Al Hilal nao hawana dogo

Muktasari:
- Klabu ya Al Hilal ya Sudani nao hawana dogo katika kipindi cha mapumziko baada ya kuamua kwenda kuweka kambi nchini DR Congo ikiwa ni sehemu ya maandilizi ya kuivaa Yanga kwenye mchezo wa hatua ya kwanza ya mtoano wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
KLABU ya Al Hilal itamenyana na Hilal Al-Fasher katika mpambano wa Kombe la Sudan kisha Jumatano, itasafiri hadi nchini DR Congo kuweka kambi fupi ambapo watacheza michezo miwili ya kirafiki dhidi ya TP Mazembe ya nchini humo.
Viongozi wa Klabu hiyo wameamua kukubali kile kinachosemwa kuwa ni mapendekezo ya kocha mkuu wao Florient Ibenge ya kwenda kuweka kambi nchini DR Congo ikiwa ni sehemu ya maandalizi yao ya kuikabili Yanga katika mchezo wa hatua ya kwanza ya mtoano ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mabingwa hao wa Ligi Kuu ya nchini Sudani mara 29 na kombe la Sudani mara 7 wanatarajia kuivaa Yanga Oktoba 7 mwaka huu watakapo anzia ugenini kisha mchezo wa marudiano ukitarajiwa kwenda kupingwa Oktoba14 mwaka huu.
Hata hivyo ukiachana na kikosi hicho cha Ibenge kujiandaa kwenda kuweka kambi nchini Congo, mechi yao ya mwisho iliibuka na ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Monarte na kufanikiwa kutinga hatua ya nusu Fainali ya Sudan Cup 2022.