Prime
Hamza, Camara waikoleza Dabi Juni 25

Muktasari:
- Hata hivyo, kwa upande wa Simba kupangwa kwa tarehe hiyo mpya, kumekuwa kama neema baada ya awali kuwa kwenye sintofahamu ya kuwakosa baadhi ya mastaa wa kikosi cha kwanza walikuwa katika hatihati ya kulikosa pambano hilo kama lingepigwa juzi Jumapili.
MASHABIKI wa soka nchini wameanza kuhesabu vidole kuhusiana na siku ya kupigwa Dabi ya Kariakoo iliyopangwa kuchezwa Juni 25 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam baada ya kuahirishwa mara mbili mfululizo Machi 8 na Juni 15.
Hata hivyo, kwa upande wa Simba kupangwa kwa tarehe hiyo mpya, kumekuwa kama neema baada ya awali kuwa kwenye sintofahamu ya kuwakosa baadhi ya mastaa wa kikosi cha kwanza walikuwa katika hatihati ya kulikosa pambano hilo kama lingepigwa juzi Jumapili.
Ipo hivi. Kusogezwa kwa mechi hiyo ya watani wa jadi Simba na Yanga kutoka jana Juni 15 hadi Juni 25 mwaka huu, kumeipa mzuka kikosi cha Fadlu Davids baada ya nyota watatu muhimu wa timu hiyo akiwamo kipa Moussa Camara na mabeki Abdulrazack Hamza na Shomari Kapombe kuthibitishwa kurejea kikosini.
Awali Simba ilikuwa na presha kubwa wakati mechi ilipotangazwa kupigwa Juni 15 baada ya awali kuahirishwa Machi 8 kutokana na Hamza kuwa na adhabu ya kadi tatu za njano , huku Camara alikuwa nje ya uwanja kwa muda baada ya kupata shida ya kifua katika mechi dhidi ya Singida Black Stars, lakini tayari kipa huyo ameanza mazoezi na yupo vyema kiafya kwa dabi hiyo ya Kariakoo.
Adhabu ya Hamza inaisha katika mechi ya KenGold inayopigwa kesho, hivyo kuwa na nafasi ya kurudi uwanjani kuanzia mechi ya Juni 22 dhidi ya Kagera Sugar kisha siku tatu baadae ataivaa Yanga ambayo ilishinda kwenye mchezo wa kwanza wa msimu huu iliyochezwa Oktoba 19, 2024.
Kwa upande wa Kapombe, aliyekuwa katika mapumziko ya wiki mbili kutokana na sababu za kiafya na uchovu wa misuli, naye anaripotiwa kuwa tayari ameanza kujifua upya na yupo mbioni kuwa fiti kwa ajili ya dabi hiyo.
Awali, taarifa kutoka ndani ya benchi la Simba zilieleza kuwa Hamza angekosa mechi ya Juni 15 kutokana na adhabu ya kadi, lakini baada ya mechi hiyo kusogezwa mbele na Bodi ya Ligi, kadi hizo sasa zitafutwa dhidi ya KenGold, hatua iliyopokelewa kwa matumaini makubwa na mashabiki wa klabu hiyo.
Hii inatokana na uwezo wa Hamza tangu ajiunge na timu hiyo msimu huu kutoka Supersport United ya Afrika Kusini akiunda ukuta mgumu sambamba Fondoh Che Malone na Chamou Karaboue wakishirikiana na Camara anayeongoza kwa clean sheet 17 kwa makipa wa Ligi Kuu hadi sasa.
Akizungumza na Mwanaspoti, Daktari wa Simba, Dk Edwin Kagabo lisema kikosi hicho kwa sasa hakina mchezaji yeyote majeruhi na kwamba nyota wote waliokuwa nje kwa matatizo ya kiafya wamerudi mazoezini.
"Mchezo wa mwisho tuliocheza dhidi ya Singida Black Stars, Camara alipata shida ya kifua, lakini tayari amerudi mazoezini na yupo fiti kabisa. Nouma (Valentin) naye alipata changamoto ndogo ila kwa sasa yupo sawa na wote wameanza mazoezi," alisema Dk Kagabo.
Daktari huyo aliongeza kwa kusema "Hatuna majeruhi kwa sasa. Wachezaji wetu wote akiwemo Moussa Camara, Mzamiru Yassin na Valentino Nouma wamerudi katika hali ya kawaida na wameanza kujifua. Kazi imebaki kwa kocha kuamua nani atatumika katika mechi zilizosalia ikiwamo dabi, lakini kwa upande wa afya, tupo vizuri."
Habari hii imeleta matumaini mapya kwa mashabiki wa Simba ambao walikuwa na wasiwasi kuhusu hali ya wachezaji wao muhimu, hasa ikizingatiwa kuwa mechi ya dabi si ya kawaida na mara zote huhitaji kikosi kamili na chenye morali ya hali ya juu.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka benchi la ufundi la Simba, wachezaji wote sasa wanafanya mazoezi kwa nguvu ili kuhakikisha wanawapa mashabiki wao furaha katika mechi hiyo muhimu itakayohitimisha msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mechi hiyo dhidi ya Yanga inatarajiwa kuwa ya ushindani mkubwa, hasa kwa kuwa timu zote zinawania heshima ya kuhitimisha msimu kwa ushindi kwenye pambano la hadhi ya juu zaidi nchini.
Simba imesaliwa na mechi tatu ikiwamo ya kesho dhidi ya KenGold, ile ya Juni 22 itakapoikaribisha Kagera Sugar na kumalizana na Yanga Juni 25 inayochuana nao kuwania ubingwa kwanio kwa sasa zimetanganishwa na pointi moja tu kileleni, Yanga ikiwa na 73 na Wekundu wakiwa na 72 kila moja ikicheza mechi 28. Mara ya mwisho kwa Simba kubeba ubingwa wa Ligi Kuu ilikuwa misimu mitatu iliyopita ikiubeba kwa mara nne mfululizo kabla ya Yanga kutawala pamoja na Kombe la Shirikisho.
Katika Dabi ya Kariakoo ya Ligi Kuu, Simba ilishinda mara ya mwisho Apr 16, 2023 ilipoichapa Yanga kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na Henock Inonga dk 2 na Kibu Denis dk 32, kisha kupoteza mara tatu zilizofuata zikiwamo za msimu wa 2023-2024 ilipochapwa 5-1 Novemba 5, 2023 , kisha kugongwa 2-1 Aprili 20, 2024 na Oktoba 19, 2024 ikalambwa tena 1-0 kwa bao la kujifunga la Kelvin Kijili.
KWA YANGA SASA
Kwa upande wa Yanga, Dabi hiyo ya Juni 25 itashuka Kwa Mkapa bila nyota watatu walioupiga mwigi katika pambano la duru la kwanza lililopigwa Oktoba 19 mwaka jana ambapo Simba ilipoteza kwa bao 1-0 lililotokana na beki wa timu hiyo, Kelvin Kijili kujifunga itawakosa baadhi ya mashine zake.
Stephane Aziz KI aliyekuwa na kismati ya kuitungua Simba hatakuwepo Juni 25 kwa vile ameuzwa na sasa anakipiga Wydad Casablanca ya Morocco, huku beki wa kulia, Yao Kouassi bado ni majeruhi hivyo hatalicheza pambano hilo, ilihali Kenneth Musonda ikielezwa naye bado hajakaa sawa kiafya.
Katika mechi ya kwanza, Aziz KI na Yao walianza kikosi cha kwanza wakati watani Simba wakilala kwa mara ya tatu mfululizo katika Ligi Kuu, huku Musonda akianzia benchi na kuingia kipindi cha pili.