu mbalimbali za Ligi Kuu msimu huu iwe kwa kusitishiwa mikataba yao au kutimuliwa, imezidi kushika kasi kwa sasa kutokana na malengo iliyojiweka, jambo linaloashiria ushindani kukua siku baada ya siku.
Kwa misimu ya hivi karibuni, wapo makocha wa timu mbalimbali walioondolewa kwa makubaliano ya pande mbili, ingawa, Yanga imekuwa ni chanzo kikubwa kutokana na vichapo vikubwa ilivyovitoa, kama ambavyo Mwanaspoti linawaelezea kwa kina zaidi.
MECKY MAXIME
Aliyekuwa Kocha wa Mbeya City, Mecky Maxime, alikumbana na kadhia ya kusitishiwa mkataba wake kwa makubaliano ya pande mbili, ikiwa ni muda mfupi tangu timu hiyo ichapwe mabao 6-0, dhidi ya Yanga, katika mechi ya Ligi Kuu, Aprili 16, 2026.
Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, mabao ya Yanga yalifungwa na Prince Dube na Pacome Zouzoua, waliofunga mawili kila mmoja huku, Maxi Mpia Nzengeli na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, wakifunga pia moja moja.
Mbeya City ilitangaza rasmi kuachana na Maxime na wasaidizi wake Kocha Msaidizi, Nizar Khalfan na Kocha wa utimamu wa mwili, Francis Mkanula, baada ya kichapo hicho kikubwa kwa kikosi hicho katika Ligi Kuu Bara kwa msimu huu wa 2025-2026.
Kuondoka kwa Maxime, kumemfanya kudumu Mbeya City kwa siku 130, tangu alipoteuliwa, Desemba 7, 2025, ambapo aliiongoza timu hiyo katika mechi 10 za Ligi Kuu msimu wa 2025-2026, huku kati ya hizo alishinda mbili, sare tatu na kupoteza tano.
Katika mechi 10, kikosi hicho kilifunga mabao tisa na kuruhusu 20, japo, kiujumla hadi anaondoka ilicheza 19, ikishinda nne tu, sare tano na kupoteza 10, ikifunga mabao 16 na nyavu zake kutikiswa mara 30, akiiacha nafasi ya 13 na pointi 17.
Kocha huyo wa zamani wa Kagera Sugar, Dodoma Jiji na Singida Black Stars zamani Ihefu, alijiunga na timu hiyo, Desemba 7, 2025, akichukua nafasi ya mtangulizi wake, Malale Hamsini, aliyepewa mkono wa kwaheri kikosini, Novemba 30, 2025.
Novemba 30, 2025, Klabu ya Mbeya City ilitangaza rasmi kuachana na aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Malale Hamsini, ikiwa ni muda mfupi tangu ichapwe bao 1-0, dhidi ya Namungo, katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini, Mbeya.
Malale alijiunga na Mbeya City, Machi 31, 2025, akichukua nafasi ya Salum Mayanga aliyejiunga na Mashujaa japo ameachana nayo, ambapo kocha huyo wa zamani wa JKT Tanzania, kwa msimu wa 2025-2026, alikiongoza kikosi hicho katika mechi tisa.
Katika mechi hizo tisa ambazo Malale aliiongoza Mbeya City, ilishinda mbili tu, sare mbili na kuchapwa tano, ambapo kwa ujumla kikosi hicho kilifunga mabao saba na kuruhusu 10 huku, Malale akiiacha ikishika nafasi ya 10 na pointi zake nane.
MOHAMED MUYA
Mohamed Muya ni kocha mwingine aliyekumbana na kadhia ya kusitishiwa mkataba wake wakati akiwa na Fountain Gate ikiwa ni muda mfupi tu pia kwake, baada ya kikosi hicho kuchapwa mabao 5-0 dhidi ya Yanga katika Ligi Kuu, Desemba 29, 2024.
Mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, mabao ya Yanga yalifungwa na Pacome Zouzoua, aliyefunga mawili, Mudathir Yahya na Clement Mzize wakifunga moja moja kila mmoja wao, huku Jackson Shiga, akijifunga mwenyewe.
Kocha huyo aliyewahi pia kuifundisha Geita Gold, msimu huu alikuwa anaifundisha Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’ ya Tanga, ingawa, aliachana nayo Aprili 8, 2026, baada ya kudumu kwa siku 184, tangu alipotambulishwa kikosini, Oktoba 6, 2025.
Kwa siku 184, Muya aliiongoza Coastal katika mechi 15, za Ligi Kuu msimu wa 2025-2026, ambapo alishinda mbili, akitoka sare saba na kuchapwa sita, akiwa ni kocha wa tatu baada ya mtangulizi wake, Alli Mohammed Ameir na sasa, Fikiri Elias.
Oktoba 1, 2025, Coastal Union iliachana na aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Alli Mohammed Ameir, ikiwa ni siku chache tangu kikosi hicho kichapwe mabao 2-0, dhidi ya Dodoma Jiji, katika mechi ya Ligi Kuu, iliyopigwa, Septemba 27, 2025.
Alli alijiunga na Coastal Union, Agosti 16, 2025, akitokea KVZ FC ya visiwani Zanzibar, akiwa na uzoefu mkubwa pia wa kuzifundisha timu mbalimbali zikiwemo, kikosi cha Zanzibar Heroes akiwa kocha msaidizi na kocha mkuu wa vijana Zanzibar.
Msimu wa 2025-2026, Alli aliiongoza Coastal katika mechi tatu za Ligi Kuu, akishinda bao 1-0, dhidi ya Tanzania Prisons, Septemba 17, 2025, kisha kuchapwa 2-1 na JKT Tanzania Septemba 22, 2025 na 2-0, mbele ya Dodoma Jiji, Septemba 27, 2025.
Hata hivyo, Aprili 10, 2026, akateuliwa Fikiri Elias, aliyewahi kuifundisha timu hiyo, ambapo kabla ya hapo, kocha huyo alikuwa huru, baada ya kuachana na KenGold ya Mbeya, Septemba 17, 2024, ambayo msimu huu inacheza Ligi ya Championship.
ROBERTO OLIVEIRA ‘ROBERTINHO’
Roberto Oliveira ‘Robertinho’, ni miongoni mwa makocha wanaoingia katika historia pia ya kusitishiwa mkataba wake baada ya kichapo kutoka Yanga, ambapo kocha huyo wa zamani wa Simba aliondolewa Novemba 7, 2023, kufuatia kufungwa mabao 5-1.
Katika mechi hiyo ya Ligi Kuu iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Novemba 5, 2023, mabao ya Yanga yalifungwa na nyota wake, Kennedy Musonda, Stephane Aziz KI na Pacome Zouzoua, huku Maxi Mpia Nzengeli, akifunga mawili.
Kwa upande wa bao pekee la Simba katika mechi hiyo, lilifungwa na aliyekuwa nyota wa timu hiyo, Kibu Denis na baada ya hapo Novemba 7, 2023, Robertinho akasitishiwa mkataba wake na aliyekuwa kocha wa viungo, Mrwanda Corneille Hategekimana.
Robertinho, alijiunga na Simba Januari 3, 2023, akichukua nafasi ya Kocha, Juma Mgunda aliyekaimu wadhifa huo, baada ya kuondoka kwa Zoran Manojlovic Maki mwenye uraia pacha wa Serbia na Ureno, aliyeachana na kikosi hicho, Septemba 6, 2022.
Tangu Januari 3, 2023, Robertinho aliiongoza Simba katika mechi 17 za Ligi Kuu, bila ya kupoteza kuanzia msimu wa 2022-2023 na 2023-2024, ingawa, rekodi hiyo bora kwa kocha huyo Mbrazili, ilivunjwa na Yanga na safari yake kuishia pia hapo.
Ushindi huo wa Yanga wa mabao 5-1, uliifanya kuvunja rekodi ya Simba ya kutopoteza mechi ya Ligi Kuu Bara, tangu mara ya mwisho ilipochapwa na Azam FC bao 1-0, Oktoba 27, 2022, la mshambuliaji, Prince Dube anayecheza kwa sasa Yanga dakika ya 35.
Kabla ya Simba kuchapwa mabao 5-1, dhidi ya Yanga, ilikuwa imecheza jumla ya mechi 28 za Ligi Kuu Bara bila ya kupoteza, ambapo kati ya hizo ilishinda 23 na kutoka sare pia tano, rekodi iliyovunjwa kwa fedheha na watani zao, Novemba 5, 2023.
Mbali na hilo, ushindi huo wa Yanga ulivunja pia rekodi ya Robertinho ya kutopoteza mechi ya Ligi Kuu Bara, kwani tangu Januari 3, 2023, alipoteuliwa Simba, msimu wa 2022-2023 na 2023-2024, alishinda 15 na kutoka sare mbili tu kati ya 17.
Moja kati ya mafanikio aliyopata Robertinho akiwa na Simba, ni kutwaa taji la Kombe la Ngao ya Jamii, kwa kuifunga Yanga kwa penalti 3-1, baada ya suluhu ya (0-0), katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Agosti 13, 2023.
Kabla ya Robertinho kuchukua kikosi hicho, Mgunda alikiongoza katika mechi 16 za Ligi Kuu ambapo kati ya hizo alishinda 11, sare nne na kupoteza moja tu, huku akiiwezesha pia timu hiyo kufuzu hatua ya makundi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mgunda anayeifundisha kwa sasa Namungo FC, aliandika rekodi ya kipekee ya kuipeleka Simba hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa msimu wa 2022-2023, akiwa ni kocha wa kwanza mzawa katika mashindano hayo, tangu mwaka 1998.
Kocha wa kwanza mzawa kuipeleka timu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, alikuwa ni marehemu Tito Oswald Mwaluvanda mwaka 1998 akiwa Yanga, akishirikiana na aliyekuwa nahodha wa kikosi hicho wakati huo, Fredy Felix ‘Minziro’.
Mwaka 1997, Yanga iliachana na Kocha raia wa England, Steve McLennan na timu kubakia kwa msaidizi wake, Juma Pondamali hadi mwisho wa msimu, kisha msimu mpya wa 1998, ulipoanza, ndipo, Tito Oswald Mwaluvanda, akashika wadhifa huo kikosini.
Mwaluvanda alitangazwa na aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo, hayati Rashid Ngozoma Matunda na kuandika rekodi bora ya kuipeleka hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya kuifunga Coffee United ya Ethiopia jumla ya mabao 8-3. Tangu mwaka 1998, hakuna kocha yeyote mzawa aliyefikia hatua hiyo ya mashindano makubwa zaidi Barani Afrika, hadi Juma Mgunda anayekinoa kwa sasa kikosi cha Namungo ‘Wauaji wa Kusini’, kuandika rekodi mpya akiwa Simba, msimu wa 2022-2023.