Prime
Fadlu aiachia msala Yanga
SAA chache baada ya kumalizana na Raja Casablanca ya Morocco, Kocha Fadlu Davids hatimaye amea-mua kuvunja ukimya kuhusu tetesi zinazoendelea kusambaa kwa muda mrefu zikimhusisha na Yanga akitoa kauli ambayo imezidi kuchochea uwepo wa dili hilo.
Jina la Fadlu limekuwa likitajwa kama mmoja wa makocha wanaopewa nafasi kubwa ya kuinoa Yanga msimu ujao, baada ya klabu hiyo kuanza mchakato wa kutafuta kocha mkuu baada ya kuondoka kwa Pedro Goncalves.
Inaelezwa viongozi wa Yanga walivutiwa zaidi na uwezo wa Fadlu walioushuhudia alipokuwa akiinoa Simba msimu wa 2024/25, hasa katika michuano ya kimataifa na aliiongoza timu hiyo katika msimu wake wa kwanza kufika fainali katika Kombe la Shirikisho Afrika.
Katika safari hiyo, Simba ilionyesha soka la kuvutia na nidhamu kubwa ya kiufundi, jambo lililomjengea heshima kubwa miongoni mwa viongozi na mashabiki wa soka nchini na kutokana na kutokuwa na timu kwa sasa inafungua njia kwa Yanga kukamilisha vyema mchakato wa kumnasa kocha huyo.
Kwa sasa Yanga ipo chini ya kocha wa muda, Abdihamid Moallin ambaye amekabidhiwa jukumu la kui-ongoza wakati uongozi ukiendelea kufanya tathmini ya kocha atakayechukua mikoba muda mrefu.
Mwanaspoti lilimtafuta kocha huyo ili kujua msimamo wake kwa sasa na alisema baada ya kumalizana na Raja Casablanca ambayo ameiacha ikiwa nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu Morocco ikiwa na pointi 42 katika mechi 23, ameamua kwanza kurejea nyumbani Afrika Kusini kwa ajili ya mapumziko kabla ya kufanya uamuzi kuhusu hatua inayofuata.
“Nahitaji mapumziko kwanza baada ya muda tutaona nini kitatokea,” alisema Fadlu katika mazungum-zo mafupi na Mwanaspoti.
Matokeo yasiyoridhisha ndani ya Raja Casablanca yamechochea pande hizo kumalizana kabla ya muda licha ya kwamba Msauzi huyo alikuwa na mkataba wa miaka miwili, jambo lililofungua mlango kwa Yanga ambao awali walitakiwa kulipa Dola 600,000 (zaidi ya Sh1.5 bilioni) ili kupata huduma yake.
Baada ya kuachana na miamba hiyo ya soka la Morocco, kocha wa zamani wa Yanga, Nasreddine Nabi anapewa nafasi kubwa ya kurithi mikoba yake na inaelezwa wamefanya naye makubaliano ya awali.
ALIVYOPEWA ‘THANK YOU’
“Sambamba na dira yake ya kimkakati ya kuendeleza mradi wa michezo na kuongeza maendeleo en-delevu ya kikosi cha kwanza, Raja Club Athletic inatangaza kusitisha ushirikiano wake na kocha wa kikosi cha kwanza, Bw. Fadluraghman Davids (Fadlu), pamoja na benchi lake la ufundi, kwa makubali-ano ya pande zote mbili,” ilisema klabu hiyo katika taarifa yake.
“Raja Club Athletic inathibitisha tena dhamira yake thabiti ya kuendelea kufanya kazi kwa kujituma ili kutimiza matarajio ya mashabiki wake waaminifu na kufikia malengo iliyojiwekea, kwa ajili ya kulinda hadhi na historia kubwa ya klabu hiyo.”