Kakolanya asimamishwa Namungo FC

Muktasari:
- Kakolanya anaitumikia Namungo kwa mkopo msimu mmoja akitokea Singida Black Stars ambapo mkataba wake na Singida Black Stars unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu.
UONGOZI wa Namungo umethibitisha kumsimamisha kipa wao, Beno Kakolanya kwa kile kinachodaiwa ni utovu wa nidhamu huku mchezaji huyo akisubiri hatma yake baada ya suala lake kupelekwa kamati ya maadili.
Kakolanya anaitumikia Namungo kwa mkopo msimu mmoja akitokea Singida Black Stars ambapo mkataba wake na Singida Black Stars unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mratibu wa Namungo, Ally Suleiman, alisema: “Tumempeleka kamati ya maadili ambayo itakaa na mchezaji kwa ajili ya mazungumzo kabla ya kutoa hukumu, lakini hadi hivi sasa hayupo pamoja na timu, ameondolewa hadi atakapoitwa na kamati.
“Shida kubwa iliyotufanya tumuondoe kikosini ni suala la utovu wa nidhamu. Kwa sasa ifahamike kuwa Kakolanya hayupo pamoja na timu.”
Mwanaspoti lilimtafuta Kakolanya ambapo alisema: “Siwezi kuzungumza chochote kile na hakuna sehemu nimelizungumzia hilo, naomba kupewa muda.”
Mara ya mwisho kwa kipa huyo kukaa langoni ilikuwa Februari 5 kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Tabora United ugenini ambapo Namungo ilikubali kichapo cha mabao 2-1.
Tangu ajiunge na timu hiyo mwanzoni mwa msimu huu, Kakolanya amecheza mechi nane za ligi akishuhudia ikishinda moja, sare moja na kupoteza tano.
Matokeo ya mechi hizo ni Tabora 2-1 Namungo, KenGold 2-3 Namungo, Kagera Sugar 1-1 Namungo, Namungo 0-2 Yanga, Mashujaa 1-0 Namungo, Singida BS 2-0 Namungo, Dodoma Jiji 1-0 Namungo na Namungo 0-2 Dodoma Jiji.