Hii kiboko, Singida BS yapitisha fagio zito

Muktasari:

  • Pamba iliyopanda Ligi Kuu msimu ujao kutoka Ligi ya Championship ikiwa sambamba na KenGold, hivi karibuni ilitangaza kuunda benchi jipya la ufundi na kuanza kusajili wachezaji wapya huku ikiwashukuru wale wote waliopambana kuipandisha timu, japo mabosi wa klabu hiyo walitoa ufafanuzi juu ya suala hilo.

SINGIDA Black Stars imeamua. Klabu hiyo iliyokuwa ikifahamika kama Ihefu na kumaliza katika nafasi ya saba kwenye Ligi Kuu Bara iliyomalizika hivi karibuni, inaelezwa imekifanya kile kilichofanywa na Pamba Jiji kwa kuifumua timu nzima.

Pamba iliyopanda Ligi Kuu msimu ujao kutoka Ligi ya Championship ikiwa sambamba na KenGold, hivi karibuni ilitangaza kuunda benchi jipya la ufundi na kuanza kusajili wachezaji wapya huku ikiwashukuru wale wote waliopambana kuipandisha timu, japo mabosi wa klabu hiyo walitoa ufafanuzi juu ya suala hilo.

Lakini sasa unaambiwa, Singida imeamua kufyagia ikielezwa kuachana na karibu wachezaji wote, wiki kadhaa tangu ilivyowasafisha watu wa benchi la ufundi waliokuwa chini ya kocha Mecky Maxime aliyeibukia Dodoma Jiji.

Singida imeshawatangaza makocha watatu wa kuziba nafasi ya Maxime na wenzake, ikimrejesha nchini kocha mkuu Patrick Aussems aliyewahi kuinoa Simba kabla ya kutua AFC Leopards ya Kenya, Ramadhani Nsanzurwimo anayekuwa msaidizi na mchambuzi wa video na Marouene Sliman akiwa kocha wa viungo.

Aussems anatarajiwa kuwasili nchini leo Jumatatu tayari kuanza rasmi kazi kikosini hapo.

Baada ya hapo chanzo makini kutoka ndani ya klabu hiyo yenye maskani mjini Singida ikitokea Mbarali, Mbeya, kinasema mabosi wameamua kugeukia wachezaji wakiwafyeka karibu wote hata wale waliokuwa katika hesabu za kuwasajili akiwamo Serge Pokou aliyekuwa akiwindwa pia na Simba aliyetua Al Hilal ya Sudan.

Taarifa hizo zinasema kuwa, wachezaji wote walioitumikia timu hiyo katika Ligi Kuu msimu uliopita wameenda na maji isipokuwa wawili pekee waliobakishwa kwa ajili ya kuunda kikosi kipya cha msimu ujao.

“Tunaanza msimu tukiwa na wachezaji wengi wapya kwa sababu wale waliomaliza msimu tumemalizana nao kwa kiasi kikubwa,” alisema mtoa taarifa kutoka ndani ya timu hiyo na kuongeza:

“Wachezaji waliobaki ni wawili Kelvin Nashon na Mkenya Elvis Rupia, lakini tayari kuna maingizo mapya ambayo muda ukifika mtaanza kuona utambulisho wake.”

Chanzo hicho kinasema asilimia kubwa ya wachezaji wa Singida walimaliza mikataba mwishoni mwa msimu uliomalizika na benchi la ufundi linataka kuanza hesabu upya isipokuwa kubaki na nyota hao wawili tu, mmoja akiwa ni mzawa na mwingine wa kigeni.

Hii inamaanisha kina  Khumein Abubakar, Fikirini Bakari, Benson Mangolo, Faria Ondongo, Kenneth Kunambi, Vedastus Mwihambi, Benjamin Tanimu, Joash Onyango, Joseph Mahundi, Morice Chukwu, Ismail Mgunda, Raphael Daud, Manu Bola Labota, Paul Godfrey ‘Boxer’, Jaffar Kibaya, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Amade Momade na wengineo wamesepa.

Raphael Daud ameibukia Namungo, huku Ezekia Mwashilindi na Vedastus Mwihambi wakijiandaa kutambulishwa Tanzania Prisons, ilhali Khumein akitajwa kujiunga na Yanga.

Mtendaji Mkuu wa Singida, Kassano Jonathan, alilithibitishia Mwanaspoti taarifa hizo za fyagia fyagia klabuni, akisema: “Wachezaji tuliobaki nao ni wale, benchi la ufundi limeona linawahitaji waendelee na timu, ingawa siwezi kusema ni kina nani waliobaki. Muda ukifika itafahamika.”

“Lakini wale walioondoka wapo ambao mikataba  imemalizika na wengine tumefanya biashara ya kuwauza baada ya kufikia makubaliano mazuri tukiangalia matakwa ya mchezaji husika,” aliongeza Jonathan.

Baadhi ya nyota wapya wanaotajwa kujiunga timu hiyo ni Metacha Mnata na Zawadi Mauya kutoka Yanga na beki Antony Tra Bi Tra aliyekuwa akiwindwa na Simba.