Chama la Wana vita bado inaendelea

Muktasari:
- Katika michezo mitano iliyobakia, miwili ni ya nyumbani na mitatu ni ya ugenini, ikianza na safari ya kupambana dhidi ya Songea United Aprili 13, kisha kurejea kwenye uwanja wake wa Kambarage Shinyanga kuikaribisha Green Warriors Aprili 19.
LICHA ya Stand United 'Chama la Wana', kuchapwa mabao 2-0 na Mbeya City Machi 30, 2025, kocha wa timu hiyo, Juma Masoud amesema kichapo hicho kwao hakijawatoa katika mbio za kuwania tiketi ya kukirejesha Ligi Kuu Bara msimu ujao.
Akizungumza na Mwanaspoti, Masoud alisema anachokitaka ni kuona wachezaji wanaendelea kupambana zaidi uwanjani kwa kila mchezo wanaocheza kwa sasa bila ya kuangalia wapinzani wao, kwa sababu kwa kufanya hivyo itawasaidia kuwaondolea presha.
"Presha ni kubwa sana hasa hii michezo iliyobakia na nafasi ambayo kila timu ipo na pointi ilizonazo, mimi sitaki kuona wanacheza kwa hali hiyo zaidi ya kuwataka kupambana hadi mwishoni mwa msimu kisha tutaangalia tutakapoangukia," alisema.
Masoud alisema gepu la pointi tatu na Mbeya City iliyopo nafasi ya pili sio kubwa, japo anachopambana nacho ni kuongeza umakini katika safu ya ulizi na ushambuliaji, licha ya kukiri ugumu wa kuwania pointi 15, kwa michezo mitano iliyobakia.
Katika michezo mitano iliyobaki, miwili ni ya nyumbani na mitatu ni ya ugenini, ikianza na safari ya kupambana dhidi ya Songea United Aprili 13, kisha kurejea kwenye uwanja wake wa Kambarage Shinyanga kuikaribisha Green Warriors Aprili 19.
Baada ya hapo, itapambana na Cosmopolitan ugenini kwenye Uwanja wa Mabatini Aprili 26, kisha kuifuata tena maafande wa Polisi Tanzania Mei 1, huku ikihitimisha msimu kwa kucheza na Geita Gold inayopambana pia kurejea Ligi Kuu Bara Mei 10.
Kikosi hicho kwa sasa kinashika nafasi ya tatu na pointi 52, baada ya kucheza michezo 25, kikishinda 16, sare minne na kupoteza mitano, nyuma ya Mbeya City iliyopo ya pili na pointi 55 na vinara wa ligi hiyo, Mtibwa Sugar yenye pointi 60.
Kocha huyo wa zamani wa FGA Talents kwa sasa Fountain Gate, amejiunga na kikosi hicho akichukua nafasi ya Meja Mstaafu, Abdul Mingange aliyejiunga na Songea United, huku akiipambania kuirejesha Ligi Kuu baada ya kushuka msimu wa 2018-2019.