Dakika 90 ngumu Yanga, JKT

Muktasari:
- Yanga na maafande hao wa JKT zitavaana kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga, huku kocha Hamdi akisema ubora wa wa wapinzani ni moja ya mambo yanayomfanya aanze kujipanga mapema baada ya kupata dawa za kukabiliana nao ili kufuizu fainali na kujiweka pazuri katika kutetea taji inalolishikilia kwa msimu wa tatu mfululizo.
KIKOSI cha Yanga tayari kipo jijini Tanga kwa ajili ya pambano la nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), huku kocha mkuu wa timu hiyo, Miloud Hamdi akisema wana dakika 90 ngumu dhidi ya JKT Tanzania akirejea kilichowakuta katika mechi ya mwishoni katika Ligi Kuu Bara.
Yanga na maafande hao wa JKT zitavaana kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga, huku kocha Hamdi akisema ubora wa wa wapinzani ni moja ya mambo yanayomfanya aanze kujipanga mapema baada ya kupata dawa za kukabiliana nao ili kufuizu fainali na kujiweka pazuri katika kutetea taji inalolishikilia kwa msimu wa tatu mfululizo.
Katika mechi ya mwisho ya Ligi Kuu, timu hizo zilishindwa kutambiana kwa kutoka suluhu kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, ikiwa ni mechi ya kwanza kwa kocha huyo aliyechukua nafasi ya Saed Ramovic aliyekuwa ametimkia CR Belouizdad ya Algeria.
Akizungumza na Mwanaspoti, Hamdi alisema maandalizi upande wao yamekamilika akijua kwamba wanakwenda kukutana na timu nzuri, hivyo amekiandaa vyema kikosi kupambana ili kutinga hatua inayofuata lengo likiwa ni kutetea taji.
Alisema kama mwalimu pamoja na benchi zima la ufundi wamewandaa vyema wachezaji kisaikolojia, lakini kuongeza morali ili kuweza kushinda na kutinga hatua ya fainali na kubeba ubingwa kwa msimu wa nne mfululizo.
Hamdi aliongeza wanajua mechi ya Jumapili kwa wachezaji wa JKT Tanzania watakuwa katika ubora wa hali ya juu, hivyo kwa kutambua hilo ni pambano la mtoano tofauti na Ligi Kuukutokana na kwamba haziji kila siku kama Yanga wanaenda kuthibitisha ubora walionao.
“Naifahamu vizuri JKT Tanzania ni timu ambayo ina kocha mwenye mbinu nzuri na wachezaji wenye vipaji vikubwa ni moja ya timu ambayo imepunguza gepu la pointi katika kikosi chetu baada ya kutoka nao suluhu ikiwa kwao, nimeiandaa timu yangu kuhakikisha tunaingia tukiwa timamu na bora kwa kushinda mchezo huo japo haitakuwa rahisi,” alisema Hamdi.
“Nina wachezaji wazuri wenye uchu wa mafanikio wameniahidi kufanya kitu bora kuelekea mchezo huo na kiujumla sina majeruhi wachezaji wote wamerejea na wapo tayari kwa mchezo matumaini ni kuibuka na ushindi tutaingia kwa kuwaheshimu wapinzani na kutumia mapungufu yao kuwaadhibu.”
Akizungumzia hali ya hewa Hamdi alisema: “Ni baridi, lakini tunajua itatusaidia kwa sababu tunajua hali ya baridi inafanya mwili kufanya kazi muda mrefu tofauti na joto.”
Alisema wanacheza nusu fainali na wanalitaka Kombe la FA kwa sababu wanataka kufikia malengo ya kutwaa kila taji msimu huu kama walivyofanya msimu uliopita hataki kuvunja rekodi akiwa ndani ya timu hiyo zaidi ni kuweka alama mpya.
Kwa upande wa JKT Tanzania iliyowahi kutwaa ubingwa wa michuano hiyo 2002 enzi hizo likifahamika kama Kombe la FA na yenyewe ikiitwa JKT Ruvu, imetamba kiu yake ni kupata matokeo na kutinga fainali ili kusaka tiketi ya michuano ya kimataifa kwa mara nyingine.
JKT licha ya kukata tiketi kwa kutwaa Kombe la FA 2002 ikiifunga timu ya daraja la nne ya Baker Rangers ya Magomeni Mapipa, Dar, lakini haikushiriki michuano ya CAF baada ya jina lake kuchelewa kupelekwa na Chama cha Soka Tanzania (FAT, sasa TFF).
Kocha wa timu hiyo, Ahmad Ally alisema dakika 90 zitaamua mechi hiyo, lakini anajua halitakuwa pambano rahisi kwa vile Yanga ni timu nzuri, ila hata wao ni wazuri ndio maana wapo nusu fainali.
Yanga imetinga hatua hiyo kwa kuing’oa Stand United kwa mabao 8-1 kwenye robo fainali, wakati JKT iliinyoosha Pamba Jiji kwa mabao 3-0. “Tumecheza nao lakini hilo halitufanyi tukaingia na akili ya mechi zilizopita, hapana. Tunaifahamu Yanga ni bora na ina wachezaji wenye uwezo, tunapambana kuhakikisha tunaingia tukiwa tunaifahamu vizuri na kujiweka tayari kwa ushindani. Ni mchezo ambao matokeo ndio yanaamua nani anasonga hatua inayofuata,” alisema Ahmad.
Safu ya ushambuliaji ya JKT Tanzania inaongozwa na mkongwe John Bocco, Edward Songo, Shiza Kichuya, Hassan Dilunga na Matheo Antony ambaye pia msimu huu alikuwa nje kwa muda kutokana na majeraha.
Nusu fainali nyingine ya michuano hiyo ambayo bingwa wake anaiwakilisha nchi katika Kombe la Shirikisho Afrika ni ile ya Simba dhidi ya Singida Black Stars itakayopigwa Mei 31 kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, uliopo mjini Babati mkoani Manyara.