JKT Tanzania, Tabora United mzigoni tena

Muktasari:
- Maafande wa JKT Tanzania na Tabora United ni pekee za Ligi Kuu zitakazoshuka uwanjani leo kuisaka tiketi hiyo ya 16 Bora ya michuano hiyo ambayo bingwa wake, inakata tiketi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
KIVUMBI cha Kombe la Shirikisho (FA) kinaendelea tena leo kwa mechi sita tofauti, wakati timu 12 zitakapokuwa zikiwania kusaka tiketi ya 16 Bora kuungana na timu zilizotangulia kutokana na mechi zilizopigwa jana Jumapili kwenye viwanja tofauti.
Maafande wa JKT Tanzania na Tabora United ni pekee za Ligi Kuu zitakazoshuka uwanjani leo kuisaka tiketi hiyo ya 16 Bora ya michuano hiyo ambayo bingwa wake, inakata tiketi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Tabora United iliyohamisha pambano hilo hadi Jamhuri, Dodoma kutokana na Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi kufungiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutokana na kutokukidhi matakwa, itakuwa wenyeji wa maafande wa Transit Camp inayoshiriki Ligi ya Championship. Mechi itapigwa saa 10 jioni.
JKT yenyewe itakuwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamahyo, Dar es Salaam kuipokea Biashara United inayoburuza mkia katika Ligi ya Championship.
Mechi nyingine zinazopigwa katika michuano hiyo itazikutanisha timu zilizopo Ligi ya Championship, First League na Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL).
Ratiba inaonyesha kuwa mechi sita zinapigwa leo kuanzia saa 10:00 jioni na Mbeya Kwanza itakuwa nyumbani kuikaribisha Mambali Ushirikiano, huku Polisi Tanzania na Songea United zitaonyeshana kazi mjini Moshi na vinara wa Championship na mabingwa wa zamani wa Ligi Kuu 1999 na 2000, Mtibwa Sugar itakwaruzana na Towns Stars huko Manungu, Turiani mkoani Morogoro.
Mechi ya mwisho itakuwa ni Girrafe Academy dhidi ya Green Warriors, mbali na zile za maafande wa JKT Tanzania dhidi ya Biashara United na ile ya Tabora United itakayovaana na Transit Camp.
JKT Tanzania na Tabora United zikimalizana na mechi hizo za KOmbe la Shirikisho, zitakutana zenyewe katika mchezo wa Ligi Kuu utakaopigwa Ijumaa ijayo ambapo bado haujafahamika utapigiwa wapi kwani mabosi wa Tabora wametoa taarifa watautangaza uwanja utakaotumika baadae.
Vigogo wa soka nchini Simba na Yanga, zenyewe zitacheza mechi za hatua hiyo ya 32 Bora wiki ijayo mara baada ya Dabi ya Kariakoo itakayopigwa Machi 8 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Simba ndio itakayokuwa ya kwanza kuikaribisha TMA Stars ya Arusha Machi 11 na siku inayofuata, itakuwa zamu ya Yanga kuikabili Wagosi wa Kaya, Coastal Union wakikumbushia fainali za mwaka 2022 iliyopigwa jijini Arusha na timu hizo kufunga mabao 3-3 katika dakika 120 kabla ya penalti 4-1 kuipa Yanga ubingwa ikiinyang'anya Simba na tangu hapo haijauachia ubingwa huo.
Yanga ndio watetezi wa taji hilo wakilitwaa baada ya kuifumua Azam FC kwa mikwaju ya penalti baada ya dakika 120 kumalizika kwa suluhu kwenye fainali iliyopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, likiwa pambano la kwanza la fainali ya Shirikisho kupigwa visiwani humo.
Ratiba ilivyo 32 Bora Leo, Jumatatu
Mbeya Kwanza v Mambali Ushirikiano (Saa 10:00 jioni)
Polisi Tanzania v Songea United (Saa 10:00 jioni)
Mtibwa Sugar v Towns Stars (Saa 10:00 jioni)
Girrafe Academy v Green Warriors (Saa 10:00 jioni)
JKT Tanzania v Biashara United (Saa 10:00 jioni)
Tabora United v Transit Camp (Saa 10:00 jioni)
Mar 11, 2025
Simba v TMA Stars
Mar 12, 2025
Yanga v Coastal Union