ALEX KAJUMULO: Kichwa kimoja, mipango kibao unaambiwa Awachana wachezaji wa Kibongo kweupeee

ALEX Kajumulo ni miongoni mwa majina maarufu nchini kwa jumla kutokana na mambo anayofanya kwenye soka, burudani na biashara.
Ni mmiliki wa wa kampuni ya Kajumulo inayojihusisha na utengenezaji wa bidhaa zenye nembo ya jina lake ‘Kajumulo’ kama zilivyo nembo za kampuni nyingine kubwa duniani kama Nike, Adidas, Reebok na nyinginezo.
Bidhaa za Kampuni ya Kajumulo soko lake kubwa liko nchini Marekani yaliko makazi yake akiuza zaidi kwenye vyuo na klabu nyingine mbalimbali duniani.
Watanzania wengi wanamkumbuka mwanamichezo huyu kipindi alipokuja nchini miaka ya nyuma na kuweka jina lake kwenye ramani ya michezo akianzisha timu yake ya Kajumulo baada ya kuinunua iliyokuwa ikijulikana kama Moro United.
Hakuwa na utani, kuonyesha kuwa alidhamiria kufanya makubwa kwenye soka la Bongo, kwanza aliipeleka timu hiyo iliyokuwa inashiriki Ligi Kuu Bara, kuweka kambi nchini Brazil kama zifanyavyo sasa Simba na Yanga zinazopishana Uturuki na Afrika Kusini.
Bosi huyo mwenye majina mengi ya utani kama Babu Kaju na Bushi Men, aliwahi pia kuichezea klabu ya maveterani ya Tanzania Stars iliyokuwa inashiriki Ligi Kuu.
Ukipata bahati ya kukutana naye kimwonekano unaweza ukajiuliza, ‘jamaa mwenyewe ndiyo huyu, mbona wa kawaida sana’, lakini asikuambie mtu jamaa kichwani akili ni nyingi na anafanya mambo makubwa sana.
Hapendi makuu
Kajumulo ana rasta. Rasta ambazo si ndefu sana, za kawaida tu lakini zinazopewa matunzo.
Hata hivyo, unaweza ukawa unajiuliza vipi matunzo yake? Kumbe mwenyewe wala hana makuu na rasta zake hizo kwa mwaka anazihudumia kwa gharama ndogo tu ya Dola 10 (Sh24,000) kwa mwaka na alianza kuzifuga tangu akiwa kijana mdogo. “Maisha yangu ni kawaida kama unavyoniona, napenda vitu vya asili, nywele hizi napaka mafuta, shampuu ya kawaida tu, sawa na ninayopaka mwili wangu, ndiyo maana gharama iko chini,” anasema Kajumulo ambaye kwa rangi ni mweusi na mwili wake ni mnene.
SIO MUHUNI
Anakiri tangu akiwa mdogo wengi walikuwa wanamchukulia ni muhuni kwa sababu ya mambo anayofanya pamoja na mwonekano wake. Hata hivyo kuitwa huko hata sasa hakumshtui kwani si jambo geni kwake na hana mpango na mambo hayo kabisa.
“Mimi si muhuni, si mtu wa anasa, sinywi pombe, sivuti sigara wala dawa za kulevya, ndiyo maana nimefanikiwa kwa sababu pesa yangu inakwenda katika mambo muhimu,” anasema.
Kajumulo ambaye mbali na biashara ni mtunzi na mwimbaji na anamiliki bendi ya Bush Men.
“Ninachoamini walinichukulia muhuni kwa sababu ya mambo ninayoyafanya ni makubwa tofauti na akili zao. Wanaona ni ajabu sana. Hata hivyo, mbona ninachofanya hata wengine wanafanya, kwa mfano kumiliki timu, wengi wanafanya hayo.”
UJIO WAKE NCHINI
Kajumulo ambaye ni Mtanzania mwenye makazi yake nchini Marekani iliko pia familia yake sambamba na biashara zake, anasema amekuja nchini akiwa na mipango yake mingi tu.
Kajumulo aliyasema hayo alipotinga kwenye ofisi za Kampuni ya Mwananchi Communications Limited, wazalishaji wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti linalokupa taarifa hizi.
“Nimekuja kwa lengo moja kubwa la kuendeleza soka Tanzania, baada ya kupata taarifa kutoka kwa rafiki yangu Zamunda (Rahimu mmiliki wa African Lyon) kuwa soka Tanzania kwa sasa haliko vizuri na hata ukiangalia kwenye viwango vya Fifa,” anasema Kajumulo ambaye anaweka wazi ana undugu na Anna Tibaijuka.
Anachozungumza Kajumulo ni kama kweli kwa sababu kwa sasa Tanzania ni ya 137 kwenye viwango vya Fifa kati ya nchi 211, zikiongozwa na Ubelgiji huku San Marino ikishika mkia. Awali Tanzania iliwahi kupanda hadi nafasi ya 67.
KUICHUKUA LIGI YA WANAWAKE
“Ligi zinaendeshwa hakuna mdhamini, ligi za wanawake na vijana si salama na ndiyo maana katika ujio wangu, nimelenga huko na nimekaa na TFF na kuzungumza nao mpango wa kuwekeza kwa wanawake,” anasema Kajumulo ambaye anamiliki pia Kajumulo World Soccer.
“Udhamini si pesa tu, nitawatafutia vifaa vya michezo, jezi, viatu na mambo mengine kama wadhamini ili mradi mambo yaende vizuri.” Anasema uamuzi huo ni kwa sababu ana mtoto wa kike anayeitwa, Nia, ni mpenzi wa soka na anacheza pia:
“Mwanangu anapenda soka, nafanya hivyo kwa ajili ya kumfurahisha yeye. Binti yangu anapokuwa na furaha na mimi nafarijika.”
Anasema jambo lingine lililomfanya awekeze kwa wanawake ni kwa sababu anaamini ligi hiyo ikiboreshwa Twiga Stars inaweza kucheza Kombe la Dunia miaka ijayo tofauti na wanaume ambao wamekuwa wanapambana lakini hawafiki mbali.
kuwatoa VIJANA
Kajumulo anasema, lengo lingine ni kuwatafutia timu vijana wenye ndoto za kuwa wachezaji wakubwa: “Mpango ni huo kwa sababu samaki unatakiwa kumkunja akiwa mbichi. Kuna programu ambayo naifanya na Zamunda lakini bado mambo hayajakaa sawa.”
“Ni mpango ambao naufanya Marekani lakini sasa nataka kuuleta hapa nyumbani Tanzania uwasaidie vijana bado naendelea na uchunguzi kuona namna gani utaenda sawa,” anasema Kajumulo ambaye anaweka wazi Marekani anamiliki akademi inayoitwa Pass Academy na hufanya mpango huo.
Anasema makocha watakuwa ni wazawa wachezaji wa zamani ambao wamekuwa hawathaminiki nyumbani, wanajisomesha kozi mbalimbali lakini hawapati kazi.
KIINGEREZA TATIZO WACHEZAJI BONGO
“Shule mimi nilikimbia darasa la tisa. Nilichokuwa nakitafuta ni kujua masomo mawili tu ambayo ni Kiingereza na Hesabu kwa sababu ndivyo natumia mpaka sasa. Nijue kuhesabu pesa kwenye Hesabu na Kiingereza katika mawasiliano,” anasema Kajumulo.
Kiingereza kwa Watanzania ni tatizo na inawakwamisha watu wengi hata wachezaji na kumtolea mfano mchezaji mmoja wa Tanzania aliyempeka Marekani na England kwa majaribio lakini kitu kikubwa kilichomkwamisha ni Kiingereza.
“Unajua kama unajua lugha rahisi, Kiswahili ni lugha kubwa lakini wanaoijua ni wachache huwezi kuifananisha na Kifaransa au Kihispania sasa kwenye timu za wenzetu walioendelea wakiona kama hauna umuhimu sana wanaachana na wewe kwa sababu utawapa kazi ya kukufundisha,” anasema Kajumulo anayekubali soka ina lugha moja lakini si kama inavyochukuliwa.
“Katika programu yangu ya kutafuta vijana wadogo wa kuwatafutia timu vipaumbele vyangu katika kuwaendeleza kwanza ni kuwafundisha mpira na pili Kiingereza ili iwe rahisi kwao,” anasema Kajumulo ambaye hatamani kuwa kiongozi wa TFF kwa sababu haishi Tanzania.
ISHU YA NTEZE JOHN NA KALI ONGALA
Kajumulo aliwahi kuwachukua wachezaji wa zamani kama Kalimangonga Ongala (Kali), Salvatory Edward na Ntenze John na kuwapeleka Marekani.
“Kali alifanikiwa kucheza kwa kiwango cha juu Marekani na Jamaica baadaye nilimpeleka England akajaribu lakini aliumia mguu hakufanikiwa akarudi Marekani. Alitoka tena Marekani kwenda England kwa makazi.” Anasema Nteze na Salvatory aliwachukua akawapeleka Uswizi na Uturuki kwa majaribio lakini hawakufanikiwa.
“Salvatory alitaka kurudi nyumbani akarudi yupo mpaka sasa na Nteze bado anaishi Marekani. Nteze anafanya kazi katika Kampuni ya Microsoft, ana familia yake na mambo yake yanakwenda vizuri kabisa,” anasema Kajumulo na kuweka wazi Nteze ni mchungaji kwa sasa. Amemzungumzia pia, Rashid Matumla ‘Snake Boy’: “Nilimchukua na kumtafutia mapambano Marekani lakini mwishowe alitamani kurudi nyumbani, nikamruhusu na sikumrudisha tena.”
anaitaka YANGA
Simba ipo kwenye mpango wa kumilikiwa na tajiri Mohamed Dewji ‘Mo’, Kajumulo anasema mpango wake kwa klabu za African Lyon na Yanga ni kuzisaidia zibaki kwa wanachama.
“Kuna mambo yako kwenye mpango, nitakayofanya juu ya African Lyon na Yanga mtajulishwa. Nimechagua Yanga kwa sababu ni timu ya wananchi na ni asili ya Mtanzania tofauti na Simba ilianza kama Sunderland ikaja kubadilishwa jina baadaye,” anasema Kajumulo na kutolea mfano timu za Barcelona na Real Madrid za Hispania ni za wanachama na zinafanya vizuri.
Anasema, hii si mara ya kwanza kwani mwaka 1998, aliisaidia Yanga jezi na kuwatengenezea nguo kwa ajili ya kuuza pamoja na hela kwenda kushiriki mashindano ya Afrika Mashariki nchini Uganda.
Kajumulo amempongeza Zamunda kwa anachokifanya kama kumiliki timu ya African Lyon na anasema hamsaidii kwa lolote, anataka apambane mwenyewe ili afanikiwe:
“Naweza kumsaidia Zamunda akasonga lakini namwacha makusudi ili apambane mwenyewe ajifunze.”
KUMBE ni YANGA BWANA
Haikuwahi kujulikana Kajumulo ni shabiki wa klabu gani kati ya Simba na Yanga lakini amelitamkia Mwanaspoti yeye ni Yanga: “Mimi ni mwanamichezo ni mpenzi wa Yanga.”
MPIRA SI PESA
Kajumulo ambaye pamoja na kuendesha klabu tofauti anasema yote hayo yanafanyika kwa sababu ya mipango tu na si pesa.
“Pesa si kila kitu, utajiri ni mawazo. Azam FC wana pesa nyingi tu na inataka kufanya mambo makubwa lakini inashindwa kufikia malengo yao kutokana na sababu tofauti,” anasema. Amesema anaweza kutoa wazo zuri bila pesa likalipa. Ametolea mfano wazo alilowahi kuwapa TFF miaka ya nyuma watengeneze jezi za Taifa Stars na aziuze kwenye maduka Marekani zitaingiza pesa kwao. Tajiri huyo ambaye ni kocha wa soka anasema, amepanga kuendesha kozi ya makocha na anafanya mazungumzo na TFF.
“Sijatamani kuja kufundisha mpira Tanzania lakini nina mpango wa kozi ya makocha ili iwasaidie muda wowote nitakapokuwa tayari na TFF kama watakubali kuniunga mkono,” anasema Kajumulo.
WACHEZAJI BONGO HAMNA KITU
Anasema wachezaji wa Tanzania kwa sasa hakuna anayeweza akapata timu Ulaya akafanya vizuri lazima aelimishwe na kujifunza kwa sababu mpira unabadilika kila siku.
“Kwenda kucheza Ulaya labda mpira wa ndondo lakini si wa ushindani kwa sababu inahitaji maandalizi mengi,” anasema Kajumulo.
Kajumulo hakuacha kuwapa neno wachezaji wa Tanzania kuwa ukitaka kufanikiwa ni lazima upambane, usote na mambo mengine mengi.
“Kuna wachezaji wanapata nafasi kucheza timu Ligi Kuu ni bahati ili kujionyesha na upate timu kubwa zaidi, lakini wa sasa wanalizika na kufanya mambo mengine yasiyokuwa na maana,”anasema Kajumulo na kutolea mfano namna alivyokuwa anacheza soka miaka ya nyuma walinyenyekea ndiyo maana wakafika hapo.
BENDI BUSH MEN SOUND
Anasema bendi yake ya Bush Men mara nyingi inapiga kwenye vyuo vya wanafunzi: “Lengo la muziki wangu ni kwa ajili ya kuelimisha zaidi na huwa napiga vyuoni Marekani.”
“Kila unachofanya ni malengo ya bendi hii ni kufikisha ujumbe na siangalii sauti yangu inafaa au haifai. Naimba kuelimisha mambo ya kijamii na mengine.”
Amezungumzia kwa nini ameiita Bush Men: “Napenda Bush Men kwa sababu ndiyo asili ya maisha yangu, pia Adam na Hawa wametoka katika maisha haya haya.”
BIASHARA inayolipa
“Biashara ya nguo za michezo ndiyo ilinipa pesa nyingi. Enzi zile Marekani walikuwa wazuri zaidi kwenye mpira wa basketi, soka hawakuwa wanajua hivyo nilitumia nafasi hiyo na nikapata masoko kwa wingi,” anasema Kajumulo
KAJUMULO ilivyokufa
“Baada ya kupambana Marekani niliamua kurudi Tanzania na kuanzisha timu lengo ni kuufanya mpira kuwa juu. Lakini kwa sababu mimi ni mfanyabiashara na naishi Marekani, baada ya kuanzisha Kajumulo Tanzania niliamua nirudi huko,” anasema Kajumulo ambaye aliwahi kuipeleka nchini Brazil kwa ajili ya kambi.
“Niliiacha timu ikiwa vizuri na mtaji wa kutosha. Niliacha malori, magari, nguo na pesa nyingi tu za kutosha lakini kilichotokea ndiyo hivyo na hii ni kwa sababu wazo lilikuwa langu niliowaachia wakashindwa kuliendeleza.”
Anasema sababu kubwa ni watu aliowaachia timu hakuwapa elimu ya uongozi na biashara (menejimenti) jambo lililosababisha mali ikapotea kwa sababu ilikuwa inatoka tu, haiingii, wakafilisika.
Anasema hii hajaifanya Tanzania kwa Kajumulo tu bali katika mataifa kama Ghana na Jamaica.
SAFARI zA nje, Utajiri
Ni mzaliwa wa Bukoba, alisoma huko elimu ya msingi na baadaye alihamia mkoa wa Morogoro Shule ya Sekondari Kigurunyembe.
Alicheza mpira na malengo yake yalikuwa atoke kwenda nje ya nchi na safari ya kwanza ilikuwa Kenya baadaye Somalia, Djibout, Yemen, Uholanzi, Ufaransa, Canada hadi Marekani alikoweka makazi yote alikuwa anatafuta nafasi kutimiza malengo yake.
“Kuna watu walinishauri nitoke kwenda nje ya nchi, wao walijaribu hawakufanikiwa na kwa sababu hayo ndiyo yalikuwa malengo yangu nikapambana,” anasema Kajumulo anayefafanua hakuzamia meli lakini safari yake ilikuwa ya meli.
Anasema alipata kazi kwenye meli kwa sababu ya kazi ya mama yake mzazi: “Nilipata kazi kwenye Meli. Kazi yangu ilikuwa kufanya usafi kwenye meli kusafisha vyakula kama maharagwe na mengine. Nikapata nafasi kuzunguka na meli kwenda mataifa hayo,” anasema Kajumulo aliyeamua kutulia Marekani kwa sababu alikuwa anapata pesa nyingi kwa sababu ya soka.
“Niliingia Marekani kwa ajili ya maandalizi ya Kombe la Dunia ndiyo ilikuwa tiketi yangu na kuanza maisha. Nikiwa Marekani nilipata pesa nyingi kwa sababu nilikuwa miongoni mwa wachezaji waliokuwa wanatembea kila jiji kutangaza soka, “anasema Kajumulo aliyeingia Marekani miaka ya 90 na Kombe la Dunia Marekani lilichezwa mwaka 1994, bingwa alikuwa Brazil.
FAMILIA YAKE
Kajumulo anasema, alioa mwanamke wa kizungu anayeitwa Cerry ambaye ni profesa. Mwanamke huyo anadaiwa kuwa na pesa nyingi. “Profesa anapata wapi pesa na nilimwoa yeye akiwa bado si profesa. Mimi ndiyo nilikuwa na pesa kutoka kwenye soka, nilimwoa akiwa hana pesa,” anasema Kajumulo anayeishi Seattle huko Marekani.