Dar City, Pazi BDL kama Simba, Yanga

Muktasari:
- Timu hizo zina wachezaji mastaa wa ndani na nje mfano Dar City kati ya waliocheza alikuwepo Hasheem Thabeet aliyecheza klabu kubwa tofauti duniani baadhi zikiwa ni Memphis Grizzlies, Dakota Wizards, Houston Rockets, Rio Grande Valley Vipers na Portland Trail Blazers.
LICHA ya juzi kuchezwa mechi tofauti za Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL) iliyokuwa na mvuto, msisimko na kujaza mashabiki katika viwanja vya Don Bosco Upanga ni ile iliyohusisha Dar City na Pazi.
Timu hizo zina wachezaji mastaa wa ndani na nje mfano Dar City kati ya waliocheza alikuwepo Hasheem Thabeet aliyecheza klabu kubwa tofauti duniani baadhi zikiwa ni Memphis Grizzlies, Dakota Wizards, Houston Rockets, Rio Grande Valley Vipers na Portland Trail Blazers.
Pia amewahi kuichezea Pazi 2023 akitokea TaiwanBeer HeroBears. Kwa Dar City alikuwa nayo toka 2024 alitokea Kaohsiung 17LIVE Steelers, pia aliwahi kuichezea Savio 2021 alitokea Hsinchu JKO Lioneers ni kati ya wachezaji waliokuwa kivutio katika mchezo huo.
Japo Dar City ilishinda kwa pointi 62-47 dhidi ya Pazi mchezo ulikuwa mgumu na presha kubwa kwa mashabiki na makocha.
Kocha wa Dar City, Mohamed Mbwana alisema: “Kutokana na usajili tuliyoufanya katika timu kama Thabeet aliyecheza NBA, wawili kutoka Nigeria ambao ni Shaloom, Clintony yupo aliyetoka Marekani alikuwa anachezea timu za vyuo Jamil Mabuary, wengi walihitaji kuona timu itakuwa na muunganiko gani.”
“Mchezo ulikuwa mgumu na mzuri kwa mashabiki, timu zimeshindana kwa kiwango cha juu, naamini Ligi ya msimu huu mashabiki watafurahia kuona burudani,” aliongeza kocha huyo huku upande wa mjumbe wa Pazi, Samwel Mapalala akisema: “Katika timu kuna wachezaji ambao wametoka Kenya na Uganda na tukikutana kucheza na Dar City inakuwa kama Simba na Yanga katika soka kwa sababu Dar City imezaliwa kutoka Pazi.”
Ukiacha mchezo wa Dar City na Pazi mechi ya wanawake baina ya Ukonga Queens iliyoifunga vikapu 53 kwa 34 JKT, ulikuwa wa aina yake, ingawa mashabiki hawakujaa kama hiyo mechi ya wanaume.
Ukonga Queens ilionekana kucheza vizuri zaidi kwa namna walivyokuwa wanarusha mipira iliyo na nguvu na kufika maeneo sahihi, ushapu wa wachezaji kama Najim Manji (miaka 16) ambaye ni mwanafunzi alikuwa na uwezo wa kutoka na mpira katika goli lao na kwenda kufunga kwa wapinzani alikuwa kivutio kwa mashabiki.
MASHABIKI
Aina ya mashabiki wa mchezo huo ni ‘masistadu’ na ‘mabrazameni’ kwani shangilia yao ni ya kistaarabu wakati mwingine unayasikia maneno ya Kingereza wakiwatia moyo wachezaji waliopo uwanjani kama “go go” (nenda, nenda) defend (linda)... kuna vaibu la aina yake la kumtoa mtu msongo wa mawazo.
Asilimia kubwa ya mashabiki hao wengi walikwenda na magari na kwa kifupi ni watu wanaoonekana kuwa hawana shida ndogondogo.
BABA LEVO
Msanii wa Bongo Fleva, Baba Levo aliyewahi kutamba na nyimbo kama Amen, Binadamu, Kanyaga Twende, Wanyee, High na Low na nyinginezo baada ya kufika uwanjani alihakikisha uwepo wake unafahamika kwa kupiga kelele akitamba: ”Nimeshafika sasa”.
Alipoingia alianza na mkwara kuwaambia wachezaji wa Dar City waifunge Pazi vikapu 100, ingawa kuna wakati presha ilikuwa kubwa iliyomfanya anyamaze kwa muda ilipokuwa inashambuliwa timu anayoishabikia.
MISOSI YA MAANA
Misosi iliyokuwa inauzwa pembeni ya viwanjani hivyo kama soseji, ndizi, mishikaki vyote vya kuchomwa na vilionekana kuandaliwa kwa kiwango cha usafi wa juu, hivyo watazamaji wa mchezo huo walinunua na kukaa jukwaani wakila na kutazama kinachoendelea.
TIMU ZINAZOCHEZA BDL
JKT, ABC, Mchenga Stars, Kampala International University, Pazi, UDM Outsiders, Dar City, Polisi, Stein Warriors, Kurasini Heat, Mgulani, Srelio, Vijana ‘City Bulls’, Savio, DB Oratory na Chui.
USHABIKI WA KISTAARABU
Mechi za juzi zilizoanza kuchezwa saa 12:00 jioni zikianza timu za wanawake Ukonga Queens ikishinda kwa vikapu 53 - 34 dhidi ya Mgulani JKT, lakini haikuwa na msisimko mkubwa kama ilivyokuwa ya wanaume kati ya Dar City na Pazi.