Baada ya ubingwa, Clara akitaka kiatu Saudia

Muktasari:
- Al Nassr inayoshiriki Ligi ya Wanawake Saudia juzi imechukua ubingwa kwa kuitandika Al Ahli mabao 3-1 bao moja likifungwa na Luvanga na unakuwa ni ubingwa wa tatu mfululizo kwa timu hiyo.
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania anayewasha moto katika klabu ya Al Nassr, Clara Luvanga amesema mabao 15 aliyofunga yanampa hamasa ya kuwania kiatu cha dhahabu huku supastaa wa dunia, Cristiano Ronaldo akiwapongeza baada ya kuchukua ubingwa.
Al Nassr inayoshiriki Ligi ya Wanawake Saudia juzi imechukua ubingwa kwa kuitandika Al Ahli mabao 3-1 bao moja likifungwa na Luvanga na unakuwa ni ubingwa wa tatu mfululizo kwa timu hiyo.
Timu hiyo imechukua ubingwa bila kupoteza mchezo wowote ikiwa imebakisha mechi mbili kumaliza msimu, imekusanya pointi 48 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yeyote.
Baada ya kuchukua ubingwa huo, Ronaldo ambaye pia anaichezea Al Nassr kwa upande wa wanaume aliipongeza timu hiyo kwa kuwapigia makofi kwenye ukurasa wa mabingwa hao.
Clara Luvanga anakuwa Mtanzania wa kwanza kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Saudia mara mbili mfululizo tangu alipojiunga nayo msimu 2023/24 akitokea Dux Logrono ya Hispania.
Msimu wake wa kwanza aliiwezesha timu hiyo kubeba taji la Ligi likiwa la pili mfululizo na kufunga mabao 11 akimaliza kwenye tatu bora ya wapachikaji mabao.
Msimu huu tayari amefunga mabao 15 mbele ya kinara, Iptissam Jraidi wa Al Ahli na Ajara Nchout (Al Qadsiah) mwenye nayo 22 na Naomi Kabakaba wa Ahli mwenye 20.
Akizungumza na Mwanaspoti baada ya kunyanyua ndoo hiyo Clara alisema "Ninafurahi kuwa moja ya wachezaji nilio ipa timu ubingwa pia kwangu mimi hii nzuri sana, natamani pia kuchukua kiatu."
Kama msimu huu nyota huyo atachukua kiatu cha dhahabu basi itakuwa mara yake ya kwanza kwenye maisha yake ya soka la kulipwa.
Logrono, Yanga Princess alikocheza kwa mafanikio hakubeba ubingwa wa ligi wala kuibuka mfungaji bora lakini huenda kukawa na dalili za kiatu msimu huu baada ya kukikosa mwaka jana.