Prime
Huu hapa mtihani wa Kibu Denis katikati ya Waarabu

Muktasari:
- Lakini sasa, hadi kufikia hatua hiyo kiungo mshambuliaji wa Simba, Kibu Denis ‘Mkandaji’ amekuwa na msimu mzuriu akiwa na vita katikati ya timu za Waarabu katika mbio za ufungaji mabao.
MICHUANO ya Kombe la Shirikisho Afrika ipo hatua ya nusu fainali ambazo zinapigwa kesho Jumapili, wakati Simba itakapokuwa wenyeji wa Stellenbosch ya Afrika Kusini na CS Constantine ya Algeria itakuwa wageni wa RS Berkane ya Morocco. Timu hizo zitarudiana wikiendi ijayo kusaka timu mbili za kwenda fainali.
Lakini sasa, hadi kufikia hatua hiyo kiungo mshambuliaji wa Simba, Kibu Denis ‘Mkandaji’ amekuwa na msimu mzuriu akiwa na vita katikati ya timu za Waarabu katika mbio za ufungaji mabao.
Nyota huyo amekuwa sehemu ya mchango mkubwa wa Simba kufika nusu fainali ya michuano hiyo kutokana na kufunga mabao manne katika mechi kumi alizocheza timu hiyo kuanzia hatua ya mtoano, Mnyama akianzia raundi ya pili, makundi hadi robo fainali.
Kibu ambaye ametumika kwa dakika 771 katika michuano hiyo kwa msimuu, kwa sasa anafukuzana na wachezaji wa RS Berkane ya Morocco katika mbio za kuwania ufungaji bora.
Kibu alianza kufunga bao katika mechi ya marudiano ya raundi ya pili dhidi ya Al Ahly Tripoli ya Libya waliolazwa mabao 3-1 jijini Dar es Salaam baada ya kutoka suluhu mjini Tripoli, Libya.
Kisha akafunga mabao mawili dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia zilipoumana Kwa Mkapa na kuongeza jingine la tatatu katika hatua hiyo ya makundi walipoicharaza CS Contantine ya Algeria kwa mabao 2-0 ziliporudiana jijini Dar es Salaam baada ya awali Simba kulazwa mabao 2-1.
Wakati akiwa katika kufukuzana huko, pia ana mtihani wa kuhakikisha anafunga mabao mawili zaidi kufikisha matano ili kuwa juu ya kinara wa sasa Ismail Belkacemi wa USM Alger ambaye ana mabao matano.
Kitendo cha USM Alger kuishia hatua ya robo fainali, kinatoa mwanya kwa nyota wa timu za Simba, RS Berkane, CS Constantine na Stellenbosch kuwa na nafasi kubwa ya kumpiku mchezaji huyo.
Nyuma ya Belkacemi, kuna Ifeanyi Ihemekwele wa Enyimba mwenye mabao manne, naye hana uwezo wa kuongeza kwani timu yake imeshaondolewa mashindanoni.
Walio karibu kuyafikia mabao matano ni wachezaji watatu ambao kila mmoja ana mabao matatu, wawili wakicheza RS Berkane, Issoufou Dayo na Youssef Zghoudi, mwingine Kibu Denis wa Simba.
Kibu vita yake hiyo ni ngumu kwani akigeuka nyuma kuna nyota wengine watatu wanaotokea RS Berkane ambao ni Imad Riahi, Paul Bassene na Oussama Lamlaoui wenye mabao mawili kila mmoja. Nao wanakuja kwa kasi wakihitaji kuweka ufalme wao.
CS Constantine itakayocheza dhidi ya RS Berkane hatua ya nusu fainali, ina nyota watano kila mmoja mwenye mabao mawili ambao ni Brahim Dib, Zakaria Benchaâ, Dadi Mouaki, Abdennour Belhocini na Mounder Temine.
Katika orodha ya wenye mabao mawili, wapo Leonel Ateba na Jean Charles Ahoua wanaocheza Simba na Andre De Jong kutoka Stellenbosch.
Unaweza kujiuliza kwanini Kibu amefunga mabao manne, lakini katika orodha ya kuwania ufungaji bora ana mabao matatu, hiyo inatokana na bao moja alilofunga hatua ya mtoano dhidi ya Al Ahli Tripoli, halihesabiwi.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), mabao yanayokuwa kwenye hesabu za kuwania ufungaji bora, yanaanzia hatua ya makundi.
Msimu uliopita nyota wa Abdul Aziz Issah na John Atwi wa Dreams ya Ghana sambamba na Paul Bassene (RS Berkane) na Abduoulaye Kanou (USM Alger) walimaliza kam vinara wa mabao kila mmoja akifunga mabao manne, huku msimu wa 2022-2023, Fiston Mayele aliyekuwa Yanga aliibuka mfungaji bora wa michuano hiyo akifunga mabao saba, mbali na saba aliyofunga katika mechi za raundi ya awali.