AKILI ZA KIJIWENI: Ombea bahati ya Morrison utoboe

Muktasari:
- Kwa hapa kijiweni wote tunakubaliana kwamba Bernard Morrison ni mchezaji mzuri sana na anayeweza kuwa na mchango mkubwa kwa timu lakini pia inawezekana kwa sasa hapa nchini yeye ndiye anayeongoza kwa kuwa na bahati.
BAHATI ni kitu cha msingi sana hapa duniani na hasa unapokuwa na bahati kama ya mtu anayeitwa Bernard Morrison, winga wa mpira ambaye usajili wake kwa sasa unasoma ni mchezaji wa KenGold.
Kwa hapa kijiweni wote tunakubaliana kwamba Bernard Morrison ni mchezaji mzuri sana na anayeweza kuwa na mchango mkubwa kwa timu lakini pia inawezekana kwa sasa hapa nchini yeye ndiye anayeongoza kwa kuwa na bahati.
Nakukumbusha tu baadhi ya matukio kuhusu mchezaji huyo ambayo yametosha kututhibitishia hapa kijiweni kwamba fundi wa mpira Morrison ana bahati kubwa maishani ukiweka kando kipaji chake cha kusukuma kabumbu.
Aliwakera Yanga kwa kucheza mechi chache kisha akatimkia Simba na baadaye walipomuacha, Yanga ikamrudisha kwa mbwembwe huku ikisahau kejeli zote alizowafanyia wakiamini anaweza kuwa msaada mkubwa kwao.
Hata hivyo, walichokitegemea hakikutokea na baadaye wakamuacha. Ghafla tukaona jamaa amepata bingo la usajili katika timu ya FAR Rabat lakini huko mambo hayakumwendea vyema akapata majeraha yaliyomuweka nje ya uwanja kwa muda mrefu hadi alipoachana nayo.
Akarejea nchini kuja kujipanga na akajikuta amekosa timu katika dirisha kubwa la usajili na wakati huo akapata majeraha, lakini upepo wa bahati ukaendelea kumfuata nyumbani.
Katika dirisha dogo la usajili msimu huu KenGold wakamfuata na kufanya naye mazungumzo ya kumsajili huku akiwa bado hajapona na hayupo fiti ikiamini kwamba angekosa mechi chache za timu hiyo kisha kurudi uwanjani kuwabeba katika mechi nyingi za kumalizia msimu.
Hata hivyo, jamaa hadi sasa bado hajaonekana uwanjani huku mechi za Ligi Kuu zikibaki saba kwa timu yake na hakuonekani kama kuna dalili za kuichezea tena timu hiyo kwenye ligi.
Watu wenye bahati zao hao, wanakaa nyumbani wakiwa majeruhi, mkataba unawafuata wanapiga hela huku wakiwa hawajakanyaga uwanjani.