KenGold waitana fasta kumalizia Ligi

Muktasari:
- Kapilima aliliambia Mwanaspoti jana kuwa wachezaji wote wanatarajiwa kuingia kambini Juni 10 kuweka mikakati ya mechi zilizobaki ili kufunga msimu na kuanza maandalizi mapya ya Ligi ya Championship.
LICHA ya kuwa timu ya kwanza kushuka daraja msimu huu, huku ligi ikiwa haijamalizika, kocha wa KenGold, Omary Kapilima amewaita kambini fasta wachezaji wote kujiandaa na mechi za mwisho za kufungia msimu ikiwamo dhidi ya Simba itakayopigwa Mbeya, Juni 18.
Kapilima aliliambia Mwanaspoti jana kuwa wachezaji wote wanatarajiwa kuingia kambini Juni 10 kuweka mikakati ya mechi zilizobaki ili kufunga msimu na kuanza maandalizi mapya ya Ligi ya Championship.
Beki huyo wa zamani aliyetamba na Majimaji, Yanga, Mtibwa Sugar na Taifa Stars alisema licha ya timu hiyo kushuka daraja, sio kigezo cha kubweteka kwa mechi zilizosalia, hivyo mikakati ni kuhakikisha wanamaliza na kuilinda heshima yao.
“Kwa sasa hatuna cha kupoteza kwa sababu hakuna kinachoweza kutubadilisha au kututoa hapa tulipo leo. Tunachokipambania ni kulinda heshima, licha ya kutambua tunakutana na mechi ngumu na wapinzani wanauhitaji wa pointi tatu,” alisema Kapilima.
Alisema licha ya mechi dhidi ya Simba kwa sasa itachezwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi na kama benchi la ufundi na wachezaji wamekubaliana na mabadiliko hayo.
Timu hiyo ilianza msimu na KochaFikiri Elias ingawa alijiuzulu mwenyewe kutokana na mwenendo mbaya Septemba 17, 2024 kisha baada ya hapo akaiongoza Jumanne Challe aliyeipandisha Ligi Kuu hadi Oktoba 22, 2024, alipoichukua Kapilima.
Kikosi hicho kimeshuka daraja na msimu ujao kitashiriki Ligi ya Championship kutokana na kutokuwa na mwenendo mzuri kikiburuza mkiani na pointi 16.