Fatema Dewji: Ilinichukua miezi mitatu kuikubali Simba Queens

ACHANA na namna wadau walivyoshituka na kupingana namna ambavyo Bodi ya Wakurugenzi ya ilipomtangaza Barbara Gonzalez kuwa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo.
Kuna mwingine anaintwa Fatema Dewji ambaye alitangazwa hivi karibuni na Barbara kuwa ni mlezi wa timu yao ya wanawake ya Simba Queens, baadhi ya wadau wa soka waliibua maswali kadhaa.
Katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti, Fatema anasema ilimchukua miezi mitatu kuridhia kuwa mlezi wa Simba Queens ambayo sasa inafanya vizuri zaidi kwenye Ligi ya Wanawake.
“Nataka Simba Queens icheze Ligi ya Mabingwa Afrika Wanawake, ijulikane kidunia, hiyo ndiyo ndoto yangu,” anaeleza Fatema ambaye wiki kama nne zilizopita alitangazwa rasmi kuwa mlezi wa timu hiyo.
Fatema ambaye ni mdogo wa Mohammed ‘Mo’ Dewji, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, anasema alipoombwa kwa mara ya kwanza kuchukua jukumu la kuilea Simba Queens alikataa.
“Haikuwa kazi ndogo kwangu, niliwaza hivi itakuwaje kama unachukua jukumu hilo halafu huifanyi vizuri kutoka moyoni?
“Niliomba nipewe muda kufikiri, ukizingatia nina majukumu mengi kwenye kampuni ya MeTL Group, pia nafanya vitu vingine vingi, nilikaa miezi mitatu nikitafakari hadi kuamua kuwa mlezi wa Simba Queens,” anasema.
MO ALIMSAPOTI?
Fatema ambaye ni Mkurugenzi wa masoko kwa miaka 10 sasa licha ya kuwa na ndoto za kuwahamasisha wanawake kushiriki kwenye michezo, anasema kaka yake, Mo Dewji amekuwa akimpa changamoto.
“Mo yeye anataka tu Simba iende mbele, hayo ndiyo malengo yake hivyo kwenye Simba Queens niwe mimi au mtu mwingine anachokitaka ni malengo ya Simba kufika mbali yatimie,”.
Anasema Simba walipenda awe mlezi wa Simba Queens, wakamueleza na akajipa muda kwanza kabla ya kuridhia.
“Mo alinipa chalenji hiyo, yeye anachokitaka ni mafanikio ya timu tu,” anasema Fatema ambaye ndoto yake kubwa ni kuwaongezea uwezo wanawake kushiriki kwenye michezo.
Anasema alipoingia kuwa mlezi, Simba Queens ilikuwa na changamoto nyingi lakini kidogo kidogo wameanza kuzipunguza.
“Lengo ni kuwasaidia ili wafike mbali, unajua ukiwa mchezaji sio kutumia nguvu tu, inatakiwa hata akili yako iwe vizuri, nimekuwa nikizungumza mara kwa mara na wachezaji wa Simba Queens.
“Nafanya hivyo kujua wanakula nini, nini kinawatatiza na hata namna ya kupambana na presha ya mpira, hii ni muhimu sana kwa mchezaji japo wengi wetu huwa wanaangalia fiziki lakini kuna vitu vingi vinakwenda sambamba na mafanikio ya mchezaji na timu,”.
ACHUKIA UBAGUZI
Katika jambo ambalo Fatema halipendi kwenye michezo ni ubaguzi wa kuona wanaume ndiyo wanastahili zaidi kushiriki sekta hiyo ukilinganisha na wanawake.
“Wanawake wanacheza, hata mimi nimewahi kuwa mchezaji na mpaka sasa nacheza gofu na tenisi, lakini bado kuna ubaguzi katika ushiriki wa wanawake kwenye michezo, wanawake mara nyingi wanaonekana hawawezi kucheza.
“Na wakicheza kama soka huwa wanaonekana hawawezi kuwa na familia zao na maisha mengine nje ya soka, wakati si kweli.
“Tunataka kutoa ubaguzi huo na kuwapa nguvu si tu katika soka bali pia kwenye maisha yao kwani ukimsaidia mwanamke mmoja umesaidia jamii,” anasema.
Fatema anasema anaandaa mpango ambao anaamini utawashirikisha wanawake kwenye michezo tangu wakiwa wadogo.
“Nilianza kucheza nikiwa na miaka sita, ile ilinijenga na hadi hapa nilipo nguvu kubwa imetokana na michezo, hivyo naamini hata mabinti wakiingia kwenye michezo tangu wadogo itawajenga.
“Kuna mifano watoto wa kike wengi wanakuwa kwenye michezo na wanapofikisha miaka 12 au 13 wengi wao wanaacha, bado jamii kubwa inachukulia michezo ipo sana kwa ajili ya wanaume, wakati si kweli,”.
HAJAINGIA SIMBA QUEENS KWA BAHATI MBAYA
Kama ulikuwa hufahamu, basi Mwanaspoti linakufichulia ukweli wa Fatema kwenye michezo.
Anasema akiwa na miaka sita, baba yao alitaka familia nzima akiwa na kaka yake Mo Dewji washiriki michezo.
“Baba yetu ndiye alitusukuma sana kwenye michezo, unajua katika maisha ni muhimu kuwa na mshauri, hivyo baba yetu ndiye alikuwa mshauri wetu kwenye michezo.

“Nakumbuka nikiwa na miaka sita, wakati huo sijui nataka nini kwenye michezo, baba aliniongoza na aliweka umuhimu mkubwa sana kwenye michezo, familia yetu wote tumecheza,” anasema.
Fatema ambaye anasema amecheza michezo tofauti, ikiwamo tenisi na gofu ambako ana makombe 100 aliyowahi kushinda anasema baba yao alikuwa na nidhamu sana kwenye michezo.
“Alitaka na sisi tuwe hivyo, nakumbuka nilikuwa nikitoka shule nafanya ‘home work’ kisha naenda kucheza na usiku kocha alikuja nyumbani kunifundisha.
“Kila siku ilikuwa lazima nipige mipira 200, hata ukichoka hakuna kuomba kupumzika, nakumbuka wakati ule tukiwa wadogo unachoka hadi unatamani kukata tamaa, lakini baba alituwekea nidhamu alitaka kila mmoja wetu kuwa na nidhamu pia kwenye michezo.
Anasema michezo imemsaidia kwa kiwango kikubwa kuwa kiongozi mzuri.
“Hata nilipokubali kuwa mlezi wa Simba Queens, haikuwa hivi hivi, sababu nazifahamu changamoto za wanawake kwenye michezo, mimi pia nilipata changamoto hiyo tena nikiwa binti ambaye wakati ule mchezo wa gofu ulionekana kuwa wa wanaume zaidi,”.
“Nafahamu umuhimu wa michezo, na lengo langu sio tu katika Simba Queens bali kuwahamasisha watoto wa kike kuingia kwa wingi katika michezo, kuna umuhimu wa kuwa na mshauri ambaye lazima azungumze na wewe, akusimamie ili uzidi kufanya vizuri zaidi.
“Wakati nacheza, mshauri mkubwa kwangu alikuwa ni baba yangu na kocha, kipindi hicho kama nilivyosema sikufahamu umuhimu wa michezo, lakini washauri wangu walikuwa wanafahamu ndiyo sababu leo niko hapa, hivyo na mimi nataka nifanye hivyo kwa wanawake wenzangu,”.
AWAASA WAZAZI
Fatema anasema katika mpango wake wa kuwajengea wanawake kuingia katika michezo atatoa elimu pia kwa wazazi ambao wamekuwa na fikra kwamba mtoto wa kike hawezi kuingia kwenye michezo.
“Katika mkakati huo, nitaanza na soka kwa kuwa ndiyo mchezo unaopendwa zaidi nchini, kisha nitahamia kwenye michezo mingine, lengo ni kuwajengea uwezo wanawake kushiriki kikamilifu kwenye michezo yote,”.
“Lakini kama mwanamke, mwezi huu ni wetu, hivyo ni muhimu kuwa pamoja, kudumisha nguvu ya mwanamke katika jamii, tuwe kitu kimoja tusaidie na wengine,” anasema