Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Azam vs Simba: Historia, ushindi na presha zikijumuika Mzizima Dabi

Muktasari:

  • Uzuri wa mechi hii ni kwamba unaweza kuwa mtoko wa sikukuu kwani baada ya mchana kushiba pilau, usiku saa 1:00 kipute kitapulizwa pale Azam Complex, ambapo wenyeji Azam wanaonolewa na kocha Mkongomani, Florent Ibenge, watakapopambania kulinda heshima nyumbani dhidi ya vijana wa kocha Steve Barker, Simba.

WAKATI leo Jumapili Wakristo wakisherehekea Sikukuu ya Pasaka inayoendana na kumbukumbu ya tukio la kufufuka kwa Bwana Yesu, Jiji la Dar es Salaam sherehe hizo zitanogeshwa na mechi kali ya Ligi Kuu Bara kati ya Azam dhidi ya Simba na mshindi hapo atakuwa ametoa zawadi kwa mashabiki wake.

Uzuri wa mechi hii ni kwamba unaweza kuwa mtoko wa sikukuu kwani baada ya mchana kushiba pilau, usiku saa 1:00 kipute kitapulizwa pale Azam Complex, ambapo wenyeji Azam wanaonolewa na kocha Mkongomani, Florent Ibenge, watakapopambania kulinda heshima nyumbani dhidi ya vijana wa kocha Steve Barker, Simba.

Hii ni Mzizima Derby, ambapo si mechi ya kawaida kwani inazikutanisha timu mbili zinazofukuzana kwa ukaribu katika mbio za ubingwa, huku kila mmoja akihitaji pointi tatu ili kuwakaribia vinara, Yanga.


VITA YA NAFASI

Hali ya msimamo inafanya mechi hii kuwa na presha kubwa. Simba kwa sasa inashika nafasi ya pili ikiwa na alama 34 baada ya mechi 15, huku ikiwa na faida ya mechi moja mkononi dhidi ya mpinzani wake wa jadi, Yanga, mwenye alama 38 kabla ya kucheza na Tanzania Prisons jana Jumamosi. Kwa upande wa Azam, ipo nafasi ya tatu ikiwa na alama 32 baada ya mechi 16. Ushindi kwa Azam itaifanya ipae hadi nafasi ya pili na kuishusha Simba, wakati ushindi kwa Simba itaifanya kukisha alama 37 na kupumua kisogoni mwa Yanga.


IBENGE VS BARKER

Mechi hi inatarajiwa kuwa wa kimbinu zaidi. Kocha wa Azam, Florent Ibenge, amejenga timu imara inayojua kushambulia kwa kushtukiza na kutumia mtego wa kumfanya adui akosee pindi mpinzani anapoanza mpira kuanzia nyuma. Ibenge anapendelea kutumia mfumo wa 4-2-3-1, akitegemea zaidi ubunifu wa viungo wake na kasi ya pembeni.

Kwa upande wa pili, kocha wa Simba, Steve Barker, anahusudu zaidi soka la kumiliki mpira na udhibiti wa mchezo. Barker amekuwa akilalamikia upotezaji wa mipira ovyo, hivyo leo anatarajiwa kuingia na mbinu ya kuhakikisha Simba inatulia na mpira ili kuwavuruga Azam.

Vita itakuwa kubwa katikati ya uwanja ambapo Simba itategemea uwiano wa Yusuph Kagoma na Alassane Kante kuzuia mashambulizi ya Azam, huku Azam wakimtumia Feisal Salum kama injini yao.

Wakati Simba inafungwa 2-0 na Azam katika mzunguko wa kwanza wa ligi, Barker hakuwepo, kikosi kiliongozwa na Seleman Matola, lakini makocha hao wakaja kukutana nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026, Ibenge akamchapa Barker 1-0.


KAZI IPO HAPA

Kwenye nyasi za Azam Complex pale Chamazi, kuna pambano la wazi la wachezaji ambapo mbali na mbinu, kuna wachezaji wenye uwezo wa kuamua mechi dakika yoyote.

Beki wa kulia na nahodha wa Azam, Lusajo Mwaikenda, amekuwa na uwezo mkubwa wa kupandisha mashambulizi, lakini hapa atakutana na mtihani mzito dhidi ya kasi ya winga wa Simba, Anicet Oura, ambaye ni moja ya silaha hatari za Barker upande wa kushoto.

Fei Toto, ambaye ana mabao saba na pasi tano za mabao, ndiye mchezaji wa kuchungwa zaidi na Simba kutokana na uwezo wake wa kutafsiri matukio kwa haraka.

Mshambuliaji wa Simba, Seleman Mwalimu, yuko kwenye fomu nzuri akiwa na mabao sita msimu huu, ndiye kinara wa mabao kikosini hapo na leo atakuwa na kazi ya kuvunja ukuta wa Azam unaoongozwa na beki wa kati, Yoro Diaby.

Idd Seleman ‘Nado’ wa Azam amekuwa mbunifu mkubwa wa mabao, akitengeneza asisti mbili katika ushindi uliopita dhidi ya Singida.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Azam, Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’ alisema kuna wachezaji watawakosa leo kutokana na majeraha ya muda mrefu ambao ni Abdul Suleiman ‘Sopu’, Yahya Zayd, Adolf Mtasingwa na Edward Charles Manyama, huku Nassor Saadun akirejea baada ya kupona.

Kwa upande wa Simba, majeruhi wao walewale wa muda mrefu akiwemo Wilson Nangu, Abdulrazack Hamza, Yakoub Suleiman hawatakuwepo sambamba na Jonathan Sowah aliyesimamishwa.


AZAM COMPLEX PAGUMU

Uamuzi wa Azam kuipeleka mechi hii Azam Complex badala ya uwanja mwingine ukiwemo Benjamin Mkapa walipocheza mara ya mwisho dhidi ya Yanga na kutoka 0-0, unaelezwa umetokana na shinikizo la Ibenge aliyetaka kikosi chake kitumie faida ya uwanja wa nyumbani.

Hilo linaweza kuwa na hoja kwani Ibenge baada ya kutoka 0-0 dhidi ya Yanga, alinukuliwa akisema hakuona sababu ya mechi hiyo kuchezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa. Hata hivyo, Ibenge aliiongoza Azam kuifunga Simba 2-0 uwanjani hapo Kwa Mkapa katika duru la kwanza.

Takwimu zinaonesha timu hizi zimekutana mara tatu pale Azam Complex, na mechi zote ziliisha kwa sare, huku mbili zikiwa za 1-1. Moja 0-0.

Matokeo hayo yanaonesha ugumu uliopo ndani ya dimba hilo kupata ushindi pindi zinapokutana Azam na Simba, hivyo leo tutarajie ugumu huo ama mwanzo mwingine mpya wa matokeo mapya.

Mara ya mwisho Mzizima Derby kuchezwa Azam Complex, ilikuwa Mei 18, 2020 ambapo matokeo yalikuwa sare ya 1-1. Rodgers Kola alianza kuifungia Azam dakika ya 37, kisha John Bocco akaisawazishia Simba dakika ya 45.

Mechi ya leo, Simba inatafuta nafasi ya kulipa kisasi baada ya kupoteza 2-0 katika mzunguko wa kwanza pale Kwa Mkapa, Desemba 7, 2025, wakati Azam ikihitaji kuendeleza ubabe kwani msimu huu imekutana na Simba mara mbili na kushinda zote bila ya kuruhusu bao.

Ilianza mechi ya ligi ikashinda 2-0, kisha nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026, ikashinda tena 1-0. Kabla ya hapo, Azam ilikutana na Simba mara tano kwenye ligi bila ushindi, ikiambulia sare tatu na vichapo vinne.

Ushindi wa Desemba 7, 2025 ulikuja baada ya mara ya mwisho kushinda 1-0, Oktoba 27, 2022.