Ahmad, Prisons ndo basi tena, Makatta kumrithi

Muktasari:

  • Makata aliyetoka kupandisha Pamba Jiji iliyodumu Championship kwa zaidi ya miaka 21, anarejea Prisons akiwa na kumbukumbu nzuri kwani msimu wa 2014/15 aliibuka Kocha Bora wa Ligi Kuu akiiweka timu hiyo nafasi ya nne.

WAKATI Tanzania Prisons ikithibitisha kocha Ahmad Ally, amevunja mkataba, muda wowote Maafande watamtangaza Mbwana Makata kuiongoza timu hiyo msimu ujao wa mashindano.

Ally aliyejiunga na Prisons kwa mkataba wa miaka miwili tangu Novemba 2023 akichukua nafasi ya Fred Felix 'Minziro' na aliikuta timu nafasi ya 14 kwa pointi 13 na kumaliza msimu nafasi ya tisa kwa alama 34.

Kocha huyo aliyewahi kupita timu kadhaa ikiwamo KMC iliyomtema kabla ya  kujiunga na Wajelajela hao, anatajwa kumalizana na JKT Tanzania inayodaiwa imeachana na Malale Hamsini.

Hata hivyo, licha ya kuingia na upepo mzuri, lakini kocha Ally hakumaliza vyema alipoongoza michezo 11 mfululizo za mwisho bila kushinda mechi yoyote akipoteza nne na sare saba.

Makata aliyetoka kupandisha Pamba Jiji Ligi Kuu anarejea tena kwa maafande hao akijivunia rekodi nzuri ikiwa ni kumaliza nafasi ya nne msimu wa 2014/15 na kuwa Kocha Bora wa msimu.

Ofisa Habari wa timu hiyo, Chacha Waisaka amesema wanamtakia kila la kheri kocha Ahmad na muda wowote watamtangaza mbadala wake kwani mazungumzo yanaendelea vyema kwa zaidi ya asilimia 95.

"Kocha Ally ameomba kuondoka kupata changamoto mpya, tumemkubalia na hatuwezi kumng'ang'ania na hatutakuwa naye, tupo katika mazungumzo mazuri na kocha mzawa ambaye atakuwa bora kwani anaifahamu timu," amesema na kuongeza;

"Ni makocha wawili tunaozungumza nao, lakini huyu mmoja tulishakuwa naye, hivyo tunamrudisha tena kwa kuwa anafahamu falsafa yetu na muda wowote tutamtangaza hadi kufikia Juni 20."

Ofisa huyo ambaye ni askari wa Jeshi la Magereza ameongeza kuwa, timu inatarajiwa kurejea kambini Julai 1, ambapo wiki ijayo wataanza kutangaza usajili mpya wa nani kaingia na yupi kutoka akieleza kuwa timu itabaki kuwa bora kwa ajili ya soka la ushindani.