Simba si mchezo Afrika

WAWAKILISHI wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika Simba watatupa karata yao ya kwanza ugenini dhidi ya Plateau United Nigeria na matokeo ambayo watayapata mara baada ya dakika tisini kumalizika ndio watatambua watakuwa na mlima mrefu kuishia hapo hapo au kusonga mbele.

Simba wanaingia katika mchezo huo wakiwa na kumbukumbu mbaya ya msimu uliopita kuanzia ugenini katika hatua ya awali dhidi ya UD Songo wakiwa Msumbuji pambano lao lilimalizika kwa suluhu wakiwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri katika uwanja wao wa nyumbani lakini mambo yalikuwa tofauti.

Katika mechi ya marudiano Simba walikubali kutoka sare ya bao 1-1 na UD Songo ambao walisonga mbele kutokana na sheria ya bao la ugenini jambo lililopelekea mashabiki wa Msimbazi kutoka uwanjani wakiwa na uzuni kubwa kutokana na awali waliamini watasonga mbele kama msimu mmoja nyuma.
Mwanaspoti lilitembelea na kuzungumza na benchi la ufundi ambao walieleza mipango yao na masuala mengine yote ya msingi ambayo yanaweza kuwa kama silaha ya msimu huu kufanya vizuri katika mashindano hayo makubwa kwenye ngazi ya klabu hapa Afrika.
MIKAKATI YAO
Kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck anasema msimu huu wameanza kuweka mikakati ya kimataifa kabla hata ya kutambua watacheza na timu gani kutoka katika nchi ipi.
Sven anasema ukiangalia kikosi cha Simba ambacho kiliondolewa katika hatua ya awali msimu uliopita ni tofauti kabisa alichokuwa nacho msimu huu, wamefanya usajili wa wachezaji wenye uwezo wa kushindana katika mashindano hayo makubwa.
“Wakati Simba wanaondolewa katika hatua ya awali msimu uliopita timu haikuwa chini yangu kwa maana hiyo msimu huu tulianza mikakati yetu ya kufika mbali kama kufanya usajili wa maana na kuwaandaa wachezaji katika misingi mizuri ili kufanya vizuri,” anasema.
“Mipango yetu ni kufika katika hatua ya makundi na baada ya hapo ndio tutaanza kuwa na malengo yale ya matamanio ambayo awali hatukuwa nayo na hilo linawezekana kutokana na viongozi, wachezaji na benchi la ufundi kila mmoja kutimiza majukumu yake,” anasema Sven.
POSHO
Uongozi wa Simba msimu huu wameweka mipango mikakati ya kuona timu yao inang’aa katika mashindano ya kimataifa na katika hatua ya awali wameweka Dola za Kimarekani 50,000 zaidi ya Sh100 milioni kwa pesa ya Kitanzania kama posho kwa wachezaji andapo watawatoa wapinzani wao katika michezo yote miwili.
Mmoja wa wachezaji wa Simba ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe, alisema wanapokuwa na mechi kubwa ikiwemo ya kimataifa viongozi mbalimbali huwa wanakwenda katika kambi yao na mara baada ya kuzungumzia masuala muhimu mwisho hutoa ahadi ya pesa kama motisha.
“Katika hatua hii ya awali utaratibu tayari umeshatengwa kama tutashinda au kupata matokeo mazuri na tukawatoa Plateau United tutapata Sh100 milioni ambayo itagawanyika kwa utaratibu wa wachezaji waliocheza kupata zaidi, waliokuwa benchi tofauti na wale ambao hawakucheza kabisa,” alisema.
“Hata msimu uliopita tuliwekea kiasi hiko cha Sh100 milioni kama tungefanikiwa kuwatoa UD Songo tulikuwa tunachukua lakini baada ya kushindwa kufanya hivyo tuliikosa pesa hiyio,” alisema mchezaji huyo.
Straika wa Simba, Meddie Kagere alisema motisha ya pesa ambayo wanaipata kutoka kwa Uongozi wao inaongeza morali kwa wachezaji kushindana katika mazoezi ili kupata nafasi ya kucheza na hivyo hivyo kuipigania timu kupata matokeo mazuri.
“Motisha hiyo ya pesa ambayo inatolewa ni nyingi ambayo inaweza kutusaidia kuendesha na kujikimu mahitaji yetu ya maisha ndio maana kila mchezaji ambaye hupata nafasi ya kucheza hupambana kadri ambavyo anaweza ili kuona tunafanikiwa katika hilo,” alisema Kagere.
UBORA NA MAPUNGUFU
Simba msimu huu wameonekana kuwa bora katika safu yao ya ushambuliaji ambayo ni nadra kumaliza dakika 90, kama ambavyo walivyofanya msimu huu katika ligi kwani ndio timu ambayo amefunga mabao mengi huku washambuliaji wake watatu, Kagere, Mugalu na Bocco wakiwa katika msimamo wa wafungaji.
Ubora mwingine ambao Simba wanao katika safu ya kiungo ya kiungo washambuliaji, Chama, Luis, Iajibu, Ndemla, Dilunga na Mzamiru wamekuwa na uwezo wa kutengeneza nafasi za kufunga na muda mwingine kufunga wenyewe.
Shida katika kikosi cha Simba ipo katika maeneo mawili kwanza mabeki wao wa kati Wawa na Onyango si wazuri katika kuruka mipira ya vichwa lakini mabeki wao wa pembeni Kapombe na Tshabalala ni wazuri katika kushambulia kuliko kukaba.
Shida nyingine ambayo imeonekana katika kikosi cha Simba ni katika safu yao ya kiungo mkabaji ambayo mara kwa mara wamekuwa wakicheza Mkude na Mzamiru ambo kuna mechi wanakuwa katika viwango bora lakini kuna nyingine wanazidiwa.
KIKOSI
Kikosi cha Simba kitaondoka hapa nchini Jumatano kuelekea Algeria wakiwa wachezaji 23, benchi la ufundi na baadhi ya viongozi.
Miongoni mwa majina ya nyota wa Simba ambao watasafiri ni, makipa Aishi Manula, Benno Kakolanya wengine Shomary Kapombe, Erasto Nyoni, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ Gadiel Michael, Pascal Wawa, Joash Onyango, Jonas Mkude.
Wachezaji wengine, Said Ndemla, Larry Bwalya, Clatous Chama, Meddie Kagere, John Bocco, Ibrahim Ame, Bernard Morrison, Luis Jose, Hassan Dilunga, Mzamiru Yassin, Ibrahim Ajibu na Kennedy Juma.
Wachezaji wengine watano waliokuwa katika kavu ambao wanaweza wasiwepo katika msafara huo ni, Ally Salim, Chriss Mugalu ambaye bado anasumbuliwa na nyonga Miraji Athumani na Charles Ilanfya.
Sven aliliambia Mwanaspoti kwa kuwa wanakwenda kucheza mchezo mmoja hawatalazimika kusafiri na wachezaji wote kuna kundi lingine litabaki hapa Tanzania.
“Ukisafiri na wachezaji wote mechi yenyewe ni moja ikatokea kuna ambao wanafanya vizuri katika mazoezi ukashindwa kuwapa nafasi ni kama wataumia ndio maana nitachukua kati yao wa kusafiri nao,” anasema Sven.
Kocha wa Biashara United, Francis Baraza aliwahi kuliambia Mwanaspoti mabeki wa kati wa Simba, Wawa na Onyango ni wazuri katika kuzuia mashambulizi ambayo hayana presha na kutumia akili nyingi.
“Mabeki hao wameonekana kuwa na shida katika mashambulizi yaliyokuwa na presha na hawana kasi ya kukimbizana na wachezaji wenye mbio kama ambao wataenda kukutana nao katika Ligi ya Mabingwa Afrika,” anasema Baraza.

By THOBIAS SEBASTIAN