Hii ndio Stellenbosch iliyoingia anga za Simba

Muktasari:
- Hadi sasa Stellenbosch imefanikiwa kutinga katika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuwatupa nje Mabingwa watetezi wa michuano hiyo Zamalek ya Misri.
Unaweza kusema ni kijana barobaro au vijana wa 2000 kutokana na umri wao kwenye soka tangu wabadilishwe jina kutoka Vasco Da Gama hadi kuitwa Stellenbosch FC.
Vijana hawa wameweza kujitengenezea jina kubwa ndani ya soka la Afrika Kusini tangu wafanikiwe kupanda daraja kutoka National Fisrt Division hadi Ligi Kuu ya DStv Premiership.

Mafanikio haya yalikuwa historia kwani Stellenbosch FC ikawa klabu ya kwanza kutoka mji wa Stellenbosch kushiriki katika ligi kuu ya Afrika Kusini.
Stellenbosch ni mji maarufu uliopo katika jimbo la Western Cape, Afrika Kusini, takriban kilomita 50 mashariki mwa Cape Town. Ni mji wa pili kwa ukubwa kati ya miji ya kale zaidi nchini Afrika Kusini baada ya Cape Town

Stellenbosch FC ilianzishwa baada ya kampuni ya Stellenbosch Academy of Sport (SAS) kuinunua klabu ya Vasco Da Gama, ambayo ilikuwa ikishiriki Ligi daraja la kwanza (National First Division). Uamuzi wa kuihamishia klabu hiyo mjini Stellenbosch ulilenga kuanzisha timu ya ushindani kutoka eneo ambalo awali halikuwa na mwakilishi katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini (DStv Premiership).

Msimu wa 2018/2019 ulikuwa wa kihistoria kwa Stellenbosch FC, baada ya kuongoza katika msimamo wa Ligi daraja la kwanza (National First Division) na kupanda daraja hadi DStv Premiership. Klabu hiyo ilivuna jumla ya pointi 56 katika mechi 30, ikimaliza kileleni mwa Ligi na kuwa klabu ya kwanza kutoka Stellenbosch kucheza Ligi Kuu.
Katika msimu wa kwanza kwenye ligi hiyo (2019/2020), Stellenbosch FC ilimaliza katika nafasi ya 10 kati ya timu 16, matokeo hayo yalithibitisha uwezo wa klabu hiyo mpya kuhimili ushindani wa timu kongwe kama Orlando Pirates na Kaizer Chiefs.
Msimu wa 2021/2022 ulikuwa wa mafanikio zaidi, ambapo Stellenbosch FC ilimaliza Ligi katika nafasi ya nne hivyo ikafuzu katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo imefika katika hatua ya nusu fainali baada ya kuiondosha Zamalek.

Kati ya vichocheo vya mafanikio haya ni uwekezaji katika maendeleo ya vijana kupitia Stellenbosch FC Academy, ambapo zaidi ya asilimia 60 ya wachezaji wa kikosi cha kwanza ni chipukizi waliotokea katika mfumo huo. Miongoni mwao ni Jayden Adams na Devin Titus waliowahi kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya vijana.
Klabu inamilikiwa na Stellenbosch Academy of Sport, taasisi inayosimamia michezo mbalimbali kwa weledi. Rob Benadie, Mkurugenzi Mtendaji wa klabu hiyo, amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha usimamizi bora, matumizi sahihi ya rasilimali, na kukuza vipaji vya ndani. Kwa kushirikiana na kocha Steve Barker, Stellenbosch imejenga utambulisho wa kucheza soka la aina yake.

Hadi sasa Stellenbosch imefanikiwa kutinga katika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuwatupa nje Mabingwa watetezi wa michuano hiyo Zamalek ya Misri.
Katika hatua ya nusu fainali Stellenbosch itavaana na Simba ambapo mechi ya kwanza itachezwa Aprili 20, 2025 Simba ikiwa nyumbani wakati mechi ya pili itachezwa Aprili 27, 2025 Afrika Kusini.