Ambundo ajichomoa Fountain Gate

Muktasari:
- Ambundo alijiunga na Fountain Gate mwanzoni mwa msimu huu akitokea Singida Black Stars na ameifungia timu hiyo mabao mawili kabla ya kuondoka kambini wakati timu ikipambana kumaliza katika nafasi nzuri katika msimamo wa Ligi Kuu iliyosaliwa na raundi nne za mechi kumalizika.
KIUNGO mshambuliaji wa Fountain Gate, Dickson Ambundo amejiengua katika kikosi hicho kwa madai ya kutolipwa malimbikizo ya fedha zikiwamo za usajili zipatazo Sh50 milioni.
Ambundo alijiunga na Fountain Gate mwanzoni mwa msimu huu akitokea Singida Black Stars na ameifungia timu hiyo mabao mawili kabla ya kuondoka kambini wakati timu ikipambana kumaliza katika nafasi nzuri katika msimamo wa Ligi Kuu iliyosaliwa na raundi nne za mechi kumalizika.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ambundo alisema ni kweli hayupo pamoja na timu kutokana na kuwa na malimbikizo ya madeni na waajiri wake hao.
“Ni kweli sipo pamoja na timu kwa sababu nina madai na timu hiyo na tayari nimepeleka malalamiko yangu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili kupambania haki yangu,” alisema nyota huyo wa zamani wa Alliance, Yanga na Dodoma Jiji.
Hata hivyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Fountain Gate, Kidawawa Tabitha alipotafutwa na Mwanaspoti ili kuthibitisha madai hayo ya Ambudno, alikanusha timu hiyo kudaiwa na kuweka wazi kuwa mchezaji huyo yupo nje ya timu kutokana na kuomba ruhusa ya kujiuguza.
“Taarifa hizo hazina ukweli wowote. Ambudo bado ni mchezaji wetu halali yupo nje ya timu, kwa sababu anaugua na taarifa hiyo ndiyo tuliyonayo kuhusu kuidai klabu ndio kwanza nakusikia wewe,” alisema Tabitha.