Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kipa JKU atajwa Dodoma Jiji

TEMBO

Muktasari:

  • Chanzo kutoka ndani ya Dodoma Jiji kimeliambia Mwanaspoti, awali kocha huyo alitajiwa jina la Ally Salim kutoka Simba, lakini akataka kumuona kwanza ajiridhishe zaidi kabla hajafanya uamuzi.

ZIKIWA zimesalia takribani siku mbili kabla ya kufika Septemba 7, 2025 litakapofungwa dirisha la usajili, taarifa kutoka ndani ya Dodoma Jiji zinaeleza kocha wa timu hiyo, Vincent Mashami anaangalia uwezekano wa kuongeza nguvu langoni, akimuulizia kipa Ahmed Issa Haji wa JKU Zanzibar.

Chanzo kutoka ndani ya Dodoma Jiji kimeliambia Mwanaspoti, awali kocha huyo alitajiwa jina la Ally Salim kutoka Simba, lakini akataka kumuona kwanza ajiridhishe zaidi kabla hajafanya uamuzi.

Hata hivyo, wakati mchakato ukiendelea, kocha huyo ameonekana kuridhishwa kwa kiasi fulani na kipa wa JKU aliyemshuhudia katika michuano ya Tanzanite Pre-Season International inayoendelea kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Babati mkoani Manyara.

Haji aliyetwaa Tuzo ya Kipa Bora wa Kombe la Muungano 2025, hivi karibuni aliliambia Mwanaspoti ameamua kubaki JKU licha ya kupokea ofa tatu kutoka timu za KVZ, Mwembe Makumbi na Mafunzo zote za Zanzibar, akisubiri usajili wa dirisha dogo akiwa na malengo ya kucheza Ligi Kuu Bara.

"Kocha anataka maboresho yafanyike kwenye eneo la golikipa na kuna mapendekezo kadhaa anayo, hivyo uongozi unayafanyia kazi kwa haraka kabla ya usajili kufungwa.

"Siku zote kocha anapendekeza kisha uongozi unafanya usajili kulingana na mapendekezo yake, hivyo lolote linaweza kutokea kabla dirisha halijafungwa," kilisema chanzo hicho.

Mwanaspoti limezungumza na kocha Mashami kutaka kufahamu kuhusu taarifa hizo na anavyokiona kikosi chake wapi kinahitaji maboresho zaidi kabla ya msimu kuanza.

"Siwezi kusema timu haijasajili vizuri, uongozi umepambana kusajili wachezaji wazuri na hata wale waliokuwa mwanzo ni wazuri pia.

"Lakini kuna sehemu zina upungufu bado hatujaweka mambo vizuri, siwezi kusema labda katika ushambuliaji au kiungo, bali tunaendelea kuangalia kupitia mechi hizi za Pre-Season, baada ya hapo tutafahamu wapi panahitaji kuongezewa nguvu."

Makipa waliopo katika kikosi cha Dodoma Jiji ni Daniel Mgore na Mohammed Hussein waliokuwa hapo tangu msimu uliopita huku Castor Mhagama akiwa usajili mpya akitokea Geita Gold.