Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kinachoitesa Dodoma Jiji misimu mitano Ligi Kuu

Muktasari:

  • Timu hiyo iliyopanda Ligi Kuu msimu wa 2020-2021 baada ya kuwa vinara wa Kundi A katika Ligi Daraja la Kwanza (sasa Championship) 2019-2020, haijawahi kurudia iliyoyafanya msimu wao wa kwanza jambo linalowafanya kuendelea kuwa na deni huku upepo ukibadilika.

KUFIKISHA pointi 44 kwenye Ligi Kuu Bara, imekuwa changamoto kubwa sana kwa Dodoma Jiji ambayo huu ni msimu wake wa tano inashiriki ligi hiyo.

Timu hiyo iliyopanda Ligi Kuu msimu wa 2020-2021 baada ya kuwa vinara wa Kundi A katika Ligi Daraja la Kwanza (sasa Championship) 2019-2020, haijawahi kurudia iliyoyafanya msimu wao wa kwanza jambo linalowafanya kuendelea kuwa na deni huku upepo ukibadilika.

Katika kuzisaka pointi hizo 44 ambazo ilimaliza nazo msimu wa 2020-2021, Jumatano hii Dodoma Jiji itaikaribisha Kagera Sugar kwenye Dimba la Jamhuri, mkoani Dodoma kwenye mwendelezo wa Ligi Kuu Bara, mechi ikipangwa kuchezwa saa 1:00 usiku.

Dodoma Jiji inaingia uwanjani ikiwa na deni ambalo waliliacha msimu huo wa kwanza kwao kushiriki Ligi Kuu Bara 2020-2021 na ilimaliza nafasi ya nane kwa kukusanya pointi 44.

Pointi hizo walizipata kutokana na kucheza mechi 34 tofauti na sasa itacheza mechi 30 kumaliza msimu, lakini kama ikizichanga vizuri karata zake, inaweza kuzifikia na kuzivuka, hivyo kuweka rekodi mpya.

Tangu msimu huo, Dodoma Jiji si tu kushindwa kufikisha pointi 44, bali haijawahi kumaliza ligi nafasi ya juu zaidi ya nane kitendo ambacho kinaonekana timu hiyo haina mwendelezo mzuri.

Msimu uliopita, timu hii iliepuka kidogo kucheza 'Play-Off', baada ya kumaliza nafasi ya 12 na pointi zake 33 kutokana na kushinda michezo minane, sare tisa na kupoteza 13. Nafasi hiyo ni ya chini zaidi katika ushiriki wao wa ligi kuu.

Takwimu zinaonyesha msimu wa pili kwao 2021-2022, timu hiyo ilishuka kiwango na kujikuta ikimaliza ligi nafasi ya 11 ikikusanya pointi 35 kwenye mechi 30, huku 2022-2023 ikirekebisha makosa yao na kupanda hadi nafasi ya tisa kwa kumaliza ligi ikiwa na pointi 37.

Timu hiyo inayonolewa na Kocha Mecky Maxime, kwa sasa ipo nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi ikikusanya pointi 31, huku hesabu zikiwa kwenye mechi tano zilizobaki ili kubaki salama na kushiriki tena ligi kwa msimu wa sita mfululizo tangu kupanda kwao daraja.

Katika mechi hizo tano, Dodoma Jiji ikishinda zote itakusanya pointi 15 na kuwafanya jumla kuwa nazo 46, mbili zaidi ya ilizomaliza nazo msimu wao wa kwanza. Hata hivyo, haitakuwa kazi rahisi kutokana na ugumu wa mechi zilivyo mbele yao.

Hadi sasa, unaweza kusema Dodoma Jiji imepanda kidogo kiwango tofauti na msimu uliopita, hivyo inahitaji pointi tatu pekee kufikisha 34 kudhihirisha ubora wao huo.

Katika mechi tano zilizobaki, mbili pekee itacheza nyumbani dhidi ya Kagera Sugar (Aprili 9) na Singida Black Stars (Mei 21). Kisha zingine tatu ugenini dhidi ya KMC (Aprili 18), Azam (Mei 13) na Yanga (Mei 25).


TATIZO LIPO HAPA

Msimu uliopita, timu hii ilifunga mabao 19 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 32, katika michezo 30 iliyocheza, japo hadi sasa imefunga 27 na kuruhusu 35, kwenye mechi 25, ikionyesha haina uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa huku tatizo kubwa likionekana ndani ya misimu hiyo miwili safu yao ya ulinzi haipo vizuri ikiruhu mabao mengi kuliko inayofunga timu hiyo.

Msimu huo wa 2023-2024, nyota aliyekuwa anaongoza kwa mabao ndani ya kikosi hicho alikuwa Hassan Mwaterema aliyefunga manne, ingawa safari hii mambo yamekuwa magumu kwake hadi sasa baada ya kutupia bao moja tu.

Ukweli ni kwamba changamoto kubwa ya Dodoma Jiji msimu huu ni katika eneo lake la ulizi na inashika nafasi ya nne kwa timu zilizoruhusu mabao mengi zaidi ambayo ni 35, nyuma ya KMC (36), KenGold (42) na Fountain Gate (43).

Msimu uliopita ilikuwa nafasi ya tisa kwa timu zilizoruhusu mabao mengi zaidi (32), nyuma ya vinara Mtibwa Sugar (54), Tabora United (41), KMC FC na Fountain Gate (39), Geita Gold (38) na Singida Black Stars iliyoruhusu 36.

Timu nyingine zilizoruhusu mabao mengi zaidi msimu uliopita ni Tanzania Prisons (35) na maafande wenzao wa Mashujaa FC walioruhusu 33, hivyo kitendo cha Dodoma Jiji kuruhusu 35 hadi sasa ni ishara tosha eneo la ulinzi limekuwa changamoto.

Msimu huu ndani ya kikosi cha Dodoma Jiji, nyota anayeonekana kuibeba zaidi timu hiyo hadi sasa ni Paul Peter aliyeifungia mabao manane ya Ligi Kuu Bara, akifuatiwa na Iddi Kipagwile aliyehusika na sita baada ya kufunga manne na kuasisti mawili kati ya 27 ya kikosi hicho kizima.

Akizungumzia kiwango cha timu hiyo na michezo iliyobaki, Kocha wa Dodoma Jiji, Mecky Maxime amesema ushindani umekuwa mkubwa ingawa changamoto kubwa anayopambana nayo kwa michezo mitano ijayo ni eneo la ulizi, kutokana na mawasiliano mabovu yanayosababisha kuruhusu mabao mengi zaidi.

"Tunakosa nidhamu ya kujilinda, hali inayosababisha kufanya makosa yanayowanufaisha wapinzani wetu, ni changamoto kubwa sana kwetu, ila sisi kama benchi la ufundi tunapambana nalo kwa sababu sio suala la kubadilisha kwa siku moja au mbili," amesema Maxime.


TAKWIMU ZA MISIMU MITANO

MSIMU: 2020-2021

NAFASI: 8

POINTI: 44

MECHI: 34


MSIMU: 2021-2022

NAFASI: 11

POINTI: 35

MECHI: 30


MSIMU: 2022-2023

NAFASI: 9

POINTI: 37

MECHI: 30


MSIMU: 2023-2024

NAFASI: 12

POINTI: 33

MECHI: 30


MSIMU: 2024-2025 (Bado mechi tano)

NAFASI: 7

POINTI: 31

MECHI: 25