Dakika 450 za Malale kufa, kupona Mbeya City

Muktasari:
Malale ametambulishwa rasmi leo Machi 31 kuinoa Mbeya City akichukua nafasi ya Mayanga aliyejiunga na Mashujaa, na sasa kocha huyo mpya anazo dakika 630 za kuipeleka timu hiyo Ligi Kuu.
Kocha Mkuu wa Mbeya City, Malale Hamsini amesema anafahamu ugumu uliopo katika Ligi ys Championship huku akieleza kuwa mkakati wake ni kukata kiu ya mashabiki wa timu hiyo kuirejesha Ligi Kuu Bara.
Malale aliyewahi kung'ara na timu kadhaa za Ligi Kuu, mara ya mwisho aliinoa JKT Tanzania na sasa anaziba pengo la Salum Mayanga aliyetimkia Mashujaa iliyoachana na Abdalah Mohamed 'Baresi'.
Hadi sasa Mbeya City ipo katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 52, ikibakiza michezo mitano kuamua hatima yake ya kurejea Ligi Kuu baada ya kuikosa kwa misimu miwili.
Katika mechi hizo itacheza ugenini tatu dhidi ya Biashara United, Polisi Tanzania na Geita Gold kisha itarejea Sokoine kuikaribisha Cosmopolitan na Green Warriors.
Malale amesema anafahamu vita ilivyo katika ligi hiyo, lakini kwa uwezo na uzoefu alionao katika soka anaamini atakata kiu ya mashabiki kuirejesha timu hiyo Ligi Kuu.
Amesema anachotaka ni ushirikiano kutoka kwa uongozi na mashabiki ili kuhakikisha kwamba wanaendelea kushinda mechi zilizobaki kufikia malengo akisisitiza kuwa timu hiyo kurudi Ligi Kuu inawezekana.
"Nashukuru kwa nafasi waliyonipa, najua kila mmoja shauku aliyonayo. Lazima tuunganishe nguvu pamoja na lazima mechi zilizobaki tutashinda na kurudi Ligi Kuu. Uwezo, nia na uzoefu ninao," amesema kocha huyo.
Kaimu Katibu Mkuu wa timu hiyo, Joseph Mlundi amesema wamempa kazi ngumu kocha huyo wakiamini anaweza kuwavusha kufikia malengo waliyonayo na kuziba nafasi ya mtangulizi wake.
"Amesaini mwaka mmoja na uongozi upo tayari kumpa aina yoyote ya ushirikiano. Tunao mwendelezo mzuri ila kiu kubwa ni Ligi Kuu. Suala la motisha tunaendelea kuongeza kila mechi kwa wachezaji," amesema Mlundi.
Mwenyekiti wa timu hiyo, Newton Mwatijobe amesema mzigo aliopewa kocha huyo anaamini ataubeba akimuomba kuwa mvumilivu kwa kuwa mashabiki wana nguvu wakitaka timu yao ipande daraja.
"Nadhani jana ameona nguvu ya mashabiki pale Sokoine kwenye mechi dhidi ya Stand United. Tunaamini atatupeleka tunapotaka, kiu yetu kubwa ni Ligi Kuu," amesema Mwatijobe.