Huyo Mwajanga ni tishio Championship

LICHA kuachwa kwa idadi ya mabao, lakini straika wa Mbeya Kwanza, Oscar Mwajanga ameweka rekodi na kuwafunika mastaa wote Championship, huku akiiwezesha timu yake kuwa nafasi ya nne kwenye msimamo.

Mwajanga amekuwa moto wa kuotea mbali kwa kuwatesa makipa kwa kufunga mabao matatu katika mechi moja ‘Hat triki’ na kufikisha mbili hadi sasa sawa na staa wa Biashara United, Boban Zirintusa raia wa Uganda.

Kama haitoshi nyota huyo amefunga bao kwenye mechi tano mfululizo kati ya sita ilizocheza Mbeya Kwanza na kufikisha mabao 14 akiachwa mawili na kinara Willy Edgar wa Ken Gold.

Mwajanga alifunga dhidi ya Mbuni, Copco, Mbeya City, TMA, na Ruvu Shooting na kuwa katika orodha ya wachezaji watatu vinara wa mabao kwenye ligi hiyo.

Juzi akiiongoza timu hiyo waliizabua Stand United mabao 4-1, huku straika huyo akiweka matatu ikiwa ni mara ya pili kufanya hivyo tangu alipowafunga TMA kwenye ushindi wa 3-1 na kuifanya Mbeya Kwanza kufikisha pointi 50.

Akizungumzia mwenendo wa nyota huyo, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Michael Mnyali alisema mchezaji huyo angekuwa amefika mbali lakini raundi ya kwanza hakuwa na nafasi mbele ya Ramadhan Kapera aliyejiunga na Geita Gold.

Alisema baada ya ushindi dhidi ya ‘Chama la Wana’ hesabu zote zipo kwenye mchezo ujao na Biashara United wakihitaji alama tatu ili kurejesha matumaini.

“Mchezo ujao ndiyo fainali kubwa kwetu, tunahitaji alama tatu ziturejeshe upya katika hesabu za kuitafuta Ligi Kuu, niwapongeze vijana kwa kazi nzuri,” alisema.